January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

‘Stahili’ aliyotumia Rais Samia kuinua kielimu jamii ya Wamasai

Na Markus Mpangala,TimesmajiraOnline,Arusha

SERIKALI ya Awamu ya Sita inapigania kwa nguvu maarifa na ufundi kuhakikisha sekta ya elimu inapata mabadiliko makubwa ikiwemo kusogeza huduma hiyo ili kuwakomboa watoto na wazazi wote nchini.

Hivi karibuni kumekuwa na taarifa kutoka kwa viongozi wa Mikoa na Wilaya kwa kushauriana na Wakurugenzi wao walibainisha umuhimu wa Wannafunzi kupewa vyakula shuleni,wazazi kuwapeleka watoto wenye umri wa kwenda shule.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas ilisikika hivi karibuni wakati akizungumzia hali ya udumavu kwa mkoa wake na kusisitiza suala la malezi bora ya watoto pamoja na wanafunzi kupewa vyakula wawapo shuleni kuwa ni jambo nyeti kwa Taifa.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, Filberto Sanga alisisitiza agizo la wanafunzi kupewa vyakula shuleni na kuhakikisha mazingira yao ya kusoma yanakuwa bora zaidi.

Kauli ya viongozi hao wawili zinafanana na zile zilizotolewa hivi karibuni na Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Kanali Wilson Sakulo ambaye alisisitiza umuhimu wa wazazi kuwapeleka watoto shuleni na kuhakikisha wanashirikiana na Serikali ya Awamu ya Sita kusimamia elimu ya wototo wao wakati akizungumza na wananchi waliohudhuria ufunguzi wa shule ya Awali na Msingi ya Omom Preci iliyopo Kata ya Enguserosambu wilayani humo.

Kauli zote hizo zimetoka kwa wawakilisha wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Zinadhihirisha msimamo wa serikali ya Awamu ya Sita ambapo hivi karibuni Rais Samia alitoa hotuba inayozungumzia elimu na maadili ndani ya familia. Kimsingi suala la maadili linaendana na sekta ya elimu.

Rais Samia alisistiza kuwa wanafunzi wanatayarishwa wakiwa wadogo kuwa viongozi kwa kuheshimu,kuzingatia na kujali elimu kama ufunguo wao wa maisha.

Wanafunzi wa ngazi zote kuanzia shule za Msingi na Sekondari ni mahali ambako wanatakiwa kupata chakula ili waweze kuondokana na hali ya udumavu pamoja na kutumia maarifa na akili zao kufikiria masuala ya elimu. Mahali penye njaa hapana adabu na ndiyo chanzo cha baadhi ya jamii kukimbia elimu pamoja na wimbi la utoro shuleni.

Kwa upande wake Mshauri Mwelekezi wa Shirika la Tanzania Heritage Foundation linalofadhili shule ya Omom Preci, Arpakwa Sikorei alisema kumekuwa na mwamko mdogo wa elimu kwa jamii ya Kimaasai, lakini halikuwa tatizo lisilotatuliwa na kwamba kwa vile Mkuu wa Wilaya Kanali Wilson Sakulo alikuwapo hapo, ni ushahidi kuwa serikali imepanga mikakati bora kuhakikisha wananchi wote wanapata elimu.

Akaongeza kuwa njia ya kwanza ni kuhakikisha Serikali ya Awamu ya Sita inadumisha mipango ya kujenga vyumba vipya vya Madarasa kwani inawasaidia wanafunzi na wazazi.

“Changamoto hii ilikuwa kubwa huko zamani, lakini Rais Samia Suluhu Hassan amefungua njia na kuongeza nguvu kwa wadau kushirikiana na serikali kuhakikisha jamii ya Kitanzania inapata elimu.

Wamaasai nanyi simameni mstari wa mbele kuhakikisha mnakuwa pamoja na wengine kwenye elimu, kwetu iwe somo na kusaidiana na serikali kupata chakula shuleni, ninyi mnakula nyama kwa wingi na boresheni afya kwa kuhakikisha watoto wenu wanakula shuleni na kupata elimu madhubuti,” alisema Sikorei.

Inaelezwa kuwa serikali ya Awamu ya Sita imepanga kuhakikisha watoto wanapata elimu bila kuwa na visingizo vyovyote kwa vile ni bure.

Serikali ya Awamu ya Sita imesisita kuwa hakuna mtoto wa yeyote atakayeachwa nyuma na hivyo itahakikisha kila mtoto mwenye kigezo cha kwenda shule anajiunga pasipo wasiwasi.

Hii inadhihirisha kuwa Kanali Sakulo anaelewa hali ya jamii ya Ngorongoro, na kwamba bila kujali mapenzi makubwa ya jamii ya Kimaasai kwenye ufugaji, bado nafasi yao katika elimu iko palepale. Kwa kuzingatia hilo Serikali imeshirikiana na kila mdau anayejitokeza kuunga mkono shughuli mbalimbali za kuimarisha sekta ya elimu.

Vilevile vibali vya ujenzi wa shule, ardhi na kuwezeshwa kwa shughuli za kiufundi zinazotolewa na Serikali ni ushahidi kuwa Rais Samia amechukua mkondo wa kuhakikisha kila jamii inafikiwa na kupewa stahiki zao kwa mujibu wa Katiba.

Serikali ya Awamu ya sita imetambua kuwa wadau wa elimu wana nafasi kubwa ya kutoa mchango, ni sababu hii inaunga mkono juhudi za ujenzi wa shule za Awali na Msingi mahali popote pale ambako kunawawezesha wananchi kupata elimu.

Wakati Serikali inapambana kuhakikisha sekta ya elimu inaondolewa kero zote ni dhahiri wadau wake wanatakiwa kushiriki na kuwa sehemu ya mafanikio na maendeleo makubwa ya sekta hiyo.

Serikali itafanya kila juhudi na kuhakikisha inafika kila sehemu kwa sharti la wadau kuwa sehemu ya juhudi hizo. Wadau wa elimu wanatakiwa kutumia nguvu na maarifa yao kuungana na Serikali ili kuwawezesha wananchi kupata elimu.

Duru za kiserikali zimebainisha kuwa Rais Samia amesimama kidete kwenye suala la elimu.

Pia ametoa mwongozo kila kiongozi ahakikishe anasimama kidete kwenye sekta ya elimu pamoja na kutekeleza mipango yote ya serikali.

Ni sababu hii inawafanya wasaidizi wake kwenda bega kwa bega na wadau wa elimu ili kurahisisha shughuli za serikali ya Awamu ya Sita na kuwajengea uelewa na umuhimu wa elimu.

Jamii ya Kimaasai ni miongoni mwa zile ambazo zinahitaji kusogezewa huduma nyingi na muhimu ili kupata ubora wa maarifa na juhudi zao katika kuleta maendeleo ya Taifa letu.

Ni jamii ambayo imejengewa misingi imara ya kuheshimu viongozi wao, ndiyo maana wameunga mkono juu ya mpango wa Serikali ya Awamu ya Sita kuhakikisha inashirikiana na wadau wao kusogeza huduma za elimu.

Ni dhahiri mpango wa serikali kuchochea mwamko wa elimu kwa kila jamii utazaa matunda kwani wadau wameitika wito na kushiriki kwa dhati.Baruapepe; mawazoni15@gmail.com/