April 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Miaka mitatu ya Rais Dkt. Samia na mikakati ya maendeleo ya Jotoardhi

Na Penina Malundo, TimesmajiraOnline,Dar

TANZANIA imezindua maandalizi ya kuandaa Kongamano la 10 la Jotoardhi Afrika (ARGeo-C10) ambalo litafanyika kuanzia Novemba 11 hadi 17, 2024 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.

Kongamano hilo lilikubaliwa, Mwaka 2022 na Rais Samia Suluhu Hassan, kufanyika nchini kwa mara ya pili baada ya ombi la Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP).

Rais Samia amekubali kongamano hili kufanyika nchini kwa sababu lina manufaa mengi kwa Taifa na Watanzania kwa ujumla.

Tafiti zilizopo zinaonesha kuwa Tanzania inaweza kuzalishaji megawati 5,000 za umeme wa jotoardhi, na kwa sasa Tanzania inatekeleza miradi mbalimbali ambayo inatarajiwa kuzalisha megawati 200 ifikapo mwaka 2027.

Uzinduzi huo umefanywa jana jijini Dar es Salaam na Kamshina wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga, ambapo amesema kongamano hilo la jotoardhi litahusuisha nchi 50 zikiwemo wanachama wa ARGeo ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Ethiopia na Djibouti.

Anasema katika kongamano hilo zaidi ya watu 1,000 wa kada mbalimbali zinazohusiana na sekta hiyo muhimu katika kuzalisha nishati safi na salama wanatarajiwa kushiriki.

Mhandisi Luoga amesema kongamano hilo ni muhimu kwa Tanzania kutokana na kuwa na rasilimali nyingi za jotoardhi, hivyo matumaini yao ni kuwa washiriki wataweza kujifunza na kubadilishana taaluma.

Anasema Serikali kupitia Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC) itashirikiana na UNEP kuhakikisha kongamano hilo muhimu linafanikiwa kwa kiwango kikubwa, ili dhamira ya Serikali kuongeza nishati jadidifu inafikiwa.

“Novemba 11 hadi 17, 2024 Tanzania itakuwa mwenyeji wa kongamano la jotoardhi ambalo litakutanisha wataalam, wawekezaji, wafanyabiashara na viongozi mbalimbali ambao watapata nafasi ya kuchochea kasi ya uzalishaji nishati hii,” amesema na kuongeza;
“Tafiti zilizopo zinaonesha Tanzania inaweza kuzalishaji megawati 5,000 za umeme wa jotoardhi na kwa sasa wanatekeleza miradi mbalimbali ambayo inatarajiwa kuzalisha megawati 200 ifikapo 2027, hivyo kusaidia nchi kukabiliana na changamoto ya umeme,” amesema.

Aidha, amesema rasilimali ya jotoardhi ilianza kufanyiwa utafiti tangu mwaka 1970, hivyo kwa sasa wanaendelea na utekelezaji wa kuzalisha kupitia TGDC ambapo wameanza kwenye baadhi ya maeneo kati ya 51 yanayoweza kuzalisha nishati hiyo.

“Tuna maeneo matano ambayo tumeyaainisha kwa ajili ya uzalishaji wa nishati ya jotoardhi ambayo ni Ngozi tutazalisha megawani 70, Kiejo Mbaka megawati 60, , Natron megawati 60, Songwe megawati tano na Ruoyi Kisaki megawati tano, hadi kufikia megawati 200,” amesema.

Mhandisi Luoga amesema pamoja na kongamano hilo kukutanisha wataalam mbalimbali, pia sekta binafsi na wananchi wa kawaida watanufaika kwa siku tano za kongamano pamoja na taasisi mbalimbali za kifedha ili ziweze kupata taarifa ya fursa ya uwepo wa jotoardhi nchi ili waweze kuwekeza.

Amesema kuna maeneo ambayo yanaweza kuzalisha umeme huo nchini kwa takribani maeneo 51, ambayo yanaweza kuzalisha kiasi cha megawati 5,000.

“Sera ya Nishati nchini, inataka kutumia vyanzo mchanganyiko wa kuzalisha nishati ili kuwa na umeme wa uhakika, nchi yetu inazalisha umeme kwa sasa kwa kutumia maji,gesi,Jua pamoja na Jotoardhi,”amesema na kuongeza

“Sasa tunataka kutumia Jotoardhi hii katika mikakati ya kuhakikisha tunakuwa na umeme wa uhakika na usalama wa umeme kwa nchi yetu bila kuathiri shughuli zozote za kiuchumi kwa nchi yetu,”amesema.

Amesema tumekaribisha kongamano hilo kwa Tanzania kwa sababu nchi inaenda kufunguka na kupata mafanikio makubwa,kwani nchi yetu inavigezo vya kufanyika kwa kongamano hili.

”Tukumbuke mwaka 2014, Tanzania tulikaribisha kongamano la 5 ambapo kipindi tunakaribisha kongamano hilo ndo tulikuwa tunatambulisha Kampuni Tanzu ya kusimamia uendelezaji wa Jotoardhi nchini,”amesema na kuongeza

”Rasilimari hii ilianza kufanyiwa utafiti tangu mwaka 1970 ndo ilianza kufanyiwa utafiti chini ya Shirika la Umeme nchini( Tanesco) ambapo ilipofika mwaka 2014 ndipo Serikali ilipoamua kuanzisha Taasisi inayojitegemea itakayoshughulikia rasilimali ya Jotoardhi,”amesema.

Amesema katika kongamano hilo la tano TGDC iliweza kupata mafanikio makubwa ikiwemo kuwakaribisha wafadhili katika tafiti zao,kuitambulisha kampuni hiyo pamoja na kutoa uelewa juu ya Jotoardhi na matumizi yake.

”Jotoardhi sio kuzalisha umeme tu ila kuna matumizi mengine kwenye masuala ya utunzaji wa mboga, utotoleshaji wa vifaranga pamoja na madawa,”amesema.

Kwa pande wake Meneja wa TGDC, Mhandisi Mathew Mwangomba, ameishukuru Serikali ya Rais Samia kwa kuhakikisha wanasonga mbele katika kuhakikisha wanakuwa na nishati yadilifu ya jotoardhi.

Amesema lengo la mkutano huo ni kuharakisha maendeleo ya rasilimali jotoardhi Tanzania pamoja na kuangalia masoko ya gesi ya ukaa .

“Uwepo wa jotoardhi Tanzania na kongamano hili nchini Tanzania wataalamu watu ndani pamoja na sekta zinazofugamana ikiwemo vyuo vikuu, kilimo, utalii tutaweza kukutana nao hii itasaidia kuharakisha upatikanaji wa jotoardhi Tanzania “amesema na kuendelea

“Upatikanaji wa jotoardhi nchini unaendana na hatua tatu muhimu ambazo ni sayansi jiolojia, jiofizikia na jiokemia ambayo ipo nchini kupitia Bonde la Ufa la Magharibi, Mashariki na Kusini (Tripple Juction),”amesema.

Amesema TGDC tunaelekea ngozi kuchimba nishati ya jotoardhi ambayo inapatikana kwa nyuzi joto 250, hivyo basi kukutana kwa wadau 1,000 kujadili jotoardhi tunaenda kupiga hatua zaidi.