May 8, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Shughuli za kibinadamu zaathiri bonde la Pangani

Na Hadija Bagasha, TimesMajira Online, Tanga

Shughuli za kibinadamu kwenye vyanzo vya maji vinavyotegemewa na Bonde la Pangani zimeelezwa kuwa huenda zikasababisha upungufu wa maji kwa wananchi wapatao milioni tano na laki sita wa Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Tanga wanaotegemea bonde hilo.

Kauli hiyo imetolewa na mkurugenzi mkuu wa Bodi ya Bonde la Pangani Segule Segule wakati wa mkutano wa pili wa jukwaa la wadau wa usimamizi wa rasilimali ya maji kwenye bonde hilo uliofanyika jijini Tanga na kushirikisha mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Tanga.

Segule amesema kuwa wanakabiliwa na changamoto ya uchimbaji wa madini kwenye vyanzo vya maji hususani maeneo ya Lushoto, Muheza katika upande wa msitu wa amani pamoja na changamoto ya ukataji wa miti katika maeneo ya hifadhi ya vyanzo.

Segule amesema changamoto hizo zisiposhughulikiwa kwa wakati athari kubwa inayoweza kujitokeza ni upungufu wa maji kwani bonde hilo ni moja ya mabonde 9 na ni kati ya mabonde yenye maji machache hivyo jitihada za makusudi zinapaswa kufanyika kwajili ya kuyatunza maji hayo.

“Tukiacha changamoto hizi zikashamiri maji yanapungua kwa maana yanaweza kupungua kiasi chake kwakuwa tayari yameshachafuliwa na hayawezi kutumika tena hivyo huwezi kuyahesabu kuwa ni maji kwajili ya matumizi, “amesisitiza Segule.

“Hili tunalisimamia kwa pamoja lakini pia ipo changamoto ya uchafuzi wa vyanzo kwa maana ya watu kutupa taka ngumu kwenye vyanzo vya maji kwa kuvigeuza vyanzo vya maji ndio sehemu ya kutupia taka, “amebainisha Mkurugenzi Segule.

Aidha Segule amesema mabadiliko ya tabia nchi yamekuwa yakisababisha athari za mafuriko na hata wakati mwingine ukame hivyo wakati wa uchukuaji wa hatua zipo changamoto wanazochukua hatua za haraka huku akibainisha mipango ya kati na ya muda mrefu.

Segule ameiasa jamii kubadilika na kuacha tabia ya uchafuzi kwenye vyanzo vya maji jambo ambalo linaweza kuhatarisha maisha yao.

“Tukiendelea na huu uchafuzi mwisho wa siku tutajitilia sumu sisi wenyewe kama haitakudhuru wewe mwenyewe basi inaweza kumdhuru mtu mwingine niseme tu kwamba serikali imejipanga kuwachukulia hatua kali wale wote watakaobainika wanachafua vyanzo vya maji, “amesisitiza Segule.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa jukwaa la jumuiya ya watumiaji maji mtambuka Mhandisi Mbogo Mfutakamba amesema bado jamii haijakuwa na uelewa wa kutosha wa kutunza vyavyo vya maji.

Mhandisi Mfutakamba amesema kuwa hivi sasa wizara ya maji imepiga hatua hivyo wataendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya athari za uchafuzi wa vyanzo vya maji.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Tanga Adam Malima amesema jitihada zaidi zinahitajika kutunza vyanzo vya maji akitolea mfano wilaya ya lushoto ambayo ilikuwa na vyanzo vingi vya maji ambavyo hivi sasa baadhi vimeharibiwa kwa shughuli za uchimbaji wa madini na kusema kuwa jambo hilo linapaswa kukemewa vikali.

Bonde la Pangani linategemewa na watu wapatao milioni sita kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kijamii na za kiuchumi.

Uhai wa bonde hilo utategemea utunzaji wa vyanzo vya maji vinavyotegemewa na bonde hilo katika msimu wa mvua na kiangazi.