December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikabidhiwa fomu za kuwania tena ubunge wa jimbo la Ruangwa na Katibu wa CCM wa wilaya ya Ruangwa, Barnabas Essau kwenye Ofisi ya CCM ya wilaya hiyo, Julai 15, 2020. Kushoto ni mkewe Mary Majaliwa. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Shughuli ya Ubunge CCM si mchezo

Wabunge waliomaliza muda wao sasa matumbo moto, Waziri Mkuu ajitosa, jimbo lake laendelea kupumua, siku mbili za kufa na kupona leo, kesho

Na Waandishi Wetu, TimesMajira Online, Dar Mikoani

SIKU ya pili ya uchukuaji na urejeshaji fomu kwa makada wanaoomba kusimamishwa na CCM kwenye kinyang’anyiro cha Ubunge, imeendelea kwa kishindo baada ya makada zaidi kuzidi kujitosa kwenye mchuano huo.

Kasi ya wanaojitosa kuwania kusimamishwa na CCM inazidi kuwatia hofu wabunge waliomaliza muda wao, huku wachambuzi wa masuala ya kisiasa wakisema hali hiyo kwa lugha yenyepes inastahili kufananishwa na kimbunga aina ya tsunami.

Miongoni mwa waliojitokeza kuchukua na kurejesha fomu jana ni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa. Waziri Mkuu Majaliwa alichukua fomu ya kuwania ubunge katika Jimbo la Ruangwa, wilayani humo, mkoani Lindi.

Waziri Mkuu ambaye alizijaza fomu hizo akiwa ofisini hapo na kuzirudisha kwa Katibu wa CCM wa Wilaya ya Ruangwa, Barnabas Essau na kulipa fedha taslimu sh. 100,000 zikiwa ni ada ya kuchukua fomu hizo.

Wakati Waziri Mkuu akichukua na kurejesha fomu hizo jana, gharika la makada wa CCM kuchukua fomu za kuomba kusimamishwa na chama hicho kuwania ubunge.

Iringa wagombea wafikia 247

Mkoani Iringa wakati zoezi la uchukuaji fomu likiingia siku ya tatu, wagombea 247 wamejitokeza ofisi za CCM kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa kugombea nafasi ya ubunge .

Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa, Brown Mwangomale, amesema hadi kufikia Julai 15  wagombea 247 wamejitokeza kuchukua fomu huku kukiwa na idadi ndogo ya wagombea wanawake kwa upande wa majimbo.

Akizungumza na waandishi wa habari  ofisini kwake, Mwangomale amesema kwa mwaka huu, CCM imevunja rekodi mkoani Iringa kutokana na uwingi wa wananchi kuhamasika kugombea nafasi ya ubunge wa jimbo ubunge viti maalumu ,udiwani, kundi la vijana,nafasi ya wafanya kazi pamoaja na

kundi maaluma la watu wenye ulemavu.

Rungwe

Katika Jimbo la Rungwe wanachama 24 walijitokeza kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa kugombea Jimbo la Rungwe akiwemo mbunge aliyemaliza muda wake, Saul Amon.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Katibu wa CCM Wilaya ya Rungwe, Clemence Mponzi, amesema katika jimbo la Rungwe kati ya watia nia 24, wanawake waliojitokeza ni wawili tu.

Dodoma Mjini

Kwenye Jimbo la Dodoma Mjini ambalo lilikuwa linaongozwa na Naibu Waziri, Anthony Mavunde, wamejitokeza makada 33 wanaoomba kusimamishwa na CCM kuwania jimbo hilo.

Jimbo la Busokelo

Katika jimbo hilo waliojitokeza ni wanachama 15 akiwemo mbunge aliyemaliza muda wake, Atupele Mwakibete. Hata hivyo Mponzi amesema waliojitokeza kwa wingi kugombea majimbo yote mawili ni vijana na wazee ni wachache.

Ndanda

Katika Jimbo la Ndanda, aliyekuwa mbunge wa CHADEMA, Cecil Mwambe amechukua fomu kuomba kuwania katika Jimbo hilo kwa tiketi ya CCM.

Hai

Kwa upande wa Jimbo la Hai, Mkurugenzi wa Kampuni ya Dolphin Sea and Air LTD, Emmanuel Kwayu amechukua fomu ya kuwania Ubunge Jimbo la Hai, ambapo endapo atapitishwa atavaana na aliyekuwa mbunge wa Jimbo hilo, Freeman Mbowe.

 Kigoma

Kwenye jimbo la Kigoma Mwanahabari mwandamizi, Baruan Muhuza, amechukua fomu kuomba kuteuliwa na Chama Cha Mapinduzi kugombea Ubunge Jimbo la Kigoma.

Songea

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro, alichukua fomu  ya kuomba kusimamishwa na CCM kuwania Ubunge Jimbo la Songea akitumia usafiri wa baiskeli.

Arusha

Wakili Albert Msando achukua fomu ya Ubunge Jimbo la Arusha Mjini. Msando alichukua fomu ya kugombea Ubunge katika Jimbo la Arusha Mjini kupitia CCM.

Segerea

Kwa upande wa Jimbo la Segerea, aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Bonnah Kamoli alichukua fomu ya kuomba kuteuliwa kwa mara nyingine kugombea

Mkuranga

Katika jimbo hilo, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, amejitokeza kuchukua fomu ya kugombea Ubunge wa Jimbo la Mkuranga, Mkoa wa Pwani.

Mtoto wa Marehemu Mchungaji Rwakatare ajitosa

Mtoto wa Marehemu Mchungaji, Getrude Rwakatare, Kellen Rose Rwakatare amechukua fomu ya kuomba ridhaa ya kupeperusha bendera ya CCM kwenye nafasi ya ubunge.

Kigamboni

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, jana amechukua fomu ya kuomba ridhaa ya Kuwania nafasi ya Ubunge Jimbo la Kigamboni kupitia tiketi ya CCM.

 Ubungo

Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Profesa Kitila Mkumbo  amechukua fomu kuwania Jimbo la Ubungo.

Profesa Mkumbo alikabidhiwa fomu jana katika ofisi ya wilaya ya Ubungo na Katibu wa CCM Wilaya hiyo, Sylvester Yared.

Mvomero

Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Brigedia Jenerali Emmanuel Maganga amechukua fomu kuwania fomu Jimbo la Mvomero.

TAKUKURU wamsafisha Lusinde

Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Dodoma, Sostenes Kibwengo amesema,taasisi hiyo haitaendelea na kesi ya tuhuma za rushwa ya aliyekuwa Mbunge wa Mtera kupitia CCM, Livingstone Lusinde (Kibajaji) kutokana na kukosekana uthibitisho wowote.

Kibwengo alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dodoma.

Kibwengo amesema kuwa hadi sasa taasisi hiyo bado haijapata uthibitisho wowote wa Mbunge huyo kuwa alitoa rushwa kwa wajumbe ili wamsaidie katika mchakato wa uchaguzi Mkuu ujao.

Akizungumza kuhusu tukio hilo, Lusinde amesema kuwa yeye hakutoa rushwa, bali aliyetoa taarifa hiyo alikuwa na lengo la kumchafua kisiasa.

“Pale kwangu nilikuwa na shughuli ya mjukuu wangu kwa hiyo nilikuwa na wageni wengi,mtu akatumia nafasi hiyo kunichafua na kutoa taarifa takukuru kuwa nilikuwa natoa rushwa kwa wajumbe.

Same Mashariki

Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Same Mashariki mkoani Kilimanjaro kwa tiketi ya CCM, Anne Kilango amejitosa kwenye kinyang’anyiro cha kura za maoni za chama hicho baada ya kuchukua fomu ya kuwania kupeperusha bendera ya CCM Jimbo la Same Mashariki. Kilango alichukua fomu hiyo jana kwenye Ofisi ya CCM Wilaya ya Same