Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
SERIKALI na wadau mbalimbali wamekuwa wakifanya jitihada za kupambana na ukatili pamoja na kuwekeza kwenye afya hivyo
SHIRIKA la Wadada Solutions on Gender Based Violence limesema litaendelea kuunga mkono jitihada za kutokomeza ukatili nchini pamoja na kuwekeza kwenye sekta ya afya.
Akizungumza wakati wakikabidhi msaada wa vifaa vya kunawia mikono kwa ajili ya kujikinga na maradhi mbalimbali jana, ofisa Mradi Haki ya Binti awamu ya pili wa Shirika hilo, Karus Masinde, amesema kupitia mradi huo wataendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kupambana na ukatili na magonjwa mengine ya mlipuko ili kuwe na taifa salama.
Amesema wametoa matenki na vifaa vya kusafishia mikono katika shule za Sekondari Mihama na Kitangiri ambapo mradi huo unatekelezwa,ili wanafunzi waweze kujikinga na magonjwa yanayosababishwa na uchafu na kuimarisha afya zao.
“Leo tumekuja kutembelea shule ya Sekondari Mihama na Kitangiri na kuwaletea matenki kwa ajili ya kuwekea maji, sabuni na vitakasa mikono kwa ajili ya kusafishia mikono ili kujikinga na Corona.
“Pia tunaendelea kupinga ukatili kama tunavyoona kipindi cha likizo watoto wamekuwa nyumbani na kesi nyingi za mimba kutokana na Corona zimeongezeka,na sisi kama wadau tunaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali za kuweza kupambana na magonjwa mbalimbali pia kuhakikisha mtoto wa kike anakuwa salama na kuepukana na mimba za mapema,”amesema Masinde.
Makamu Mkuu wa shule ya Sekondari Mihama Mwl.Francis Ouma, amelishukuru shirika hilo kwa kuwapatia vifaa hivyo vya kujikinga na magonjwa ya kuambukizwa vinawafaa kutokana na hali halisi hapo shuleni ambao wanatumia ndoo za lita 20 ambazo zimewekwa kila darasa na ukilinganisha na idadi ya wanafunzi ambao 529 kidogo ilikuwa ni changamoto.
“Tenki hilo la kuwekea maji litatusaidia kwa kiasi kikubwa sana,shirika hilo limekuwa marafiki wazuri kwetu kwani wameanza kuwalea wanafunzi wetu tangu 2016 kwenye mradi wa Haki ya Binti awamu ya kwanza mpaka leo awamu ya pili wameendelea kuwalea pia ni washauri wazuri wa watoto wetu,kiasi imepelekea tuwe na watoto wazuri ambao wanapendeza kwenye jamii ambapo kupitia shirika hilo mimba zimepungua na katika kipindi cha corona hawajapokea kesi ya mimba , amesema mwalimu Ouma.
Kwa upande wake dada mkuu wa shule ya Sekondari Mihama Rahma Suleimani, amesema tenki litawasaidia katika utunzaji wa maji kwani yalipokuwa yakikatika wanakosa maji ya ziada hivyo aliomba waendelee kuwasaidia kwani changamoto ni nyingi shuleni hapo ikiwemo kukosekana kwa taulo za kike na kuwa na chumba kidogo cha kujihifadhia wakati wa hedhi na matundu ya vyoo vya watoto wa kike ni machache ambayo yapo sita ukilinganisha na idadi yao ambao wapo zaidi ya 200.
Naye Kiongozi Mkuu wa Serikali ya Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mihama Charles Robert, amesema vifaa hivyo vitasaidia kuhifadhi maji ambayo yatakuwa ni msaada kwao kwa kuhakikisha suala la usafi la unawaji mikono linazingatiwa na ikizingatiwa kipindi walichotoka hapo nyuma kulikuwa na ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na kirusi cha Corona na bado tahadahari inaendelea kuchukuliwa.
Amesema tangu wametoka kwenye likizo ya Corona walimu wao wanejidhatiti kuwaelimisha namna ya kujikinga na ugonjwa huo kwa kunawa mikono na kuvaa barakoa ingawa suala la kuvaa barakoa halikutiliwa maanani ila la kunawa mikono hadi leo linaendelezwa.
Mlezi wa Club ya Wadada Centre shule ya Sekondari Kitangiri,Mwalimu Nezia James amesema vifaa hivyo walivyopatiwa na shirika hilo vitawasaidia katika suala ya usafi na shule yao ni ya kutwa hivyo muingiliano ni mkubwa itasaidia kuboresha afya zao,na kupitia miradi ya haki ya binti imesaidia mabinti kujitambua,kujikomboa na ukatili wawapo nyumbani na njiani pamoja na mimba zimeweza kupungua huku baada ya kufungua shule bado hawajapata kesi yoyote ya mimba.
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kitangiri wakibeba tenki la maji lililotolewa na shirika la Wadada Solutions on Gender Based Violence,kwa ajili ya kujikinga na maradhi mbalimbali na kuimarisha usafi shuleni hapo na kuboresha afya zao.picha na Judith Ferdinand.
Ofisa Mradi wa Haki ya Binti awamu ya pili wa Shirika la Wadada Solutions on Gender Based Violence Karus Masinde, kushoto akishikana mkono na mmoja wa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kitangiri baada ya kukabidhi tenki na vifaa vya kunawia mikono kwa ajili ya kujikinga na kuimarisha usafi shuleni hapo.Picha na zote na Judith Ferdinand.
More Stories
Balozi Nchimbi kuongoza waombolezaji mazishi ya Kibiti leo
Dkt.Tulia,apewa tano kuwezesha wananchi
Nkasi yajipanga kukusanya mapatoÂ