KUTUNGWA kwa Sheria ya kulinda ardhi ya kilimo ni muhimu kwa wakati huu ambapo kila siku idadi ya Watanzania inaongezeka na ukubwa eneo la Tanzania liko palepale.
Hivi karibu Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga azindua masoko ya tumbaku kwa mwaka 2019 Kitaifa Wilayani Urambo Mkoani Tabora na kuahidi kupeleka katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Muswada unahusu ulinzi wa ardhi ya kilimo.
Anasema kuwa kumezuka tabia katika baadhi ya maeneo nchini watu wanabadilisha maeneo ya kilimo wanajenga nyumba na kuendesha shughuli nyingine.
Hasunga anasema ili kukabiliana na tatizo hilo wanakusudiwa kuweka ulinzi wa kisheria wa maeneo yote yanayofaa kwa kilimo kama njia ya kuwahakikisha wakulima hakosi maeneo ya kuendeshea shughuli zao na kuhakikisha kunakuwepo na usalama wa chakula na mazao ya kilimo hapa nchini.
Anasema lengo ni kuhakikisha kuwa ardhi inayofaa kwa shughuli ya kilimo inabaki kwa ajili ya matumizi ya kilimo hapa nchi ili kuwahakikishia Watanzania uhakika wa chakula.
Hasunga anasema kuwa idadi ya wananchi inakuwa kila siku na ukubwa wa Tanzania bado uko pale pale, hivyo ni vema kuwepo na Sheria ambayo italinda ardhi ya kilimo isitumike kwa matumizi mengine zaidi ya uzalishaji wa chakula na mazao mengine.
Anaongeza kufuatia endezeko la wananchi na eneo la ardhi ni lile lile ipo haja ya kuwa Sheria hiyo ambayo itasaidia kulinda ardhi kwa ajili ya kilimo ili kuepuka kuvamiwa na shughuli nyingine.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Mahmoud Mgimwa anasema wakati umefika kwa Serikali kuhakikisha inaandaa Sheria ya kumlinda Mkulima kama ilivyo katika sekta ya madini.
Anasema lengo ni pamoja na kulinda mkulima na kumpa uhuru wa kuuza mazao yake anapopenda bila kuliingiliwa na watendaji wa Serikali.
Mgimwa anasema kuwa kilimo ndio kitasaidia kuwaondoa wananchi wengi katika umaskini na kuleta mapinduzi ya uchumi wa viwanda nchini.
Aliyewahi kuwa mkuu wa Mkoa wa Singida,Dkt. Paseko Kone mwaka 2012 akiwa katika maonenyesho ya nane nane mjini Dodoma aliwahi kutoa wito wa kuanza kujengwa nyumba za makazi za ghorofa ili kulinda ardhi kwa ajili ya matumizi mengine ikiwemo kilimo.
Alisema ujenzi wa sasa wa nyumba nyingi kwa mtindo wa kulala badala ya kwenda juu(maghorofa) unachukua nafasi ambayo ingetumika katika shughuli za maendeleo ikiwemo kilimo , ujenzi wa viwanda na ufugaji.
Naye Mkazi wa Manispaa ya Tabora Neema Maganga anasema sheria hiyo imechelewa kutungwa kwa kuwa sehemu nyingi ambazo zingesaidia katika uzalishaji wa chakula zimeshavamiwa kupimwa viwanja na kuuziwa wananchi.
Anatoa mfano wa maeneo ya Manispaa ambayo yalikuwa yakitumiwa na wakulima hivi sasa yamejengwa ni pamoja na uledi, malolo na lile ambalo linapakana na shule ya Sekondari Milambo,baadhi ya maeneo ya Ipulu yalikuwa yakifaa katika kilimo cha Mpunga kwa kuwa ni mbuga yenye maji mengi.
Neema anasema hatua hiyo imesababisha kipindi cha mvua baadhi ya wakazi wa maeneo hayo kuvamiwa na mafuriko na wakati mwingine kupata hasara ya kupoteza mali zao.
Mohamed Rufunga anasema kuwa ipo haja ya kuangalia upya na sheria nyingine ambazo ndio zinachochea maeneo ya kilimo kubadilishwa matumizi pindi eneo linapoendelea na kuwa mji ikiwemo Sheria ya Mipango Miji Na. 8 ya mwaka 2007.
Anasema ni vema eneo linapokuwa mji kutengwa pia eneo kwa ajili ya shughuli za kilimo na kuacha na ile zana kuwa mjini ni viwanda na biashara tu na hakuna kulima wala kufuga.
Rufunga anasema kila siku wananchi wanatafuta maendeleo kiasi kwamba katika maeneo ambayo yalikuwa vijiji kwa miaka 90 sasa ni miji na ndio hivyo itakavyoendelea kuwa kwa sababu ya maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia yanaendelea hapa duniani.
Anasema na kwa sababu dunia ni kama kijiji kimoja ni lazima kila eneo hapa nchini litakuwa na sura ya kimji na kama sheria ya baadhi ya Halmashauri kukataza kulima maeneo ya mijini na kupima viwanja maeneo ya kilimo ipo wakati kutakuwa na upungufu wa chakula utatokea.
“Nafikiri hata nchi zilizoendelea zimetebga eneo maalumu kwa ajili ya kilimo na ufugaji …nadhani eneo hilo haliwezi kubadilishwa matumizi kama vile kupima viwanja na ndio linatumika kulima kama tulivyokuwa tukisoma shule za Msingi katika Somo la Jiografia … kilimo cha ngano Canada huko katika mbuga za Saskatchewan” anasema
Anasema vitendo vya kila Halmashauri kutumia sheria hiyo kupima yaliyokuwa mashamba ya wakulima kwa kisingizio kuwa eneo hilo limegeuka mji ni kupunguza ardhi ambayo ingetumika kutoa ajira kwa wananchi wengi.
Rufunga anasema wakati umefika wa kuuza viwanja juu ya nyumba zilizopo na kuzibadili kutoka nyumba za kawaida na kuwa maghorofa ili kulinda aridhi kwa ajili ya kilimo na shughuli nyingine za maendeleo.
More Stories
Ubunifu wa Rais Samia kupitia Royal Tour unavyozindi kunufaisha Tanzania
Rais Samia anavyojenga taasisi imara za haki jinai kukabilina na rushwa nchini
Rais Dk. Samia alivyowezesha Tanzania kuwa kinara usambazaji umeme Afrika