Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
Waumini wa dini ya kiislamu na watanzania kwa ujumla, wameombwa kuwapenda na kuwalea yatima pamoja na kushirikiana na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) kutatua changamoto za watoto na vijana wanaoishi na kufanya kazi mtaani ili waweze kurejea katika familia zao na kuwa na jamii salama.
Wito huo umetolewa na Sheikh wa Mkoa wa Mwanza Hassan Kabeke,wakati walipo jumuika pamoja na watoto yatima na wajane kwenye hafla ya chakula cha kusherekea sikukuu ya Eid kilichoandaliwa na BAKWATA kwa kushirikiana na Rock Solution Limited sambamba na kutembelea makazi (maskani)ya watoto na vijana wanaoishi na kufanya kazi mtaani ambao wanaishi nje ya makaburi ya waislamu Mlango Mmoja jijini Mwanza.
Sheikh Kabeke,amewaomba Watanzania kurudi kwenye asili yao ya zamani ya kuwalea yatima katika nyumba zao na siyo kuwapeleka katika vituo vya kulelea watoto hao.
Amesema katika uislamu kukaa na watoto yatima katika nyumba ni jambo bora zaidi na baraka kwa Mungu kuliko kuwalea katika vituo vya kulelea watoto hao ambapo zamani mtu akifariki kitu cha kwanza kushughulikiwa ilikuwa watoto wale wanalelewa na nani lakini sasa watoto wamekuwa wakiachwa na mapenzi ya ndugu yamepungua.
“Waislamu wote tumekimbia kuwalea watoto yatima nyumbani na tumeamua kuwaweka kwenye vituo ingawa ni jambo zuri wito kwa waislamu na wasiyo waislamu wenye uwezo kuwasaidia wanaowalea watoto yatima,sababu jamii ya kiislamu baadhi yetu tumeacha jambo hili ambalo ni jema lililo raha zaidi la watoto hawa kukaa katika nyumba zetu,kwani Mtume anasema yoyote yule anaishi na yatima basi atakuwa pamoja peponi,”amesema Sheikh Kabeke.
Amesema,kila mwaka katika sikukuu ya Eid wamekuwa na utaratibu wa kujumuika na yatima kula chakula pamoja,hivyo maumivu walionayo ni kuona watoto wadogo wenye umri wa kwenda shule lakini wapo mtaani na kutokana na mazingira wanaoishi ikiwemo kuvuta bangi wanaweza kutumika na watu wabaya kufanya maovu.
“Tulikuwa tunasema watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu lakini tulikuwa hatujawaona,Mungu akataka leo tuje tuwaone bayana,na kweli tumewakuta hapa na mkatwambia kuwa nyie mpo zaidi ya 60 hapa lakini tunalo ombi kwa umri wenu inawezekana kuna mambo yaliowakwaza yakishughulikiwa kikamilifu mnaweza kurudi kwenye familia zenu,tunaomba jamii ishirikiane na BAKWATA kutatua changamoto zenu ili muweze kurudi katika familia zenu,”amesema Sheikh Kabeke.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Rock Solution Limited Zacharia Nzuki, amesema wamekuwa wakiwasaidia watoto walio katika mazingira magumu ambao ni wengi ndani na nje ya Mwanza, ambapo jambo hilo ni msukumo hivyo amewahimiza watu wengine wenye uwezo waone umuhimu wa kuwasaidia watoto hao kwani wapo wanaohitaji chakula,elimu na vitu mbalimbali.
Mmoja wa vijana wanaoishi katika eneo hilo la makaburi ya waislamu Mlango Mmoja, Joseph Jeremiah,amesema kipigo kutoka kwa baba wa jambo ndio kimepelekea yeye kukimbilia mtaani,changamoto wanazokutana nazo ni pamoja na kukosekana na mavazi huku akiishukuru BAKWATA kwa kuweza kusherekea pamoja nao sikukuu hiyo jambo ambalo hawajawai kufanyiwa.
Pia ameiomba jamii na wazazi kuacha tabia za kuwanyanyasa watoto wao ili wasiweze kukimbilia mtaani sanjari na kuwasihi watoto wengine wasikimbilie mtaani kwani maisha ya mtaani ni magumu huku akiendelea kuiomba jamii kuwasaidia elimu,mavazi pamoja na mahali pa kulala.
Naye Hassan Athuman,ametoa shukrani zake kwa waumini hao kuweza kujumuika nao kusherekea sikukuu hiyo,huku akieleza kuwa watoto hao ni wadogo na wanajifunza zaidi tabia mbaya ambazo haziwezi kumsaidia katika maisha yake ni rahisi kutumika katika vitendo viovu na kulipa taifa mzigo lakini wangejifunza mambo mema tangu wakiwa wadogo wangejua mazuri na mabaya ila kwa sasa wanajua mabaya na wanaweza kutumika na watu wabaya kufanya.
Mstahiki Meya wa Jiji la Mwanza Constantine Sima,ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo amesema,jambo hilo limekuja wakati serikali ikisisitiza umuhimu wa familia kutotelekeza watoto huku ndugu na jaama kuendelea kuwatunza watoto yatima.
“Sisi kama serikali tunatambua tunao wajibu wa kuhakikisha kwamba kundi hili maalumu tunaendelea kilitunza na kuendelea kuliangalia kwa ukaribu kwa sababu tunaamini kuwa yatima wa leo ni mzazi wa kesho,hivyo ni vyema kushiriana na viongozi wa dini ili kuhakikisha yatima hawa wanakuwa salama,” amesema Sima.
More Stories
Wakuu wa Wilaya,Wakurugenzi watakiwa kusimamia programu za chakula shuleni
Mbowe akuna wengi kuhusu maridhiano
Waziri Chana amuapisha Kamishna uhifadhi NCAA, ampa maagizo mazito