May 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Sheikh Kabeke afiwa na mkewe,CCM yamfariji

Na Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza

Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mwanza kimetoa salamu za pole kwa Sheikhe wa Mkoa huo Alhaji Hassan Kabeke kwa kuondokewa na mkewe Hajat Hadija Binti Athuman aliyefariki juzi asubuhi.

Salamu hizo zimetolewa kwa nyakati tofauti na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Michael Masanja ‘Smart’ na Mjumbe wa NEC Jamal Abdul Babu, nyumbani kwa Sheikhe Kabeke, Majengo Nyegezi wilayani Nyamagana mkoani hapa.

Akitoa salamu hizo za pole kwa Sheikhe Kabebe, Mwenyekiti Smart amesema msiba huo ni mzito ni jambo gumu kulivumilia na kulistahimili hivyo wanamwombea marehemu Hajat Hadija ,Mwenyezi Mungu amwondolee moto wa kaburi.


“Uongozi wa CCM Mwanza na wana chama wake unakupa pole Sheikh Kabeke kwa kuondokewa na mwenzi wako katika kipindi hiki kigumu, Mungu akupe subira na ustahimilivu wa jambo hili gumu na zito,”amesema Smart.

Kwa upande wake Mjumbe wa NEC Jamal amesema Sheikhe Kabeke amekuwa kiongozi wa dini wa mfano licha ya kufanya kazi ya kiroho amekuwa akiiombea CCM,serikali na Rais Dkt.Samia.

Naye Katibu wa CCM Omary Mtuwa amesema kutokana na chama kuguswa na msiba huo kimetoa ubani na lita 100 za mafuta ya kusafirisha mwili wa marehemu kwenda Kigoma kwa maziko.

Akitoa shukrani kwa niaba ya Sheikhe Kabeke Ustaadhi Twaha Utali amekishukuru Chama Cha Mapinduzi kwa salamu hizo za pole kwa msiba huo.