May 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali,BAKWATA kujenga vituo vya afya

Na Daud Magesa,TimesMajira Online Mwanza

SERIKALI ya Mkoa wa Mwanza,imeeleza kuwa itaendelea kushirikiana na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) mkoani humo ili kuhakikisha vituo vya afya vinavyojengwa na baraza hilo vinakamilika na kuwahudumia wananchi.

Ahadi hiyo imetolewa leo na Mkuu wa Wilaya ya Ilemela,Hassan Massala,kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Adam Malima katika harambee ya kuchangia ujenzi wa kituo cha afya cha BAKWATA wilayani humo.

Amesema serikali inatambua juhudi kubwa zinazofanywa na BAKWATA za kusimamia dini na maendeleo ikiwemo ujenzi wa miradi ya vituo vya afya jambo linalogusa maslahi ya wananchi wote.

“Mkuu wa Mkoa anawapongeza kwa kazi mnazofanya na anaendeleza pale alipoachia Mhandisi Robert Gabriel, kazi hii anatambua inakwenda kugusa maisha ya wana Mwanza,”ameeleza Massala.

Pia ameeleza kuwa ni njia moja ya kumsaidia Rais Samia Suluhu Hassan kutekeleza mpango wa kujenga hospitali kila wilaya,kituo cha afya kila kata na zahanati kwa kila kijiji.

Sheikhe wa Mkoa wa Mwanza,Alhaji Hasani Kabeke, akizungumza na waumini wa dini ya Kiislamu waliojitokeza kwenye kukimbukizi ya vita ya Badir sambamba na harambee ya ujenzi wa vituo vya afya iliyofanyika kwenye Uwanja wa Furahisha,Kirumba wilayani Ilemela.

Amesema kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022,Mwanza ina watu milioni 3.6,idadi inayoashiria tunahitaji kuwafikishia huduma za msingi za afya,maji,elimu na barabara,zilizokasimiwa kufanywa na serikali.

“Wanapojitokeza wadau kufanya hayo serikali inafarijika,jambo hili la kujenga vituo vya afya lingekuwa haligusi maisha na maslahi ya watu tusingekuwa hapa,wanakwenda kupata huduma na kwetu sisi tunakuja kuwashika mkono, vikikamilika vitahudumia watu wa dini zote bila kubagua,”amesema Mkuu huyo wa Wilaya.

Aidha amemtia moyo Sheikhe wa Mkoa wa Mwanza,Alhaji Hasani Kabeke kuwa kazi kubwa anayofanya inaonekana kwa watu wengi,asikatishwe tamaa kwa kelele na yanayozungumzwa kwa sababu mti wenye matunda ndio unaopigwa mawe,hivyo aendelee na falsafa ya kutojali kelele zinazipigwa.  

Awali Sheikhe wa Mkoa wa Mwanza Alhaji Hasani Kabeke akimkaribisha mgeni rasmi huyo,amesema harambee hiyo iliofanyika sambamba na kumbukizi ya vita ya Badir El Kubra, amewataka waislamu kupambana katika vita ya maendeleo ili wanaobeza na kuitukana BAKWATA haiwezi kusimamia miradi isipokuwa ndoa,wasipate nafasi hiyo.

“Tulipoingia madarakani Oktoba 2018 BAKWATA haikuwa na kitu si kwamba wazee hawakufanya kitu la!Tumeleta mabadiliko ya maendeleo bado watu wanatutukana,hatuwezi kukubali kuvunjiwa heshima,hivyo tumekualika leo uje kuandika historia ya Badir Mwanza,kwa uchache na unyonge wetu,kwa imani na nguvu ya nyumba ya Mtume S.A.W. tutashinda vita hii ya maendeleo,”amesema.

Naye Katibu wa BAKWATA mkoani humo,Ramadhani Chanila amesema ujenzi wa vituo vya afya unaolenga kusogeza huduma karibu na wananchi bila kubagua imani na itikadi za kidini.

Pia unaunga mkono juhudi za serikali katika kuwahudumia Watanzania, umefanikiwa  kwa kiasi kikubwa kwa michango ya wadau mbalimbali.

“Tulizindua harambee Aprili 2022  na kupata milioni 25, ilihitimishwa Julai 2022  kwa kukusanya milioni 28.4 tasilimu na ahadi ya milioni 102.7,bado wadau wengi hawajatekeleza ahadi ya fedha walizoahidi kiasi cha milioni 131.09, hivyo tunawakumbusha ili watimize ambapo kituo cha afya Ilemela jengo la wagonjwa wa nje (OPD) limekamilika,”amesema Chanila

Chanila amesema licha mafanikio zipo propaganda za makusudi za kukwamisha miradi hiyo zinazofanywa na baadhi ya Waislamu wakiwemo viongozi wasiolitakia mema baraza.

Ambao wanaendelea kuishi katika historia na dhana mbaya ya kufikirika kuwa BAKWATA haiwezi kusimamia na kuendesha miradi pia wengi kutobadilisha fikra za kuchangia maendeleo ya Uislamu.

Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Hasani Masala kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima, akizungumza kwenye kukimbukizi ya Badir el Kubra kabla ya kufanyika harambee ya ujenzi wa vituo vya afya vya BAKWATA wilayani humo.

Katibu wa BAKWATA Mkoa wa Mwanza,Ramadhani Chanila,akisoma taarifa ya harambee ya mradi wa ujenzi wa vituo vya afya mkoani humu leo wakati wa kumbukizi ya vita ya Badir el Kubra iliyopiggwana mwaka 1400 iliyopita.