Na Mwandishi wetu,Timesmajira,Online
SERIKALI imezindua mfumo wa uchakataji leseni katika Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), huku ikiitaka mamlaka hiyo kutokuwa kikwazo cha kukwamisha wawekezaji nchini.
Hayo yamesemwa mkoani Dar es Salaam na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt Faustune Ndugulile mara baada ya kizindua mfumo katika Ofisi za TCRA, ambapo katika hafla hiyo viongozi mbalimbali wa serikali walikuwepo.
Amesema mfumo huo, utasaidia uwajibikaji na uwazi sambamba na kupunguza muda wa ucheleweshawaji wa leseni kwa waombaji.
Dkt. Ndugulile amesema Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais, Samia Hassan Suluhu imejipanga kuboresha sekta ya mwasiliano nchini ambapo mfumo wa uombaji leseni ndogo kwa sasa ni siku tatu hadi tano, huku leseni kubwa ni siku 45 kutoka mwaka mmoja ilivyokuwa hapo awali.
“Kwa sasa dunia inafanya mabadiliko makubwa katika sekta ya mawasiliano na serikali imejipanga kufanya mabadiliko hayo, ili kuhakikisha wawekezaji hawapati changamoto tulikuwa na changamoto ya ucheleweshaji wa huduma ya utolewaji leseni na ilikuwa kero kwa wawekezaji,” alisema.
Dkt. Ndugulile aliipongeza TCRA kwa kuwa wazalendo kwa kutumia wataalamu wa ndani katika kutengeneza mfumo huo.
Alitoa wito kwa wananchi, kujitokeza kuwekeza katika kuomba leseni za usikivu wa vituo vya redio kwenye wilaya 69 nchini, ambapo matangazo ya maombi yatafanyika hapo baadaye.
“Tunataka kufanya uhamasishaji wa wawekezaji katika usikivu wa redio kwenye wilaya 69, Watanzania wajitokeze kwani baadhi ya maeneo hakuna usikivu wa redio,” amesema.
Katika hatua nyingine, Dkt. Ndugulile ameiagiza TCRA kumalizia haraka mchakato wa mapitio ya tozo mpya za maudhui ya mtandaoni, ili hadi kufikia Septemba Mosi mwaka huu ziwe zimefanyiwa kazi kwa ajili aweze kuwasilisha kwa Rais Samia.
Kwa upande wake Waziri wa Habari Sanaa Utamaduni na Michezo, Innocent Bashungwa amesema mfumo huo utaleta weledi na ufanisi katika vyombo vya redio na televisheni.
Amesema mfumo huo utasaidia kuondoa vitendo vya rushwa kwa watoa huduma na kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya habari.
Amesisitiza kuwa serikali, haitamfumbia macho mtumishi yeyote atakayesababisha ucheleweshaji katika kutoa huduma hiyo.
“Mtumishi yeyote ambaye atalegalega na kusababisha kuchelewesha, serikali haitamfumbia macho na mfumo huu utaongeza weledi na ufanisi na weledi katika vyombo vyetu vya habari,” amesema.
Akiuelezea mfumo huo kwa namna utakavyofanya kazi Mkurugenzi wa Leseni na Udhibiti kutoka TCRA, John Daffa amesema mfumo huo utasaidia maombi ya leseni hizo, kufanyiwa tathmini na wataalamu kwa muda mfupi tofauti na hapo awali.
Amesema mfumo huo, utasaidia kupunguza muda wa uchakataji maombi ya leseni kutoka mwaka mmoja hadi siku tatu hadi tano kwa leseni ndogo.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba