Na Daud Magesa,TimesMajira Online, Sengerema
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Adam Malima amewaagiza waajiri kuzingatia sheria za kazi ikiwemo kuwasilisha michango ya wafanyakazi kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii kwa wakati.
Pia katika kujali maslahi ya watumishi Serikali ya awamu ya sita,mkoani Mwanza imewalipa bilioni 1.74 watumishi 571 walioghushi vyeti na milioni 660 walilipwa watumishi 503 za malimbikizo yasiyo ya mishahara.
Malima akizungumza leo kwenye maadhimisho ya siku ya Wafanyakazi yaliyofanyika kimkoa uwanja wa Mnadani wilayani Sengerema ,amesema waajiri wasiozingatia sheria za kazi watawajibika kwa kuchukuliwa hatua stahiki za kisheria.
“Hili la mikataba ya ajira kwa watumishi,makato ya michango kutowasilishwa kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii na kuwalipa kima cha chini cha mshahara kinyume,waajiri hasa sekta binafsi wasidhani wana hiari hiyo ni la msingi wa kisheria,nawaagiza waajiri wote wahakikishe sheria za kazi zinazingatiwa,maslahi na mishahara wanalipa kwa wakati,” amesema.
Malima.Ameeleza kuwa mwaka 2022 serikali imewalipa watumishi 3,744 kiasi cha bilioni 2.4 za madai yasiyo ya mshahara,zaidi ya wafanyakazi 4,000 walipandishwa madaraja, 290 walikopeshwa bilioni 2.65 zisizo na riba, 1,122 wameajiriwa na 649 wanajiendeleza kwa masomo.
“Kazi inayofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan, ni kubwa,yapo maeneo itaendelea kujipanga kuboresha maslahi ya wafanyakazi na kufanyia kazi nyumba za watumishi na stahiki zingine hatua kwa hatua,”amesema.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema Rais Samia kama mtumishi na Rais yuko tayari kupokea na kufanyia kazi changamoto za wafanyakazi ili kuboresha maslahi na stahiki zao,hivyo uwajibikaji na uadilifu unatakiwa na kuonya waajiri wasiangalie upande mmoja na kuahidi kuondoa kasoro hizo ili kuleta tija na uzalishaji zaidi.
Amekerwa na walinzi wa NSSF kugeuka kitengo cha huduma kwa wateja na kuwanyanyasa wanachama wa mfuko huo kuwa si sawa na kuwaagiza Wakuu wa Wilaya wahakikishe unyanyasaji huo unakomeshwa pia makato ya mafao yawasilishwe kwa wakati na waajiri walipe fedha za nauli na posho za uhamisho wa watumishi.
Awali Mratibu wa Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) mkoani humu, Zebedayo Athuman,amesema baadhi ya waajiri ikiwemo Redio Sengerema na Hospitali ya Bukumbi,wanakiuka sheria kwa kuwasilisha michango ya watumishi kwenye mifuko ya jamii,hawatoi mikataba ya ajira na hawalipi mishahara kwa wakati.
Amesema kikotoo bado ni kaa la moto kwa wafanyakazi kiangaliwe upya,pia idara ya kazi imekosa uadilifu na inawakandamiza watumishi ikishirikiana na waajiri,mikataba isiyozingatia sheria na watumishi wa vituo vya afya kutolipwa stahiki zao kwa ukosefu wa mapato na kuomba utaratibu huo utazamwe upya.
“Tunaipongeza serikali kwa nyongeza ya mishahara mwaka 2022 lakini kwa sekta binafsi bado haikidhi,tunachangamoto ya waajiri kutowasilisha kwenye mifuko ya jamii michango na wanakwepa malipo ya mafao ya wastaafu na watambue ni haki yao,usumbufu kwa wastafu unaofanywa na walinzi wa NSSF na PSSSF pamoja na waajiri kutowalipa fedha za saa za ziada na likizo,” ameeleza Zebedayo.
Ameiomba serikali ifanyie kazi na kusaidia kutatua changamoto hizo ili kuwapa nafuu wafanyakazi na kukomesha tabia za waajiri wasiozingatia sheria za nchi ambapo kauli mbiu ya mwaka huu; “Mishahara Bora na Ajira za Stara ni Nguzo ya Maendeleo ya Wafanyakazi.” Wakati ni Sasa.
More Stories
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili
ACT-Wazalendo,waitaka Polisi kutobeba chama kimoja