May 17, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yatia saini mkataba wa kufanya tathmini ya athari ya kimazingira na kijamii

Na.Penina Malundo

SERIKALI imetia saini  Mkataba wa kufanya Tathmini ya Athari ya Kimazingira na Kijamii kwa ajili ya Ununuzi wa Meli za  Uvuvi , Kupitia Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP).

Akizungumza mara baada ya kutia saini mkataba huo jana  Jijini Dodoma, Katibu Mkuu  Ofisi ya Waziri  Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonaz amesema mkataba huo ,utawezesha kufanyika kwa tathmini ya athari ya mazingira pamoja na  matengenezo ya meli zitakazotumika katika uvuvi wa bahari kuu ili  kupata mazao ya bahari yatakayochangia katika uchumi wa nchi.

Dkt. Yonaz ameendelea kusema kuwa, sambamba na tathmini hiyo  pia utafanyika  upembuzi  yakinifu katika kuundwa kwa vyombo hivyo  kazi itakayofanyika kwa muda wa  siku 75  ambapo itagharimu kiasi cha sh. Milioni.

“Tanzania inazo rasilimali nyingi za majini, sasa ili kuhakikisha tunainua uchumi kupitia  Uchumi wa Bluu Serikali imeona ni muhimu kutengeneza meli kubwa zitakazovua katika kina kirefu ili kupata mazao ya bahari ambapo meli nne zitatengenezwa  kwa ajili ya Zanzibar na Meli tano kwa Tanzania Bara hivyo kukamilika kwake kutasaidia kuinua uchumi wa Taifa,’’amesema Dkt. Yonazi.

Amewahimiza  wadau wa uvuvi ambao ni  Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) na Shirika la Uvuvi la Zanzibar (ZAFICO) kushirikianana Mkandarasi huyo kuhakikisha  kazi hiyo inafanyika kikamilifu huku akihimiza kila mmoja kuwajibika kwa sehemu yake kwa lengo la kupata matokeo chanya.

Kwa  upande  wake Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Ushauri wa masuala ya Mazingira (TANSEQ), Lusako Raphael amebainisha kwamba lengo la kufanya tathimini hiyo ni kuhakikisha mradi hausababishi athari hasi katika mazingira na jamii.

“Mradi huu unalenga kuwezesha ununuzi wa meli pamoja na uanzishwaji wa viwanda vya kuchakata samaki hivyo tunategemea kupata ushirikiano kutoka kwa wadau wote  kama ZAFICO, TAFICO na Wizara ya Kilimo,”amesema na kuongeza

‘’Pia kuna mkakati wa kudhibiti athari za mazingira ambao ndiyo utakuwa muongozo wa utekelezaji wa mradi,’’amesema.

Ikumbukwe kuwa AFDP ni mradi wa Kuendeleza Kilimo na Uvuvi unaoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu ukifadhiliwa na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD).