January 4, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yatafuta muarobaini wa kushuka kwa bei ya mafuta ya kula

Na Doreen Aloyce, Timesmajira online,Dodoma

SERIKALI imekutana na wadau wa kuzalisha mafuta ya kupikia kwa ajili ya kujadili changamoto zinazosababisha kushuka kwa bei ya mafuta na alizeti nchini.

Kikao hicho kimefanyika Mei 23, 2023 kilichowakutanisha Mawaziri kutoka Wizara tatu akiwemo Waziri wa Viwanda , Biashara na Uwekezaji Dkt.Ashatu Kijaji , Waziri wa Kilimo Husssein Bashe na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt.Mwigulu Nchemba.

Akifungua kikao hicho Waziri wa Uwekezaji, Viwanda,Biashara na Uwekezaji Dkt. Ashatu Kijaji amesema lengo la kikao hicho ni kuongea kwa pamoja,kuboresha maisha,kuchangia uchumi wa taifa na hatimaye kuzalisha mafuta ambayo yatajitosheleza ili kuacha kutumia fedha za kigeni kuagiza mafuta nje ya nchi.

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Dkt.Ashatu Kijaji katikati akiwa na Waziri wa Kilimo Husssein Bashe kushoto pamoja na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt.Mwigulu Nchemba kulia katika kikao kilichowakutanisha wazalishaji wa mafuta ya kula nchini hapa kilichofanyika jijini Dodoma.

Amesema kuwa kwa sasa zao la alizeti limeshuka kwa asilimia 50 na mafuta ya kupikia kwa asilimia 17 jambo ambalo limesababisha wananchi hususani wakulima kuwa na malalamiko hivyo serikali ikaona wajadiliane ili kwenda pamoja .

“Tuna viwanda 771 vinavyochakata mafuta , tunazalisha tani laki tatu na mahitaji yetu ni tani laki tano na sitini hivyo mafuta bado hayatoshi hali inayopelekea kuruhusu wenzetu walete kutoka nje ya nchi, kupitia hali hiyo Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan akaelekeza tuwe na mikoa mitatu ya kilimo cha alizeti ndani ya taifa letu ambayo ni Dodoma, Singida na Simiyu lengo ni kutafuta malighafi ya kutosha,”amesema Dkt Kijaji.

Pia amesema kuwa nguvu imewekwa kwa wakulima ambao wameweza kuzalisha alizeti ya kutosha lengo ilikuwa kufikia uchumi shirikishi na kwamba kupitia kikao hicho wataondoa changamoto ili kukuza uchumi wa pamoja.

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Dkt.Ashatu Kijaji akiongea kwenye kikao kilichowakutanisha wazalishaji wa mafuta ya kula hapa nchini kilichofanyika jijini Dodoma.

Naye Waziri wa Fedha na Mipango Dkt.Mwigulu Nchemba amesema kuwa ili kuondokana na changamoto hiyo kuna haja ya kutengeneza sera ya kuwakuza kiuchumi hivyo ndani ya miaka mitatu serikali haitaagiza mafuta nje ya nchi.

Amewataka wazalishaji wa mafuta ya alizeti kuwaripoti maofisa wa serikali wanaowataka kutoa rushwa ili waweze kuchukuliwa hatua.

“Natamani tufanye vizuri sisi wazalishaji tuondoke kwenye umimi bali wote tuangalie tunapata nini kwenye huu mnyonyoro wa thamani,viwanda vilivyofungwa inasikitisha sana wengine ni vitisho vya hao maofisa wa serikali ambao mnashindwa kuwaripoti,” amesema Dkt. Mwigulu.

Waziri wa Kilimo Hussein Bashe,akiongea kwenye kikao kilichowakutanisha wazalishaji wa mafuta ya kula hapa nchini kilichofanyika jijini Dodoma.

Kwa upande wake Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amesema kuwa wazalishaji wa mafuta wanapaswa kukutana wao kukaa kwa pamoja kuchagua uongozi mzuri ambao utawasaidia kuwaunganisha na serikali.

“Ninachotaka kuwaambia hapa mbele ya Waziri ni kwamba wachakataji wa mafuta ya alizeti waazishe taasisi ambayo itakuwa na umahili na sio chama cha uanaharakati kwani imekuwa chanzo cha serikali kutokuwa kitu kimoja,” amesema Bashe.

Nao washiriki wa kikao hicho wamesema kuwa kupitia kikao hicho wanategemea mapinduzi makubwa ili waweze kufanya uzalishaji ulio bora.

Aidha washiriki hao akiwemo Meneja wa Kampuni ya Mount Meru Millas,Nelson Mwakabuta na Fatuma Salum mzalishaji wamesema kuwa wamefurahishwa na kikao hicho na wana uhakika changamoto zilizowakabili ikiwemo upungufu wa malighafi na masoko yanaenda kupatiwa ufumbuzi.

“Tunaona taswira njema kupitia kikao hiki kwani tutapata mbegu ya uhakika , kiwanda kufanya kazi kwa muda mrefu bila kutegemea msimu,” amesema Nelson Mwakabuta.

Baadhi ya washiriki wa kikao kilichowakutanishaserikali na wazalishaji wa mafuta ya kula hapa nchini kilichofanyika jijini Dodoma.

Hata hivyo kikao hicho kimeleta tija kwa wazalishaji wa mafuta kutokana na majibu na mikakati iliyotolewa na serikali huku wakiomba ushirikiano pande zote mbili jambo ambalo litasaidia kuinua uchumi wa nchi.