December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yasisitiza ushirikiano kukabili vifo vya wajawazito na watoto

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima ametoa wito kwa wadau wa maendeleo nchini kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali kuboresha miundombinu rafiki ili kupunguza vifo vya wajawazito na watoto.

Dk Gwajima amesema hayo leo kwenye mkutano wa mwaka wa tathimini ya utekelezaji wa kitita cha uzazi salama kiancholenga kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi uliofanyika jijini Mwanza na kusisitiza ushirikiano unahitajika katika kuboresha vifaa tiba, vituo vya afya na huduma.

Amesema hadi sasa kuna vituo zaidi ya 8,530 vya kutolea huduma za Afya ukijumlisha Hospitali, Vituo vya Afya na Zahanati, hivyo vituo 30 kwenye mikoa 5 havitoshi katika kuendana na kasi ya kufikia malengo endelevu ya mwaka 2030.

Ameeleza serikali inalenga ifikapo 2030 ni kufikia vifo vitokanavyo na uzazi chini ya 70 kwa vizazi hai 100,000 kutoka 566/100,000 kwa takwimu za mwaka 2015/16 na kupunguza vifo vya watoto wachanga hadi kufikia angalau vifo 12 kwa vizazi hai 1,000 toka 25/1,000 kwa takwimu 2015/16.
Dk Gwajima amesema tathmini ya mwaka juu ya utekelezaji wa mradi wa Kitita cha Uzazi salama hapa Tanzania inafanyika takribani wiki moja tangu kufanyika kwa Mkutano wa Mwaka wa Kisayansi uliolenga kuongeza kasi katika kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto wachanga hapa nchini.

Amesema Mradi wa Kitita cha uzazi salama “SaferBirths Bundle of Care” unalenga kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi, watoto wanaozaliwa wafu na vifo vya watoto wachanga kwa kutekeleza afua zinazoendana na vipaumbele na miongozo ya Serikali.

Dk Gwajima amesema Mradi huo wa miaka mitatu, ulianza Oktoba 2020, utakamilika mwezi Septemba, 2023. Shughuli mahususi za mradi huu zinatekelezwa kwenye vituo vya kutolea huduma 30, kuanzia mikoa mitano ambayo ni Mwanza, Manyara, Tabora, Geita na Shinyanga.

Kwa upande wake Barozi wa Norway Nchini Tanzania, Elizabeth Jacobsen alipongeza waandaji na washiriki wa hafla hiyo ikiwemo Hydom Hospital kwa kuandaa hafla hiyo na kuwakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya afya kulenga kupunguza vifo vya wajawazito na watoto.

Alisema ushirikiano wa pamoja utasaidia kuifanya Tanzania kuwa eneo salama kwa mama na mtoto na kulifanya taifa kuweza kumudu gharama za raslimali muhimu katika huduma ya afya ikiwemo watumishi, vifaaa tiba na elimu.

Alisema serikali ya Norway kwa ushirikiano na wadau tofauti ulimwenguni kupitia Mfuko wa Kimataifa wa Ufadhili wa Wanawake, Watoto na Vijana (GFF) wanaendelea kuunga mkono juhudi za serikali ya Tanzania kukabili vifo vya wajawazito na watoto.