May 21, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yaridhishwa utekelezaji shamba la mbegu ya mpunga Mngeta

Na Joyce Kasiki,timesmajira online,,Chita

WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Innocent Bashungwa amesema,Serikali imeridhishwa na kazi inayofanywa na Jeshi ya Kujenga Taifa (JKT) katika shamba la Mbegu ya mpunga lililopo wilayani Kilombero na kumuhakikishia Mkuu wa JKT Meja Jenerali Rajab Mabele kwamba shamba hilo lItaendelea kubaki mikononi mwao ili kuleta tija zaidi katika uzalishaji wa mbegu ya zao hilo.

Akizungumza wakati akikagua shamba hilo ,Waziri Bashungwa amesema,kuna baadhi ya watu ambao wamekuwa wakihamasisha ili shamba hilo ambalo lilinyang’anywa kutoka kwa mwekezaji,lirudi tena mikononi kwa mwekezaji jambo ambalo amesema haliwezekani.

“Shamba hili lilikuwa linamilikiwa na mwekezaji na mwaka oktoba  2021 lilichukuliwa na serikali na kupewa JKT na sasa tumeona matunda yameanza kuonekana,kwa hiyo wale watu wanaotegemea  shamba hili litarudi mikononi mwa wawekezaji hilo wasahau, kwa sababu umeonyesha faida kubwa kwa wananchi na serikali.”amesema Bashungwa

Amesema,moja ya mafanikio ambayo yameonekana katika mradi wa shamba la mbegu la Mpunga la Mngeta  ni pamoja na uzalishaji wa mbegu za zao la Mpunga ambazo huzitawanya katika vikosi vya JKT pamoja na maeneo mbalimbali kwa ajili ya wakulima kuzitumia.

Amesema mashamba hayo yalitolewa kwa JKT kwa sababu ya kutokuwa na usimamizi wowote baada ya mwekezaji kushindwa kuyandeleza kwa muda mrefu.

“Serikali iliamua kuyatoa kwa JKT ili yafanyiwe kazi na kuleta tija kwa wananchi, kama mnavyoona zao la mpunga lilivyostawi na shughuli za kilimo zinaendelea kama kawaida,”alisema Bashungwa.

Kutokana na hilo Bashungwa amesema asitegemee mtu yoyote kama mashamba hayo yatarejeshwa kwa wawekezaji na kuwataka JKT kuendelea kuchapa kazi ikiwemo kutokuwa na wasiwasi wowote kuhusu kuchukuliwa kwa shamba hilo.

Bashungwa amesema,awali mkulima na mzalishaji mbegu walikuwa wanasubiri mvua inyeshe ndipo waanze taratibu za kuzalisha na kulima,ilihali wanatakiwa kupishana lakini hivi sasa tunakoelekea,tatizo hilo halitakuwepo kwa sababu JKT ambaye ni mzalishaji anatangulia kuzalisha mbegu kupitia mradi huo,na msimu wa mvua unapowadia mkulima anaipata mbegu kwa wakati sahihi.

Kutokana na hilo Waziri Bashungwa amesema jitihada za serikali zinaonekana kwenye kuhakikisha usalama wa chakula unakuwepo ikiwemo kuzalisha chakula cha ziada ambacho kitauzwa nje, lakini pia wakulima wananufaika kwa kuendesha kilimo chenye tija ambacho kitawainua kiuchumi.

Kwa mujibu wa Bashungwa  uwepo wa JKT katika mradi wa Mgeta Plantation kumesaidia kwa kiasi kikubwa kutunza mazingira ya vyanzo vya maji,ambapo vyanzo hivyo vinasaidia kupeleka maji katika Bwawa la Mwalimu Nyerere ambalo serikali imewekeza fedha nyingi kwa ajili ya kuhakikisha wanazalisha umeme wa kutosha.

“Lazima Mgeta Plantation iendelee kulindwa kwa sababu inaleta faida kubwa kwa taifa na wananchi kwa ujumla,”alisema Bashungwa.

Hata hivyo amemuagiza Mkuu wa JKT,Meja Jenerali Rajabu Mabele kuwasilisha vipaumbele vyao katika miradi wanayotekeleza ili aweze kuiwasilisha Bungeni, kwa ajili ya kuweka katika bajeti ijayo.

Kwa upande wake Mkuu wa JKT Meja Jenerali Rajabu Mabele ameishkuru serikali kutokana na kutoa sapoti kwa JKT ili kuhakikisha wanatekeleza miradi yao ipasavyo,ikiwemo kufikia malengo yao ifikapo 2025 wajitegemee kwa chakula.

Meja Jenerali alimuhakikishia Waziri na serikali kwa ujumla kuwa JKT itaendelea kuzalisha mbegu pamoja na vyakula ili kuhakikisha Jeshi hilo lnajitegemea kwa chakula kama walivyojiwekea kwenye mikakati yao.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Dustan Kyobya aliwataka wananchi kutumia fursa ambazo zinatolewa na Jeshi hilo ka ajili ya kujiongezea kipato kwenye kilimo ambacho wanafanya katika maeneo mbalimbali ya Kirombelo.

Amesema uwepo wa JKT umeonyesha faida kubwa kwa wananchi kwa sababu sababu wanapata mbegu kutoka kwa Jeshi hilo lakini pia kuna uwepo wa ulinzi wa vyanzo vya maji ambavyo vinawazunguka.