January 9, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yaokoa Bilioni 2.7/- ukaguzi wa magari ndani ya nchi

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online, Dar

SERIKALI kupitia Shirika la Viwango Tanzania (TBS) imeokoa sh. bilioni 2.7 tangu ilipoanza kufanya ukaguzi wa magari ndani ya nchi kuanzia Aprili hadi Agosti 3, mwaka huu fedha ambazo kwa utaratibu wa awali wangelipwa mawakala waliokuwa wakifanyakazi hiyo nje ya nchi.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Profesa Kitila Mkumbo jijini Dar es Salaam leo alipofanya ziara katika vituo viwili vya ukaguzi wa magari yanayotoka nje, kimoja kikiwa bandarini na kingine UDA.

Profesa Mkumbo amesema; “Jambo hili ni zuri, kwani katika kipindi cha Aprili hadi Agosti 3, mwaka huu TBS kwa niaba ya Serikali wamekusanya takribani sh. bilioni 3.9, kwenye fedha hiyo kama wangeendelea na utaratibu wa zamani shirika kwa niaba ya Serikali lingepata asilimia 30 na asilimia 70 (sawa na sh. bilioni 2.7) zingebaki kwa mawakala waliokuwa wakifanyakazi kazi hiyo.”

Amesema Serikali kwa kuamua kutekeleza mpango huo inaokoa fedha nyingi ambazo zilibaki nje, kwani kwa kipindi cha takiribani miezi mitatu wamekusanya sh. bilioni 3.9 na fedha hiyo inaingia Mfuko Mkuu wa Serikali, kwa hiyo hilo ni jambo kubwa.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Profesa Kitila Mkumbo (Kushoto) akisikiliza maelezo kutoka kwa mmoja wa maofisa wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kuhusu ukaguzi wa magari unaofanyika nchini.

Ameongeza kuwa zoezi hilo linakwenda vizuri na wanafurahishwa, kwani TBS wamejipanga vizuri na wanatekeleza jukumu hilo kwa umakini mkubwa.

“Nafurahi utaratibu huu unazidi kuimarika ambapo taarifa ambayo nimeipata hadi kufikia Agosti 3, yalikaguliwa magari 11, 179 na kati ya hayo, magari 7,707 yalikidhi ubora na mengine ambayo yalibaki yalienda kutengenezwa kwenye gereji zetu zinazomilikiwa na Watanzania,”amesema Profesa Mkumbo.

Amesema jambo la pili kupitia mpango huo vijana wengi wameajiriwa kwa ajili ya kufanyakazi ya ukaguzi wa magari hayo, lakini pia na kwenye magereji kunachangamka maana wanapata kazi za kufanya.

“Kwa hiyo niwaombe Watanzania waendelee kuunga mkono shughuli hii. Lakini natoa wito kwa wananchi wanaoagiza magari na wafanyabiashara wanaofanyakazi ya kuondoa magari bandarini kwamba utaratibu huu ni mzuri, waendelee kutoa ushirikiano pale ambapo kuna upungufu watueleze kama ambavyo wamekuwa wakifanya na sisi kupitia TBS tunafanya marekebisho, tunaamini kwamba baada ya muda mambo yataboreshwa vizuri zaidi ,”amesema.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Profesa Kitila Mkumbo (Katikati aliyenyosha mkono) akisisitiza jambo leo alipofanya ziara kwenye vituo vya ukaguzi wa magari kutoka nje bandarini na UDA.

Naye Meneja wa Ukaguzi wa Bidhaa Zinazotoka Nje wa TBS, Saidi Mkwawa, amesema kwa mapato hayo ya sh. bilioni 3.9 ambayo yametokana na ukaguzi huo, kama ukaguzi ungekuwa unafanyika nje ya nchi, Serikali ingepata asilimia 30 ambazo ni sawa na sh. bilioni 1.3.

Amesema kwa mapato hayo ya sh. bilioni 3.9 Serikali imeweza kuokoa sh. bilioni 2.7 zilizokuwa zinabaki nje na hiyo inaonesha ni kwa kiasi gani TBS inatekeleza maelekezo ambayo imepewa na Serikali ya Awamu ya Sita, ambayo inasisitiza kuboresha biashara na kukusanya mapato.

Mkwawa amesema magari ambayo hayakufaulu katika hatua ya awali ya ukaguzi na kuhitaji marekebisho yamenufaisha Watanzania, kwani matengenezo yanafanyika kwenye ngereji ambazo zinamilikiwa na Watanzania tofauti na hapo nyuma ambapo yangetengenezwa nje ya nchi.

“Kwa hiyo inaonesha jinsi gani dhamira yetu ya kukuza biashara inatimia na tumeamua kufanyakazi kwa weledi,” alisisitiza Mkwawa.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dkt. Yusuf Ngenya (Aliyesimama), akimkaribisha Waziri wa Viwanda na Biashara, Profesa Kitila Mkumbo, alipofanya ziara katika vituo viwili vya bandarini na UDA kujionea ukaguzi wa magari unavyofanyika hapa nchini.

Kabla ya utaratibu huo kuanza Aprili, mwaka huu magari yote yalikuwa yanakaguliwa nje na yalikuwa yanaletwa nchini yakiwa na cheti cha ubora na kuidhinishwa TBS kwa kuruhusiwa kutumika nchini.