November 15, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yakiri tatizo watoto wanaoishi, kufanyakazi mitaani

Na Joyce Kasiki, TimesMajira,OnlineDodoma

SERIKALI imesema pamoja na jitihada mbalimbali za kukabiliana na tatizo la watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani na ombaomba, lakini bado changamoto hiyo ni kubwa hapa nchini.

Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt.Dorothy Gwajima, ameyasema hayo juzi wakati akifungua kikao cha kujadili na kuweka mikakati ya pamoja ya kushughulikia tatizo la watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani.

“Kwa msingi huu tumeona ni vyema kuwa na kikao hiki chenye wadau muhimu ili tuweze kujadili na kuwa na mkakati wa pamoja unaolenga kuondoa changamoto hii na ni imani yangu kikao hiki kitatoka na mkakati utakao tusaidia kutatua changamoto hii kwa maslahi mapana ya watoto wetu na Taifa kwa ujumla,” amesema Dkt.Gwajima

Aidha, amesema kundi la kundi la watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani liko katika hatari ya kutumikishwa katika magenge yasiyofaa ya kihalifu na kwamba ni vyema kundi hilo liangaliwe kwa jicho pana na la kipekee, kwani kwa kufanya hivyo itasaidia kuwaokoa watoto hao kwa faida yao wenyewe, kwa familia zao na Taifa zima kwa ujumla.

“Kikao hiki ni cha muhimu sana kwetu kwani kitatusaidia kujadili na kuwa na mkakati wa pamoja wa namna bora ya kuondokana na changamoto hii.” amesisitiza

Amesema lengo kuu la kuwa na mkakati wa pamoja ni kuwa na mtazamo wa pamoja unaounganisha nguvu kwa lengo la kumaliza kama siyo kupunguza changamoto hiyo.

Ametumia nafasi hiyo kuwataka wajumbe wa mkutano huo kuhakikisha wanaandaa mkakati unaotekelezeka na kuwa na tija kwa vizazi vijavyo.

Aidha ameagiza kufanyika zoezi la utambuzi wa watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani na omba omba katika mikoa yote pamoja na kuhakikisha kuwa watoto hao wanarejeshwa katika jamii zao .

Ameagiza elimu itolewe kwa jamiii ili waepukane na kutoa fedha kwa ombaomba, kwani inahamasisha ombaomba wakiwemo watoto kuwepo mitaani.

Kingine amesema ni elimu sahihi ya malezi kwa familia na jamii na kuondoa mila potofu zinazochangia kuongezeka kwa matendo ya ukatili, ambayo hupelekea watoto kukimbilia mtaani.

Ameshauri Mamlaka za Serikali za Mitaa zitunge sheria ndogo kwa ajili ya kusimamia afua za kudhibiti suala la watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani pamoja na ombaomba.

Pia ameziagiza halmashauri kusimamia wadau na kuwaelekeza badala ya kuwapatia misaada watoto wakiwa mitaani, waelekeze huduma na misaada kwenye familia na makao ya watoto.

Dkt.Gwajima ameziagiza Serikali ngazi za vijiji/mitaa kusimamia familia ili wazazi/walezi waweze kutoa malezi sahihi, kuimarisha uratibu kupitia kamati za MTAKUWWA,kuwatambua na kuwaunganisha watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani na mafunzo ya ufundi stadi kama sehemu ya marekebisho ya tabia na kujenga stadi za maisha.

Amesema,watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani ni moja ya makundi ya watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi yaliyoainishwa katika Sheria ya Mtoto Na. 21 ya 2009 na kufanyiwa marekebisho mwaka 2019.

“Kutokana na mazingira wanayoishi hujikuta katika hatari ya kukumbana na changamoto mbali mbali ikiwemo kuingia katika mkinzano na sheria kutokana na kutokuwa na uangalizi madhubuti na uhakika wa kupata mahitaji muhimu kama vile chakula, mavazi, malazi na afya,”amesema.

Pia amesema,wapo wengine wanaokumbana na vitendo vya ukatili vikiwemo kubakwa na kuingiliwa kinyume na maumbile. Pia miongoni mwa watoto hao wapo wanaingia katika kundi la ombaomba ambapo hutumia fedha wanazopata kujikimu mahitaji yao.

Dkt. Gwajimu amesema kwa takwimu Tanzania inakadiriwa kuwa na idadi ya watoto 35,919 wanaoishi na kufanya kazi mitaani katika majiji na miji mbalimbali hapa nchini (Taarifa ya TAMISEMI, 2018).

Tafiti mbalimbali zimefanyika ili kubaini hali halisi ya watoto hawa mathalani “Head Count Survery” ya mwaka 2017 katika mikoa ya Mwanza, Dodoma, Arusha, Mbeya, Iringa na Dar es Salaam ambapo ilibaini watoto 6,393 walikuwa wanaishi na kufanya kazi mtaani.

Zaidi ya asilimia 90 ya watoto hao wazazi au walezi wao wanafahamika wanapoishi.