Na Dorina Makaya
SERIKALI imeiagiza Kampuni ya Uhifadhi Mafuta (TIPER), kuhakikisha inatoa taarifa za uendeshaji wa kampuni hiyo kwa wakati, ili kuepusha changamoto ambazo zinaweza kujitokeza baadaye kutokana na kutokutoa taarifa kwa wakati.
Agizo hilo limetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali wakati wa ziara yake kwenye kampuni hiyo iliyolenga kujionea hali halisi ya uendeshaji wa Kampuni ya TIPER.
Katika ziara hiyo, Naibu Katibu Mkuu Mahimbali ametembelea kwenye maeneo mbalimbali ya kampuni hiyo ikiwa ni pamoja na matenki ya kuhifadhia mafuta, jambo ambalo alionyesha kuridhishwa na utendaji kazi wa Tiper.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa TIPER, Michael Mjinja ameishukuru serikali kwa kufika katika eneo hilo ambapo waliweza kukubaliana masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupeana taarifa kwa wakati.
Amesema licha ya mafanikio waliyonayo, bado kuna changamoto zinazowakabili huku kubwa ikiwa kuharibika kwa vifaa vya kusukuma mafuta pindi wanapoyatoa kwenye meli, vifaa ambavyo havipatikani nchini hadi viagizwe nje ya nchi.
Kutokana na hali hiyo, Mahimbali amesema endapo taarifa hizo zitatolewa mapema itakuwa mwarobaini wa changamoto hizo.
Ziara hiyo ni mwanzo wa ziara nyingine katika taasisi zote zenye ubia na serikali kwenye sekta ndogo ya mafuta nchini kwa lengo la kuboresha ufanisi na utendaji.
Katika ziara hiyo, Naibu Katibu Mkuu huyo ameambatana na baadhi ya viongozi na wataalamu kutoka Wizara ya Nishati, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji nchini (EWURA) na Kampuni ya Serikali ya Uagizaji na Usambazaji wa Mafuta (TANOIL).
More Stories
Bodaboda wamchangia Rais Samia Mil 1 ya fomu ya Urais
HAYA HAPA MATOKEO YOTE FORM II NA DARASA LA IV
Ufaulu waongezeka matokeo ya Darasa la Nne na Kidato cha Pili