July 2, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yahimiza matumizi ya Usuluhishi kutatua migogoro

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

Serikali imewahimiza Watanzania kutumia zaidi njia mbadala za utatuzi wa migogoro, hususan usuluhishi, badala ya kukimbilia mahakamani, ikieleza kuwa mfumo huo husaidia pande zote zinazohusika kufikia maridhiano na kuridhika na matokeo ya mchakato huo.

Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Zainab Katimba,jana alipotembelea banda la Wizara ya Katiba na Sheria katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), ambapo pia alishiriki kutoa huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi.

Katimba amesema wizara hiyo imeendelea kutumia maonesho hayo kama fursa ya kuwafikia wananchi kwa kuwapatia elimu ya sheria na huduma za msaada wa kisheria ili kuongeza uelewa kuhusu haki zao na namna ya kuzidai kwa njia sahihi.

“Nitumie fursa hii kuwakaribisha Watanzania wote wenye changamoto za kisheria kufika katika banda la Wizara ya Katiba na Sheria ili waweze kupata huduma za msaada wa kisheria,” amesema.

Akizungumzia umuhimu wa usuluhishi, Katimba amesema pamoja na mahakama kuwa na mamlaka ya kikatiba ya kusimamia utoaji wa haki, Serikali inaamini njia mbadala za utatuzi wa migogoro zina mchango mkubwa katika kujenga maridhiano, kuimarisha mshikamano na kudumisha amani katika jamii.

“Tunaamini kwamba usuluhishi ni njia inayowafanya wale wenye migogoro waridhiane na kutoka wote wakiwa washindi, tofauti na mfumo wa mashauri mahakamani ambapo mara nyingi hupatikana mshindi mmoja na mwingine kushindwa,”amesema.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri huyo amesema Serikali imeanza rasmi utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 sambamba na mwaka mpya wa bajeti wa 2026/2027, hali inayohitaji mapitio makubwa ya sheria ili ziendane na mahitaji ya maendeleo ya sasa na ya baadaye.

Amesema Tume ya Marekebisho ya Sheria imepewa jukumu la kuhakikisha sheria zote za nchi zinaendana na mwelekeo mpya wa maendeleo na mageuzi yanayotarajiwa kupitia Dira 2050.

“Kuna mabadiliko makubwa tunayotarajia kuyatekeleza kupitia Dira 2050, na mafanikio yake yanategemea uwepo wa sheria zinazowezesha utekelezaji wake,” amesema.

Katimba pia amesisitiza umuhimu wa kuzingatia maendeleo ya teknolojia katika mchakato wa kutunga na kurekebisha sheria, akibainisha kuwa Tanzania inaelekea kwenye uchumi wa kidijitali unaotegemea zaidi mifumo ya kisasa ya kifedha na matumizi madogo ya fedha taslimu.

“Tunapaswa kuhakikisha sheria zetu zinaendana na maendeleo ya teknolojia. Tunaelekea katika uchumi wa kidijitali na matumizi ya mifumo ya kisasa ya kifedha, hivyo sheria lazima ziwezeshe mabadiliko hayo,” amesema.