July 2, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

JAB yatoa huduma sabasaba Dar es Salaam

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

WADAU wa sekta ya habari na wananchi kutoka maeneo mbalimbali wanaendelea kupata huduma katika banda la Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), banda lilipo katika kijiji cha Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwenye Maonesho ya 50 ya kimataifa ya biashara ya Dar es Salaam sabasaba.

Maonesho hayo yanaendelea katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Barabara ya Kilwa, jijini Dar es Salaam.

Afisa habari mkuu wa bodi, Editha Mayemba, amesema huduma zinazotolewa ni pamoja na ugawaji wa vitambulisho vya ithibati kwa waandishi waliokidhi vigezo.

Amesema huduma nyingine ni usajili waandishi wa habari, marekebisho ya taarifa za usajili, pamoja na utoaji wa elimu kuhusu majukumu na huduma mbalimbali zinazotolewa na Bodi hiyo na kuwa huduma zote zinaendana na Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229.

Amesema JAB inawakumbusha waandishi wa habari na wadau wote wa sekta ya habari kutumia fursa ya maonesho hayo ambapo amesema lengo ni kupata huduma kwa haraka na kwa ukaribu.

Amesema huduma hizo zinaendelea sambamba na zile zinazotolewa katika Makao Makuu ya Bodi kwa wale wasioweza kufika sabasaba.

Amesema picha zilizopigwa leo zinaonesha maafisa wa JAB wakitoa huduma kwa wadau na wananchi waliotembelea banda la Bodi.