Na Joyce Kasiki
WAZIRI wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, amepongeza juhudi zinazofanywa na Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) za kupanua wigo wa elimu kupitia programu za ujasiriamali na stadi za biashara zinazolenga makundi mbalimbali, ikiwemo wafungwa wanaokaribia kumaliza vifungo vyao.
Balozi Omar alitoa pongezi hizo Julai 2, 2026, baada ya kutembelea banda la IAA lililopo ndani ya banda la Wizara ya Fedha kwenye Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba).
Akizungumza mbele ya Waziri huyo, Mkuu wa Kitengo cha Ushirikiano wa Kimataifa, Uhusiano na Masoko wa IAA, Sarah Goroi, alisema chuo hicho kwa sasa kinaendesha shughuli zake kupitia kampasi sita zilizopo Arusha, Kigoma, Babati, Songea, Dar es Salaam na Bukombe, huku maandalizi ya kufungua kampasi Zanzibar yakitarajiwa kukamilika kabla ya Oktoba mwaka huu.
Alieleza kuwa IAA ina zaidi ya wanafunzi 25,000 na inaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali ili kuimarisha utoaji wa mafunzo ya ujasiriamali pamoja na stadi za biashara kwa makundi tofauti ya jamii.
Goroi alibainisha kuwa miongoni mwa washirika wa chuo hicho ni Jeshi la Magereza Ukonga, ambapo wafungwa wanaokaribia kuhitimisha vifungo vyao hupatiwa mafunzo maalumu ya kuwawezesha kujiajiri na kupata kipato halali wanaporejea kwenye jamii.
Alisema mafunzo hayo hutolewa ndani ya kipindi cha miezi sita kabla ya wafungwa kuachiwa huru, yakilenga kuwajengea uwezo wa kujitegemea na kupunguza uwezekano wa kurejea tena gerezani.

More Stories
Balozi Omar akoshwa na usimamizi matumizi ya Moduli
GASCO yaeleza majukumu sabasaba, yaboresha miundombinu Gesi
Mipango haiwezekani bila Takwimu