Na Zena Mohamed,TimesmajiraOline,Dodoma
SERIKALI kwa kushirikiana na Wadau imegawa vifaa vya TEHAMA vyenye thamani ya jumla ya Mil. 769 kwa shule za msingi na sekondari 19 katika mikoa tisa ambayo ni KusiniUnguja– Zanzibar, Dodoma, Iringa, Ruvuma, Arusha, Geita, Kilimanjaro, Mbeya na Mtwara.
Akizungumza katika hafla ya ugawaji wa vifaa vya TEHAMA kwa shule za Msingi na Sekondari nchini jijini hapa leo Machi 30,2026 Naibu Waziri wa Elimu Wanu Hafidh Ameir,alisema uwekezaji huo ni muendelezo wa dhamira ya Serikali katika kuimarisha sekta ya elimu nchini.
“Matumizi ya vifaa hivi yataongeza uelewa kwa wanafunzi kwa kuwapa fursa ya kujifunza kwa vitendo na kwa kuona, hususan katika masomo ya sayansi na teknolojia. Kwa upande wa walimu, teknolojia hizi zitawawezesha kutumia mbinu bunifu za ufundishaji, kuandaa maudhui kwa ufanisi zaidi na kufuatilia maendeleo ya wanafunzi kwa urahisi kupitia mifumo ya kidijitali,”amesema Wanu.

Aidha amesema kuwa Wizara hiyo inaendelea kwa dhati kutekeleza mageuzi makubwa katika sekta ya elimu, kama yalivyoainishwa katika Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 (Toleo la 2023) pamoja na mitaala iliyoboreshwa. Lengo ni kuboresha ubora wa elimu na kuandaa rasilimali watu yenye ujuzi, maarifa na stadi zinazokidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye.
“Katika kufanikisha hilo Serikali inaendelea na
Utekelezaji wa elimu ya lazima ya miaka 10, ili kuhakikisha kila mtoto anapata elimu ya msingi na sekondari ya chini bila kukatishwa,Mkondo wa elimu ya amali, unaolenga kuwapatia wanafunzi stadi za ufundi, ujasiriamali na ubunifu, na hivyo kupanua fursa za ajira na kujiajiri,Matumizi ya teknolojia za kidijitali, katika ufundishaji, ujifunzaji na usimamizi wa elimu, ili kuongeza ufanisi na ubora wa huduma za elimu na
Mafunzo ya ualimu, ili kuhakikisha walimu wanapatiwa mafunzo ya kisasa yanayowawezesha kufundisha kwa ufanisi masomo ya sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati (STEM),”amesema.
Amesema ili kufanikisha hilo, Serikali imeandaa na kuanza kutekeleza Mkakati wa Kitaifa wa Matumizi ya Teknolojia za Kidijitali katika Elimu pamoja na miongozo yake, ikiwemo Mwongozo wa matumizi ya TEHAMA katika shule na vyuo vya ualimu na Mwongozo wa matumizi ya Akili Unde (AI) katika elimu.
“Mkakati huu unalenga kujenga mfumo wa elimu wa kisasa, jumuishi na unaotumia teknolojia kwa ufanisi katika ufundishaji, ujifunzaji, tathmini na usimamizi wa elimu. Vilevile, unalenga kuongeza upatikanaji wa rasilimali za kidijitali, kukuza ujuzi wa TEHAMA, na kuhakikisha elimu inaendana na mahitaji ya karne ya 21,”amesema
Pamoja na hayo Wanu amesema Serikali inaendelea pia kuboresha mazingira ya ujifunzaji kwa kuwekeza katika teknolojia za elimu, ikiwemo madarasa janja, mbao janja, vishikwambi na kompyuta katika shule mbalimbali nchini. Mathalani, katika mwaka wa fedha 2025/26, Serikali imeanzisha madarasa janja Matano (05) na kufunga mbao janja mia nne ishirini na mbili (422) katika shule za sekondari.


More Stories
Mbega ataka viongozi kuimarisha ulinzi kudhibiti wageni
Mbega ataka viongozi kuimarisha ulinzi kudhibiti wageni.
Kero za Walimu kutoshughulikiwa kwa wakati chanzo Cha msongo wa mawazo-CWT