May 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yafunga kamera 306 ukuta wa madini Mirerani

Mary Margwe na Pamela Mollel,TimesMajira Online,Simanjiro

SERIKALI imefanikisha kufunga mfumo wa CCTV kamera 306 kuzunguka mgodi wa madini ya Tanzanite mjini Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara.

Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila wakati akipokea mradi kuimarisha usalama eneo tengefu la machimbo ya madini ya Tanzanite mjini Mirerani kwa kutumia Mfumo wa Usalama ( CCTV Camera System ) katika ukuta na majengo yaliyopo katika mgodi pekee wa madini ya Tanzanite Mirerani, ambavyo vinafanya kazi nyakati zote za mvua, vumbi na baridi.

Profesa Msanjila aliyekuwa mgeni rasmi katika shughuli hiyo amesema, baada ya mradi wa ujenzi wa ukuta kukamilika na katika kuimarisha ulinzi kwenye eneo la machimbo ya madini ya Tanzanite Mirerani ilionekana kuna umuhimu mkubwa wa kuweka mfumo wa CCTV kamera kwa lengo la kugundua vitu na watu wanaoingia eneo la ukuta, kuhifadhi taarifa za kudumu, kuzuia wanaokusudia kufanya uhalifu na kufuatilia katukio yanayofanyika eneo la ukuta.

“Nimshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt.John Pombe Magufuli kwa miongozo makini anayotupatia katika kusimamia sekta ya madini ili kuhakikisha madini yetu yanawanufaisha watanzania, ni wazi kuwa kiongozi wetu huyu amekua mstari wa mbele katika kutoa maelekezo yenye lengo la kuhakikisha kuwa madini anaongezwa thamani hapa nchini,ushiriki wa watanzania katika uzalishaji na biashara ya madini unakua, wachimbaji wadogo wataendelezwa na kuongezeka kwa mchango wa sekta ya madini katika pato la Taifa,”amesema Katibu Mkuu.

Kufuatia uwekwaji wa mfumo huo wa CCTV kamera, amewataka wafanyakazi wa wizara na taasisi zilizo chini ya wizara kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kwa kuzingatia kanuni, na maadili ya utumishi wa umma, ambapo alitoa rai kwa wadau wote katika eneo hilo tengefu la Mirerani kujiepusha kabisa na vitendo vya rushwa na utoroshaji madini.

Aidha, Profesa Msanjila amesema, Februari 2019, wizara ilialika makampuni sita kwa ajili ya kushiriki zabuni ya usambazaji na ufungaji wa mfumo wa kamera za usalama katika ukuta wa migodi ya Tanzanite Mirerani ambapo wazabuni watano waliwasilisha gharama zao.

” Makampuni na watu mbalimbali walikuja wizarani na wengine waliletwa na taasisi za serikali kwa lengo la kutaka kupatiwa kazi ya kufunga mfumo wa CCTV kamera katika eneo hili la Mirerani, gharama walizowasilishwa zilikua kubwa sana, kwa mfano wapo waliowasilisha gharama ya sh.bilioni 83, bilioni 76, bilioni.33 na wengine bilioni 27 lakini kama wizara tulichambua na kuona gharama hizo kuwa ni kubwa sana na kuamua kutowapatia kazi, ndipo tulipoipatia kazi kampuni ya Starfix Enterprises kwa gharama ya shilingi bilioni 1.2,” amesema Profesa Msanjila.

Aidha, ameongeza kuwa baada ya kufanyika na kukamilika kwa taratibu za manunuzi kampuni ya Starfix Enterprises ilikidhi vigezo vyote vya zabuni hiyo na kusainiana mkataba na wizara kwa kiasi cha sh.bilionii 1.2.

Mbali na kazi hiyo wizara imekamilisha ujenzi wa jengo la wafanyabiashara wa madini (Brokers House), jengo la kituo cha pamoja (One Stop Centre) ndani ya ukuta wa Mirerani, uwekaji wa miundombinu ya umeme na taa kuzunguka ukuta umekamilika.

Amesema, ufungaji wa kamera za ulinzi ( CCTV ) kuzunguka eneo la ukuta wa migodi ya Tanzanite umekamilika na jana ndiyo waliupokea.

“Vilevile ujenzi wa jengo la scanner, ufungaji wa scanner na kuweka mfumo wa ‘biometric entrace’ unatarajia kuanza muda si mrefu, uwekezaji huu huu kwa pamoja unagharimu takribani kiasi cha sh.bilioni 4.2,”amesema.

“Lengo la hayo yote ni kuhakikisha kuwa shughuli zote zinazohusu biashara ya madini ya Tanzanite zinafanyika ndani ya ukuta, hatua hii inaimarisha upatikanaji wa takwimu sahihi, kudhibiti utoroshaji wa madini ya Tanzanite na kuongeza mapato ya serikali yatokanayo na madini ya Tanzanite,”amesema Profesa Msanjila.

Hata hivyo alisema kufuatia ujenzi wa miundombinu hiyo, mapato ya serikali yameongezeka kabla ya ujenzi kutoka sh.milioni 238 kwa mwaka 2016-2017 hadi kufikia sh.bilioni 3.587 kwa mwaka 2018-2019 ambapo miundombinu hiyo imewezesha kupatikana mawe ya Tanzanite kutoka katika mgodi wa Saniniu Kurian Laizer ambayo yalivunja rekodi ya uzito duniani wa kilo 9.27, 5.103 na 6.33 yenye jumla ya thamani ya sh.bilioni 12.590,689,974.94 huku Serikali ikijipatia mapato ya sh.milioni 919,120,368.17 kutoka malipo ya mrahaba, ada ya ukaguzi na ushuru.