May 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yaeleza hatua za zilizochukuliwa kushughulikia malalamiko ya waliokuwa wafanyakazi wa Kampuni ya Barrick

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.

Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu imesema imepokea na kushughulikia malalamiko ya waliokuwa wafanyakazi wa Kampuni ya Barrick ambao waliachishwa kazi kwa nyakati tofauti kuanzia mwaka 2007 yalihusiana na wafanyakazi kutopimwa afya wakati wa kuachishwa kazi, kutopatiwa huduma ya matibabu na kutopewa malipo ya fidia kutokana na ajali au magonjwa waliyoyapata kutokana na kazi.

Hayo yameelezwa jijini Dodoma na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo ,Prof.Jamal Katundu wakati akizungumza na waandishi wa habari na kusema kuwa malalamiko hayo yameshughulikiwa katika hatua mbali mbali, kupitia Wakala wa Usalama na Afya Mahali Pa Kazi (OSHA), Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) na Idara ya Kazi.

Amefafanua kuwa mbali na hatua hiyo wafanyakazi hao waliendelea kuwasilisha malalamiko katika mamlaka mbalimbali za Serikali wakidai kutoridhishwa na hatua zilizochukuliwa.

“Kutokana na hali hiyo, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu ilichukua hatua mbalimbali za kiutawala (administrative measures) ili kuyapatia ufumbuzi malalamiko hayo ikiwa  ni pamoja na kuunda Timu Maalum mwaka 2021 na 2022 zilizojumuisha wataalam kutoka katika Taasisi mbalimbali za Serikali, Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) kwa lengo kufanya uchambuzi wa kina wa malalamiko ya wafanyakazi hao na kutoa mapendekezo ya namna bora ya kuyahitimisha,”alisema

Katibu Mkuu huyo pia amesema timu husika zimeshughulikia jumla ya walalamikaji 427, kati yao walalamikaji 150 walishughulikiwa mwaka 2021 na 277 mwaka 2022 na kwamba kati ya walalamikaji 277 wa mwaka 2022, walalamikaji 47 walishashughulikiwa na Timu ya mwaka 2021.

“Mwaka 2022, kabla ya Timu kuanza kazi, mwezi Mei, 2022 Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu ilitoa tangazo kupitia Vyombo vya Habari kuwataka waliokuwa wafanyakazi wa Kampuni ya Barrick wenye malalamiko ambayo hayajawahi kuwasilishwa na kutolewa maamuzi na vyombo vya Serikali, kuwasilisha malalamiko yao ili yafanyiwe kazi,”amefafanua na kuongeza kuwa;

Timu iliyoundwa imekamilisha uchambuzi na kuwasilisha taarifa kwangu,Katika taarifa hiyo imeainishwa kuwa wapo walalamikaji waliobainika kuwa na magonjwa yanayotokana na kazi na hivyo mwajiri atawajibika kuwapatia matibabu, wapo wenye magonjwa yatokanayo na kazi na wamefikia ukomo wa kuimarika afya zao na hivyo mwajiri atatakiwa kuwafanyia taratibu za kuwalipa fidia,wapo pia waliobainika kuwa na magonjwa yasiyotokana na kazi,”amesema.

Aidha,kwa kuzingatia matokeo hayo, alisema walalamikaji wote waliowasilisha malalamiko yao watapatiwa majibu yao kwa barua ndani ya siku kumi za kazi baada ya kutoka tangazo ambapo Barua hizo zitatolewa kupitia Ofisi za Idara ya Kazi za Mikoa au Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kahama kwa kutumia anuani walizobainisha katika barua zao za malalamiko. Aidha, yeyote ambaye atapenda kupata barua kwa njia tofauti na zilizoelezwa, awasiliane na Ofisi ya Kamishna wa Kazi kupitia namba ya simu 0655 544 489.

“Ninapenda kutoa taarifa kuwa nimemtaka mwajiri kuweka Dawati/Ofisi maalum kwa ajili ya kusikiliza na kutatua malalamiko na kero za wafanyakazi na tayari nimearifiwa kuwa Mwajiri ameshatekeleza agizo hilo, amefungua Ofisi maalum katika eneo la Boomgate Bulyanhulu (Nje ya mgodi) hivyo, niwatake wale wote wenye malalamiko dhidi ya Kampuni ya Barrick kufika katika Dawati/Ofisi hiyo kuwasilisha malalamiko yao ili yaweze kufanyiwa kazi,”amesitiza

Pamoja na hayo alitumia nafasi hiyo kuutaka  Uongozi wa Kampuni hiyo kuandaa utaratibu wa namna ya kupokea malalamiko kwa kutoa namba ya simu maalum na watumishi ambao watashughulikia malalamiko.

“Aidha, Ninapenda kuchukua fursa hii kuwakumbusha Waajiri wote nchini kuwa Wakala wa Afya na Usalama Mahali Pa Kazi (OSHA) ndiyo yenye mamlaka kwa mujibu wa Sheria ya Usalama na Afya Mahali Pa Kazi Na. 5 ya 2003 ya kupima afya za wafanyakazi ili kubaini endapo wana madhara yaliyosababishwa na kazi wanazofanya,”amesema

Vile vile Katibu mkuu huyo alitoa rai kwa waajiri na wafanyakazi katika Sekta ya Madini kutekeleza wajibu na majukumu yao kwa Uadilifu na kufuata misingi ya kitaaluma kwa lengo la kudumisha Mahusiano mema pahala pa kazi na hivyo kuepuka kuwepo kwa malalamiko na migogoro isiyo ya lazima ili kujenga nguvu kazi shindani na Maisha bora kwa watanzania wote.