December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Fides (T) Limited inayozalisha vikonyo vya maua na kusafirisha nje ya nchi, Bas Van Lankveld akimpa maelezo ya namna wanavyozalisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo,Gerald Kusaya wa pili kutoka kushoto. (Picha na Mashaka Muhando).

Serikali yadhamiria kuwapa utajiri wakulima wa mbogamboga, matunda

Na Mashaka Mhando, Arusha

SERIKALI imesema mchakato wa kuandaa mpango mpya wa Kilimo cha Horticulture utalenga kuondoa changamoto zinazokabili kilimo hicho hapa nchini ili kuongeza mnyororo wa thamani ikiwemo vikwazo katika usafirishaji wa mazao hayo nje ya nchi.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya amesema hayo alipotembelea Asasi ya Kilimo cha Bustani, Mbogamboga, mizizi, matunda na maua (TAHA) mjini hapa na kuelezwa changamoto mbalimbali zinazowakabili.

Katibu Mkuu amesema kuwa, mpango huo utaenda sambamba na kuanzishwa kwa sheria mpya ya afya ya mimea ambayo itasaidia kupima viwango vya mazao kabla ya kusafirishwa nje ya nchi ili kuinua ubora wa mazao hayo.

Amesema, mpango huu utaondoa changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya kilimo hasa kilimo hicho cha bustani, mbogamboga na matunda na kwamba utawasaidia wakulima wadogo na wakubwa kulima wakiwa na masoko shambani.

Amesema, mpango huo utatazama mazao yanayohitajika katika soko na kutengeneza mazingira yatakayowezesha wakulima kusafirisha mazao yao katika masoko mbalimbali duniani.

“Mpango wa sasa unaosimamia mazao ya Horticulture unaisha mwaka 2021, tupo katika mchakato wa kuandaa mpango mpya ambao huu utajikita zaidi kwenye kuondoa changamoto,”amesema Kusaya.

Katibu mkuu alifurahishwa na kazi zinazofanywa na taasisi hiyo ya TAHA na akawahidi kwamba Serikali itashirikiana nayo bega kwa bega ili waweze kufikia malengo yao ikiwemo suala la masoko.

Awali Mkurugenzi Mtendaji wa TAHA, Dkt.Jaqueline Mkindi amesema, taasisi hiyo kwa sasa inakua kwa kasi hadi kusafirisha nje mazao ya Horticulture yenye thamani ya Dola za kimarekani milioni 760 kwa mwaka.

Amesema, kila mwaka wamekuwa wakiongeza uzalishaji wa mazao hayo ambapo wamelenga kusafirisha mazao yenye thamani ya Shilingi Bilioni 3 kwa mwaka.

“Nchi yetu ina maeneo mazuri yenye kustawi mazao hayo hivyo ‘target’ yao kubwa ni kusafirisha mazao yenye thamani ya shilingi bilioni 3 kwa mwaka, “amesema Dkt.Mkindi.

Akielezea changamoto wanazokutana nazo, Dkt.Mkindi amesema, wamekuwa wakiingia gharama za usafirishaji kwa kutumia viwanja vya ndege vilivyopo nchi jirani pamoja na bahari.

“Kama nchi mheshimiwa Katibu Mkuu, eneo la usafirishaji tuje na mkakati wa kupandisha mazao yetu kwenye soko, ili ndege ziweze kuja nchini badala ya kuzifuata nchi jirani, ” amesema Dkt.Mkindi.

Ametaja changamoto nyingine kuwa ni tozo wanazotozwa na mamlaka mbalimbali zinazokadiriwa kufikia kumi na tano jambo linalowapa usumbufu.

“Kuna makampuni makubwa yalikuja hapa nchini yakawekeza katika kilimo hiki, lakini baada ya miaka miwili wakafunga wakaondoka, “amesema na kuongeza kwamba kuna kampuni 11 zimefungwa hazifanyi kazi licha ya kuajiri zaidi ya Watanzania 300.

Mkurugenzi huyo wa TAHA ameomba Serikali kuzifufua kampuni hizo ili ziweze kuleta ajira na ushindani katika uzalishaji wa mazao hayo ya horticulture hapa nchini.

Katibu mkuu ambaye alifika TAHA kujifunza na kuona uzalishaji baada ya kutembelea kituo cha kuzalisha Mbegu kilichopo Njiro na kisha baadae alitembelea taasisi ya kuzalisha mbegu za maua ya Fides (T) Limited inayoongoza na Bas Van Lankveld.