May 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yadai haihusiki bomoa bomoa vibanda vya Wafanyabiashara Kivule

Na Heri Shaban, Timesmajira Online, Ilala

Mkuu wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo amesema zoezi lililofanyika Kata ya Kivule ya bomoa bomoa vibanda vya biashara Serikali haihusiki na kitendo kilichofanyika.

Mpogolo amesema hayo wakati wa ziara yake Kata ya Kivule kwenda kuwapa pole wafanyabishara na wamachinga zaidi ya 37 waliovunjiwa vibanda vyao na kundi la wahuni .

“Bomoabomoa ya vibanda vya biashara Kivule ni kitendo kilichofanyika cha kihuni Jeshi la Polisi Wilaya ya Ilala alijatuma askari wake ,Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ajatuma Askari Mgambo wake wala Mbunge wa Ukonga Jery Silaa viongozi wote wa Serikali wametoa pole kwa jambo hilo,”amesema Mpogolo.

Ampongeza Diwani wa Kata ya Kivule Nyasika Getama, kwa taarifa za haraka ambazo amewasilisha wilayani ambapo ameeleza kuwa kuna kundi limemzunguka Diwani huyo na kufanya vitendo vya kihuni.

Aidha Mpogolo amesema kutokana na tukio hilo Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ilala imeunda tume ya kufanya uchunguzi waliohusika wakibainika watakamtwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria

Katika hatua nyingine Mkuu wa wilaya Mpogolo amesema eneo lililotengwa kwa ajili ya soko la Kivule sio rafiki na mkataba wake ni wa kitapeli ambapo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Jomary Mrisho Satura na wataalam wake watakuja kuupitia upya mkataba huo na Serikali itatoa fedha kwa ajili ya ukarabati soko hilo ili liweze kutumika hivyo wafanyabishara waendelee kufanya biashara katika maeneo yao ya awali.

Ameshangazwa na viongozi wa serikali kutumika vibaya ambapo amesema viongozi wa namna hiyo wanamtia mashaka katika uongozi kwani kiongozi bora anajali shida na matatizo ya wananchi.

Diwani wa Kata ya Kivule Nyasika Getama amesema katika tukio hilo umefanyika unyama mkubwa wananchi wake wameibiwa vitu mbali mbali ikiwemo mali na fedha.

Huku akieleza kuwa wakati zoezi la bomoabomoa ya vibanda vya biashara likifanyika inadaiwa kuwa magari ya Serikali yalitumika ambapo pia kundi hilo limedai litarejea tena kuwabomolea .

Amesema Jumamosi November 7 mwaka huu kuamkia Jumapili November 8 vibanda 37 vilibomolewa vya wafanyabishara wa Kivule ambao wanajitafutia mahitaji yao ya kila siku .

Kaimu Mwenyekiti wa wafanyabishara Kivule Yusuph Salehe amesema idadi ya wafanyabishara wa eneo hilo ni 37 vibanda vilivyovunjwa ni 24 na kudaiwa kuiba vitu vya thamani ikiwemo fedha taslimu katika maduka ya kubadirisha fedha, feni,kompyuta na vitu mbalimbali.

Salehe amesema kwa sasa mara baada kutokea hasara hiyo wamekosa mitaji ya biashara na wengine wapo katika mikopo ya marejesho maisha yamekuwa magumu .