Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Dar es Salaam
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameiagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kushirikiana na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kuendelea kufunga mtandao katika vijiji vyenye umeme ili kuwawezesha wanafunzi kufanya mitihani ya masomo ya sayansi kwa mtandao.
Rais Samia ametoa maagizo hayo leo wakati wa hafla ya kilele cha Maadhimisho ya Miaka 50 ya Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) iliyofanyika katika Ofisi za Baraza hilo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu serikali imefanya uwekezaji katika TEHAMA ambao umeimarisha utendaji wa Baraza na kuongeza matumizi ya teknolojia katika usajili wa watahiniwa, uchapaji na usahihishaji wa mitihani na uchakataji wa matokeo.
Taarifa hiyo ilimkariri Rais Samia akisema ‘Serikali itaendelea kuijengea uwezo NECTA na walimu ili kuhakikisha ufundishaji, usomeshaji na utahini unafanyika kwa umahiri mkubwa kuwawezesha watahiniwa kumudu mahitaji ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia.’
Aidha, Rais Samia ameitaka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na NECTA kutafuta mkakati wa kushughulikia changamoto ya udanganyifu wa mitihani.
Aidha, Rais Samia pia amelitaka Baraza la Mitihani kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kuendana na shabaha ya sera ya elimu hususan katika upimaji wa umahiri.
Rais Samia amesema serikali itaendelea kuimarisha utendaji wa Baraza kulingana na mazingira mapya ya kiteknolojia na kushirikiana na Baraza hilo ili lifikie malengo ya muda mrefu ya kuweka mitambo ya kisasa ya uchapaji kadri uwezo utakavyoruhusu.
More Stories
LALJI yatoa msaada wa sare na vifaa vya shule kwa yatima
Dkt.Biteko aagiza Kituo cha huduma kwa wateja Tanesco kusukwa upya
Rais Samia aridhishwa na uongozi safi wa Mwinyi