May 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali kuwamulika watendaji wala rushwa ndani ya CCM

Na Jackline Martin, TimesMajira Online, Mwanza

KATIBU wa NEC,Itikadi na uenezi wa Chama cha Mapinduzi(CCM)Paul Makonda amesema serikali itaendelea kuwamulika watendaji walio ndani ya Chama Cha Mapinduzi ambao ni wazembe, wala rushwa na si waaminifu kwa Mali za umma ili pesa ya mwananchi anayelipa kodi na pesa ya Rais Samia anayoitoa kwaajili ya maendeleo iwaletee tija wananchi wa kawaida.

Makonda ameyasema hayo Jana wakati akizungumza na wananchi wa Kisesa, Wilaya ya Magu Mkoa wa Mwanza ikiwa ni muendelezo wa ziara yake katika mikoa ya Kanda ya ziwa ambapo alisema Rais Samia amewakabidhi Chama kukisemea mema ya Chama hicho.

“Wapo watu wazembe, Wala rushwa, ni jukumu letu kama Chama kuendelea kuimulika serikali na kuisimamia kikamilifu ili pesa ya mwananchi anayelipa kodi na pesa ya kiongozi wetu anayoitoa kwaajili ya maendeleo iwaletee tija wananchi wa kawaida”

“Kuna watu hata kwenye familia wapo, ukiwapa pesa siyo waaminifu, hata kwenye mahusiano watu wapo, wanaahidi mambo kwa wapenzi wao hawafanyi, Sasa kama kwenye familia au kwenye mahusiano siyo waaminifu na watekeleza ahadi zao inawezekana pia hata ndani ya serikali tukawa na watendaji si waaminifu kwa Mali za umma, hao Chama kitaendelea kuwamulika”alisema Makonda.

Makonda amesema kiapo Cha Chama Cha Mapinduzi na msingi wake ni binadamu wote sawa hivyo wanataka uadilifu uliotukuka ikiwemo utoaji wa huduma stahiki kwa wananchi.

“Tunataka uadilifu uliotukuta, ukienda hospitali uhudumiwe kikamilifu, ukienda Manispaa/ Halmashauri uhudumiwe kikamilifu, usihudumiwe kwasababu umesoma au una pesa, au una ndugu kiongozi,bali uhudumiwe kwasababu wewe ni Binadamu, na kiapo chetu kina sema Binadamu wote ni sawa na huo ndiyo msingi wa Chama Cha Mapinduzi”

Pia amesema Chama kimekubali kubadilika kulingana na mazingira na mahitaji ya wakati husika na kupelekea kuwepo kwa maendeleo endelevu kwa wananchi.

“Faraja niliyonayo kwenye Chama hiki ndiyo Chama pekee chenye uwezo wa kuwa na sifa 3 ambazo hazipatikani kwenye Chama kingine, hiki ni Chama kinachokubali kukosolewa, ni Chama kinachokubali kujirekebisha na Chama kinachokubali kubadilika kulingana na mazingira na mahitaji ya wakati husika,

“Hapa hakukuwa na barabara ya lami inayotuunganisha kwenda usagala, hata round about iliyopo hatukuwa nayo, ujenzi wa Reli ya SGR hatukuwa nayo, Chama kimekubali kubadilika kutokana na mazingira na mahitaji ya watanzania”

“Hizi shule ambazo Rais wetu ameleta pesa kwasababu ya ongezeko la watu shule Moja haitoshi na madawati hayatoshi, serikali yetu ikakubali kubadilika kulingana na mahitaji ya wakati tukaletewa pesa tukajenga madarasa na watoto wetu wanaenda shule,”amesema Makonda.

Kuhusu Kadi mpya za Chama za Kielektroniki kwa wananchi, Makonda amesema kutokana na agizo la Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo Chama kinaendelea kushughulikia Kadi hizo ambapo hadi ifikapo mwezi Februari mwakani Chama kitaanza kutoa Kadi hizo.

“Hapa tulipo wote inawezekana tukawa tunajiuliza hivi Chama hiki kitaendelea kutoa Kadi za zamani au Kadi mpya? Katibu wetu Mkuu Komredi Chongolo ametoa maelekezo ifikapo mwezi wa pili mwaka 2024 Chama kianze kuwapatia wanachama Kadi mpya za kielektroniki,”amesema.

Makonda amewataka wanakisesa kuyapokea mawazo ya vyama vingine na kuwashirikisha Chama Cha Mapinduzi CCM ili yafanyiwe kazi.

“Wengine ambao mnapenda vile vyama vya watoa taarifa watakavyokuja kwenu na taarifa pokeeni, lakini mnisaidie kuwauliza hiyo taarifa ni ya ukweli au ya uwongo? wakisema ya ukweli mwambie tunaiomba tutampeleka mwenezi Makonda atupatie majibu na kama ni ya ukweli tutaifanyia kazi,

“Yawezekana wakawa na mawazo mazuri nduguzetu wa vyama vya watoa taarifa, nduguzangu wakiwa mbowe, Tundulisu n.k, tukayapokea mawazo yao kwakuwa tunae Rais Samia, Mwenyekiti wa Chama aliyesema anataka nchi iwe na umoja na kila mtu anahaki sawa, ndiyo maana aliruhusu mikutano ya hadhara, changamoto tu waliyoipata ndugu zangu wameishiwa mafuta ya hedikopta na mimi nimewaombea kwa Rais awape mafuta ili waendelee na mikutano ya hadhara,”amesema.