November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali kuimarisha matumizi ya Nishati safi ya kupikia

-Majiko banifu kusambazwa Kaya za Vijiji na Vijiji-Miji

-Wazalishaji wa mkaa mbadala kupewa ruzuku

Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko amesema kuwa katika mwaka 2024/25 Serikali itaendelea kutekeleza hatua madhubuti za kuimarisha matumizi ya Nishati Safi ya kupikia nchini.

Dkt Biteko ameyasema hayo leo Aprili 24, 2024 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka 2024/25

“Serikali kwa kushirikiana na wadau itaendelea kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia wa mwaka 2024 – 2034 kwa kupatia ufumbuzi vikwazo vya matumizi ya nishati hiyo, ikiwemo gharama kubwa, upatikanaji hafifu na uhaba wa miundombinu yake na kukosekana kwa elimu ya kutosha kuhusu madhara ya nishati zisizo safi na salama za kupikia”, amesema Dkt. Biteko.

Ameongeza “Wizara itaendelea kusimamia na kuratibu utekelezaji wa Programu ya Nishati Safi ya Kupikia inayolenga Kuwawezesha Wanawake Barani Afrika Kutumia Nishati Safi ya Kupikia”.

Pia, Dkt. Biteko amebainisha kuwa Serikali pia itaendelea na utekelezaji wa mradi wa kusambaza majiko banifu kwenye kaya zilizopo katika maeneo ya vijijini na vijiji-miji, kutoa ruzuku kwa wazalishaji wa mkaa mbadala kwa ajili ya ununuzi wa mashine zitakazotumika katika uzalishaji wa mkaa huo, kuendelea kushirikiana na Jeshi la Magereza katika ujenzi wa miundombinu ya nishati ya kupkia katika maeneo 211 pamoja na kuendelea na usambazaji wa gesi asilia majumbani, hususan katika Mikoa ya Dar es Salaam, Mtwara, Lindi na Pwani.

Wizara ya Nishati imewasilisha maombi ya shilingi 1,883,759,455,000 kwa ajili ya matumizi ya Wizara hiyo na Taasisi zake.