January 8, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali kuendeleza bunifu ziingie sokoni kukuza uchumi,ajira kwa vijana

Na Joyce Kasiki,Timesmajiraonline,Dodoma

SERIKALI imesema,maonyesho ya Kitaifa ya Sayansi ,Teknlojia na Ubunifu (MAKISATU) ya mwaka huu,yameibua wabunifu wapatao 2,785 huku ikidendelea kuwaendeleza wabunifu wapatao 200 walioibuliwa katika mashindano ya miaka iliyopita kwa lengo la kuhakikisha bunifu zao zinaingia sokoni.

Akizungumza katika uwanja wa Jamhuri jijini hapa wakati wa uzinduzi wa maonyesho hayo yaliyoandaliwa na Wizara ya Elimu ,Sayansi na Teknolojia,Makamu wa kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Othman Masoud Othman amesema kuwa Serikali  zote mbili zimezimia kujenga uwezo wa ndani kwa kuendelea kuwekeza katika rasilimali watu,miundombinu na vifaa vya kisasa vya utafiti na ubunifu na kuimarisha mahusiano kati ya taasisi za sayansi na teknolojia na pia sekta ya viwanda.

“Matunda na jitihada za serikali katika utekelezaji wa malengo hayo na hatua zinazochukuliwa yote yanabainika kupitia mashindano ya Kitaifa ya Sayansi,Teknlojia na Ubunifu ambapo Jumla ya wabunifu wachanga 2,785 wameweza kuibuliwa mwaka huu,

“Miongoni mwao walio mahiri zaidi wapatao 200 wanaendelezwa na serikali lengo ni kuwa bunifu na teknlojia zao walizozalisha zifikie hatua ya kupelekwa sokoni na kutumika na hivyo kuongeza fursa za ajira kwa vijana na kuchangia pato la Taifa”amesema Othman

Aidha amesema,maonyesho ya Wiki ya Ubunifu (MAKISATU) Kitaifa na mashindano  ya mwaka huu bado yanakwenda kuibua zaidi bunifu na teknolojia zitakazo kwenda kujibu na kuleta ufumbuzi wa changamoto za kiuchumi katika jamii na Taifa kwa ujumla.

Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda

Kwa mujibu wa kiongozi huyo,Serikali itaendelea kujenga mazingira na kutoa fursa ya  kuibua wabunifu zaidi na kuwaendeleza kwa lengo la kuchochea kasi ya maendeleo na kuimarisha maendeleo ya uchumi na ustawi wa jamii.

Amesema,Serikali inatambua umuhimu wa wiki hii na ndio maana maonesho haya yanafanyika ili kuendelea kuibua na kukuza vipaji tunapaswa kufanya maonesho naamini itatusaidia kuongeza kasi ya maendeleo kwa taifa.

Kwa upande wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  amesema,nayo inachukua hatua mbalimbali kwa lengo la kuhamasisha ubunifu na teknlojia ili kuongeza ubora wa bidhaa zinazozalishwa na wabunifu.