May 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali kuendelea kusambaza majiko banifu

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online. Dar

SERIKALI imesema itaendelea na utekelezaji wa mradi wa kusambaza majiko banifu kwenye kaya zilizopo katika maeneo ya vijijini na vijiji-miji na kutoa ruzuku kwa wazalishaji wa mkaa mbadala kwa ajili ya ununuzi wa mashine zitakazotumika katika uzalishaji wa mkaa huo.

Hayo yamesemwa leo Aprili 24,2024 na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt.Doto Biteko bungeni jijini Dodoma wakati akisoma hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025.

“Tutaendelea kushirikiana na Jeshi la Magereza katika ujenzi wa Miundombinu ya nishati ya kupikia katika maeneo 211 pamoja na kuendelea na usambazaji wa gesi asilia majumbani hususani katika mikoa ya Dar es salaam,Mtwara,Lindi na Pwani”amesema Dkt.Biteko

Pia amesema, uzalishaji wa umeme kupitia mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maji wa Julius Nyerere (JNHPP) wenye uwezo wa kuzalisha Megawati 2,115, ambapo uzalishaji huo umeanza kwa Megawati 235 kupitia mtambo namba tisa.

Aidha amesema, Mwaka 2024/25, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) itaendelea kuchukua hatua za kupeleka nishati vijijini ili kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi na maendeleo ya kijamii katika maeneo hayo.

Pia ameeleza kuwa, miradi iliyopangwa kutekelezwa ni pamoja mradi wa kupeleka umeme katika Vitongoji 20,000 ambapo kazi zitakazofanyika ni pamoja na ununuzi wa wakandarasi wa kutekeleza mradi, kufanya usanifu wa kina wa mradi na kuanza ujenzi wa miundombinu ya mradi.

Waziri Biteko amesema, Serikali itaendelea na utekelezaji wa mradi wa kupeleka umeme katika vitongoji katika Mkoa wa Songwe na Kigoma kwa kukamilisha ujenzi wa miundombinu ya kusambaza umeme Msongo Mdogo, kufunga transfoma na kuunganisha wateja. Vilevile, Serikali itaendelea kutekeleza mradi wa kupeleka umeme katika Vitongoji 3,060 (vitongoji 15 kila Jimbo) kwa kujenga miundombinu ya mradi, kufunga transfoma na kuunganisha wateja.

Hata hivyo, miradi mingine itakayotekelezwa ni mradi wa ujazilizi Awamu ya Pili B; mradi wa Ujazilizi Awamu ya Pili C; mradi wa kupeleka umeme katika maeneo ya Vijijini-Miji; mradi wa kusambaza umeme katika Migodi Midogo, maeneo ya Kilimo na Viwanda; mradi wa kupeleka umeme katika minara ya mawasiliano ya simu na mradi wa ufungaji wa mifumo ya umeme jua kwenye makazi yaliyopo Visiwani na yaliyopo mbali na Gridi ya Taifa.