May 1, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali imetakiwa kutoa adhabu kali kwa watu wanaooa au kuhusika kuozesha wasichana wa umri mdogo

Na Penina Malundo, TimesMajira, Online

WASICHANA mbalimbali nchini wameungana na kutoa tamko la pamoja katika kusherekea siku ya mtoto wa kike duniani huku wakiitaka Serikali kutoa  adhabu kali kwa watu wanaooa na kuhusika kuozesha wasichana katika umri mdogo na kutilia mkazo mabadiliko ya sheria ya ndoa inayomkandamiza mtoto wa kike ya mwaka 1971.

Tamko hilo lililotolewa jana jijini Dar es Salaam na wasichana hao na kusomwa na Mwanafunzi kutoka Mkoa wa Dar es Salaam, Neema Bernard wakati wa mkutano wa ajenda ya Msichana iliyoandaliwa na Taasisi ya Tai Tanzania, C-Sema,Flaviana Matata Foundation, Msichana Initiative  na Girl Effect.

Bernard  amesema Serikali ikiweka mikazo mbalimbali itaweza kusaidia kutoa fundisho kwa wengine ili vitendo hivi visiendelee  kwa jamii yetu.”Serikali itilie mkazo mabadiliko ya sheria ya ndoa inayomkandamixa mtoto wa kikena kufanya umri wa kuolewa kwa wasichana na wavulana uwe miaka 18 na kuendelea,”amesema 

Amesema  pia serikali iondoe kodi katika bidhaa za pedi ili kuweza kurahisisha wasichana waweze kumudu kutumia bidhaa hizi kwani wasichana wanalalamika kodi ikitolewa kwenye pedi mabinti wengi wanaweza kukaa na kusoma huru .
Amesema serikali ikifanya hivyo itasaidia kwa kiasi kikubwa wasichana kuweza kujistiri kwa urahisi na kupata pedi kwa bei rahisi zaidi. “Serikali iangalie namna ya kugawa pedi kwa wasichana wote kwani wasichana wengi wanashindwa kumudu bei na kutumia vifaa ambavyo sio salama kwa afya zao  hivyo tunaomba Serikali itilie mkazo suala la pedi hasa kwa wasichana wa vijijini waweze kupata kwa urahisi,”amesema 

Kwa Upande wake Mwanafunzi kutoka mkoa wa Dodoma Martha Mwagusila amesema taulo za kike ni bidhaa muhimu kwa wasichana ili kuweza kujistiri au kujihifadhi kipindi cha hedhi kila mwezi lazima binti ahitaji taulo hizo.
Amesema  kutokana na bei kubwa ya bidhaa hizi wasichana wengi wanashindwa kununua pesi badala yake kutumia njia mbadala na kutumia vifaa ambavyo sio salama kwa afya.”wasichana wengine wanakosa siku 3 hadi 5 za masomo darasani   kutokana na kukosa bidhaa hii hususani wale wanaoishi vijijini,”amesema 
Amesema pia ndoa ya utotoni ni tatatizo kubwa nchini Tanzania  na inasababisha wasichana wengi kutotimiza ndoto zao hasa za kielimu.”Ndoa hizi usababishwa mara nyingi na hali ya duni za kimaisha Mila na desturi potofu,ukeketaji,ukosekanaji wa elimu juu ya madhara ya ndoa za utotoni pamoja na mwanya wa sheria za ndoa mwaka 1971 inayomlazimisha mtoto wa kike kuolewa kwa umri mdogo,”amesema 

Naye Mwanafunzi kutoka mkoa wa Tabora ,Loveless Athumani amesema maadhimisho haya ya siku ya mtoto wa kike duniani uadhimishwa kila Oktoba 10 ya kila mwaka na nchini Tanzania maadhimisho haya  yanatimiza miaka 10 tangu kuanza kwake mwaka  2012.

Amesema  ili kusherekea mafanikio ya wasichana taasisi hizo zimeungana  kuleta pamoja sauti za wasichana kuhusu changamoto mbalimbali zinazowakabili na kutafuta suluhisho.” Wasichana walifanya shughuli mbalimbali katika maeneo ya Dodoma, Tabora,Iringa ,Lindi ,Shinyanga na Visiwani Zanzibar ili kuwafikia wasichana na jamii ili kutoa elimu zinazowakabili ili kuletewa ufumbuzi “amesisitiza