Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online ,Dodoma
KATIKA kipindi cha miaka minne ya mafanikio makubwa (2021–2024), Mfuko wa SELF umeweza kufikia wananchi kwa kiwango kikubwa kupitia utoaji wa mikopo nafuu, elimu ya fedha, na huduma za bima.
Kwa mujibu wa Meneja wa Rasilimali Watu na Utawala wa SELF, Johari Hassan, zaidi ya wateja 127,000 wamefikiwa, huku mikopo 9,853 yenye thamani ya takribani shilingi bilioni 162.3 ikitolewa kwa makundi mbalimbali ya wananchi kote nchini.
Sambamba na mikopo hiyo, mfuko pia umehudumia wateja wa bima 7,442, kupitia huduma zinazojumuisha bima ya magari, nyumba, wizi na nyinginezo zinazopatikana ndani ya nchi.
Hassan amesema hayo wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha yaliyofanyika katika Viwanja vya Chinangali, Dodoma, ambapo SELF ni miongoni mwa taasisi zilizoshiriki ili kutoa elimu na huduma kwa wananchi kuhusu fursa mbalimbali zinazopatikana kupitia mfuko huo.
Ametumia nafasi hiyo kuwaasa wananchi wote kutembelea banda la SELF katika Viwanja vya Chinangali kujifunza kuhusu huduma zinazotolewa, kushiriki mafunzo ya fedha, na kujiandikisha kwa ajili ya mikopo au bima.
“Tunawakaribisha wananchi wote. Fursa ipo kwa kila Mtanzania kuanzia mkulima mdogo, mama lishe hadi mfanyabiashara wa kati. Lengo letu ni kumwinua mwananchi mmoja mmoja ili Taifa nalo linufike kiuchumi,” ameongeza Bi. Hassan.
Historia na Maono ya Mfuko wa SELF
Kwa mujibu wa Hassan,Mfuko wa SELF ulianza rasmi mwaka 2014 ukiwa na lengo kuu la kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia utoaji wa mikopo nafuu kwa watu binafsi, vikundi na taasisi.
Amesema,mikopo inayotolewa inawagusa watumishi wa umma, wajasiriamali wadogo na wa kati, wafanyabiashara, wazabuni, wakulima, pamoja na wale wanaojishughulisha na nishati safi.
Aidha amesema,SELF imekuwa mstari wa mbele katika kutoa elimu ya fedha, ambayo hutolewa kwa kila mteja anayeomba mkopo. Elimu hiyo inalenga kumjengea mteja uelewa kuhusu matumizi sahihi ya fedha na mbinu bora za kurejesha mkopo kwa wakati.
Upatikanaji wa Huduma na Matawi
Amesema,SELF ina matawi 12 na vituo viwili vilivyosambaa katika mikoa mbalimbali ikiwemo Dar es Salaam, Tanga, Morogoro, Mtwara, Dodoma, Kahama, Geita, Mwanza, Iringa, Mbeya, na Arusha. Licha ya idadi hiyo ya matawi, huduma za SELF zinapatikana nchi nzima, hata katika maeneo ambayo hayana tawi rasmi, kwa kupitia timu zinazotembelea wananchi moja kwa moja.
Kuwezesha Kilimo na Ushirikiano na Benki ya Kilimo
Kwa upande wake, Meneja wa SELF Kanda ya Kati, Aristid Tesha, amesema mfuko pia unatoa mikopo kwa wakulima mmoja mmoja na asasi za kifedha kama vyama vya ushirika, hasa zile zinazojihusisha na shughuli za kilimo.
Aidha amesema,changamoto ya kupata dhamana imekuwa ikitatuliwa kupitia ushirikiano wa SELF na Benki ya Kilimo, ambapo wakulima wanaosaidiwa kupata dhamana ili waweze kufanikisha maombi ya mikopo yao.
“Hii inawasaidia wakulima na taasisi zao kujiendeleza kwa shughuli endelevu na hatimaye kuchangia uchumi wa mtu mmoja mmoja pamoja na Taifa kwa ujumla,” amesema Tesha.
Mikopo kwa Wajasiriamali na Nishati Safi
Tesha amesema,SELF imepanua wigo wake kwa kuanzisha bidhaa mpya ya mikopo kwa wajasiriamali wanaojihusisha na biashara za nishati safi, kama vile wauzaji wa gesi na vifaa vyake, pamoja na vifaa vya umeme vinavyotumia nishati mbadala kama umeme jua.
Lengo kuu la mpango huu ni kusaidia juhudi za serikali za kupunguza matumizi ya nishati chafu kama kuni na mkaa, hivyo kuboresha mazingira na afya ya wananchi.
“Kwa sasa, SELF inalenga kuendelea kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa wananchi wote wenye sifa na vigezo, bila kujali eneo au hali zao za kijamii, ilimradi shughuli zao za kiuchumi ziwe halali na endelevu.”amesema Tesha

More Stories
Silinde azindua baraza la sita la Wafanyakazi Tume ya Taifa ya Umwagiliaji
NMB ilivyosaidia Serikali kukusanya zaidi ya Sh trilioni 9.8
Serikali yaongeza nguvu kwa wachimbaji wadogo,yasisitiza usalama Migodini