August 11, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Airtel yatoa elimu ya Usalama dhidi ya Matapeli wa Mtandao

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

Kampuni ya mawasiliano ya Airtel Tanzania imeshiriki kikamilifu katika Maonesho ya Wakulima ya Nane Nane katika mikoa ya Dodoma, Morogoro, Arusha, Mbeya, Rukwa, Mwanza na Tabora, ambapo imetumia jukwaa hilo kutoa elimu kwa wananchi kuhusu usalama dhidi ya utapeli wa mtandao, sambamba na kusogeza huduma zake za kidijitali karibu na wateja.


Kupitia maonesho hayo, Airtel imeendelea na kampeni ya “Minyoosho Inaendelea”, inayolenga kuwahamasisha wateja kutumia huduma za kidijitali kufanya miamala kupitia My Airtel App, pamoja na kutumia huduma mbalimbali za Airtel Money kwa urahisi, haraka na kwa usalama zaidi.

Akizungumza katika Maonesho ya Nane Nane, Meneja wa Biashara wa Airtel Mkoa wa Dodoma, Bw. Salum Juma Ngululu, amesema ushiriki wa Airtel katika maonesho hayo ni sehemu ya dhamira ya kampuni ya kuwa karibu na wateja, kuwaelimisha kuhusu matumizi salama ya huduma za kidijitali na kuhakikisha wanaendelea kunufaika na fursa zinazotokana na teknolojia.


Ngululu amesema elimu kuhusu usalama wa mtandao ni muhimu kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya huduma za kidijitali na miamala ya kifedha kupitia simu, hivyo wateja wanapaswa kuwa makini na watu wanaoweza kujaribu kutumia njia mbalimbali za mawasiliano kwa lengo la kuwaibia au kupata taarifa zao za siri.


Amesema wateja wanapaswa kulinda taarifa zao binafsi na za kifedha, hususan PIN ya Airtel Money, OTP, nenosiri na taarifa nyingine za siri na kutokumkabidhi mtu mwingine taarifa hizo kwa kisingizio cha kuwasaidia kupata huduma au zawadi.


“Tunawahimiza wateja kuwa makini wanapopokea simu, ujumbe au mawasiliano kutoka kwa watu wasiofahamika wanaodai kuwa wawakilishi wa Airtel. Mteja hapaswi kutoa taarifa zake za siri, na anapaswa kutumia njia rasmi za Airtel anapokuwa na mashaka au anapohitaji msaada kuhusu huduma zake,” amesema Ngululu.


Akizungumzia kampeni ya “Minyoosho Inaendelea”, Ngululu amesema kampeni hiyo inalenga kuongeza matumizi ya huduma za kidijitali kwa kuwahamasisha wateja kutumia My Airtel App kufanya miamala yao ya kila siku ya Airtel Money kwa njia rahisi na salama.


Kupitia kampeni hiyo, wateja wanaotumia My Airtel App kufanya miamala inayokidhi vigezo wanapata fursa ya kushiriki katika mchezo wa Spin & Win na kujishindia zawadi, hivyo kuhamasisha matumizi zaidi ya huduma za kidijitali.


Ngululu amesema kampeni hiyo inaendana na dira ya Airtel ya “Kila Kona”, inayolenga kuhakikisha huduma za mawasiliano na kidijitali zinawafikia Watanzania katika maeneo mbalimbali nchini na kuwawezesha kutumia teknolojia kurahisisha shughuli zao za kila siku.


Ameongeza kuwa ushiriki wa Airtel katika Maonesho ya Nane Nane unalenga pia kusogeza huduma karibu na wananchi, kutoa elimu kuhusu bidhaa na huduma mbalimbali za kampuni, pamoja na kuwapa wateja fursa ya kupata huduma moja kwa moja katika mabanda ya Airtel.