May 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Sauti ya mwalimu Nyerere na miaka 59 ya Uhuru wa Tanganyika

Na Judith Mhina,TimesMajira Online-MAELEZO

HISTORIA imeandikwa na itaendelea kuandikwa, kwa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Waziri Mkuu wa kwanza wa Jamhuri ya Tanganyika na baadaye Rais wa Jamhuri ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sauti yake kamwe haiwezi kuzimwa wala kuchosha Watanzania itaendelea kusikika ndani na nje ya nchi.

Hakika imetimia miaka 59 ya uhuru wa Tanganyika ambapo wewe Baba wa Taifa umeweka misingi imara ya Utaifa na Umoja ambao dunia inashangaa uliwezaje, umefanyaje, kuunganisha makabila zaidi ya 126 yaliyopo mashariki, magharibi, kusini, kati na kaskazini mwa Tanzania na kuwafanya kuwa wamoja na kuwashangaa wale wote wanaoshabikia ukabila.

Mwalimu Nyerere kauli yako ya kwanza kuhusu Afrika kwamba nanukuu “Uhuru wa Tanzania hautakuwa na maana kama nchi nyingine za Afrika zitaendelea kutawaliwa”

Kila uchweo maandiko yako na sauti yako inasikika katika pande zote za Tanzania kuanzia kwenye magazeti, redio, televisheni, nyimbo, ngonjera, mashairi na ngoma za asili. Hii ikiwa ni pamoja na nyimbo za muziki wa dansi, muziki wa kizazi kipya, kwaya, michezo ya watoto halaiki na hafla mbali mbali za kitaifa na mataifa.

Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere misingi yako uliyoiweka inasikika ndani ya sauti yako ambayo bado inatoa ulinzi na usalama kutoka Beirut Lebanon, ambapo Jeshi la Wananchi wa Tanzania-JWTZ linalinda amani, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Afrika ya Kati na Darfu Sudan Sudan Kusini) ikiwa ni sehemu ya matunda yako ya nchi wanachama Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika-SADC ambao wapo mstari wa mbele kutokana na misingi uliyoiweka.

Sauti yako inasikika katika hotuba zako maarufu ulizowahi kuhutubia na kuongea ndani na nje ya nchi matamshi yenye hisia kali yakitamkwa kwa unyenyekevu na upendo kwa Watanzania. Sauti yako inaelimisha, inahamasisha, ikitoa taarifa, ikionya, kuasa na kupongeza kwa mambo mbalimbali yaliyotokea katika Jamii yetu, nje ya nchi na kwa watu mashuhuri hapa Tanzania na duniani kwa ujumla.

Mwalimu usiku wa kuamkia Desemba 9, 1961 ni siku ya kukumbukwa na Watanzania wote kwa kuwa wahenga walisema, ilikuwa kama ndoto ambayo ilitokea kweli. Tanganyika kuwa huru na kujitoa katika makucha ya wakoloni bila kumwaga damu ilikuwa ni kielelezo tosha kama ulivyo toa hotuba yako fupi iliyokuwa na matumaini lukuki kwa Watanganyika ya Uhuru na Umoja.

Aidha, hotuba zako za mwanzo kama Waziri Mkuu wa Tanganyika Mwalimu Nyerere ulionekana pale Mnazi Mmoja ukielezea juu ya Katiba tarehe 31, Mei, 1962 na sherehe za ufunguzi wa chemchem ya maji ya mnazi mmoja Dar-es-salaam na tarehe 08 Desemba 1962.

Nimekariri na kutafakari baadhi ya hotuba zako kama zile za kisiasa na historia za kuapishwa kuwa Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo tukio la kuchanganya udongo wa Bara na Visiwani lilifanyika Oktoba 1, 1965 pale Zanzibar bado sauti yako ilitamka maneno haya;
“Kazi ya nchi na watu wa Tanzania ni kuwaunganisha waafrika kuleta uhuru na umoja kwa waafrika wenzao” huu ni msingi uliousimamia mpaka kuhakikisha Afrika yote inakuwa huru.

Hiki kilikuwa kishindo na mashangao mpaka leo dunia imeshindwa kufahamu kwa vipi umeweza kuunganisha Tanganyika na Zanzibar, hotuba ya kwanza ya mkutano wa hadhara aliofanya pale Zanzibar Desemba 20,1964.

Uliwaeleza Watanzania kibaga ubaga kuwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar sio wa kwako na Shekhe Abeid Amani Karume bali ni wa Watanzania kwa kuwa asilia sisi tu wamoja.

Mwalimu Nyerere mnamo April Mosi,1965 akafungua mkutano wa pili tangu Tanzania iwe Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ulijikita zaidi katika kuzungumzia rushwa makazini.

Sauti yako Mwalimu imesikika pale Zanzibar, katika sherehe za miaka 10 ya Azimio la Arusha na miaka 20 ya Afro Shiraz Party-ASP na wakati wa kuzaliwa kwa chama kipya yaani Chama cha Mapinduzi – CCM huko Zanzibar tarehe 05 Februari 1977. Nakumbuka hotuba yako uliyoitoa kwa viongozi wa chama na serikali wakiwemo wazee wa Mkoa wa Dar-es-salaam pale Diamond Jubilee Desemba 9,1978.

Sauti yako Mwalimu inabakia kuwa gumzo na kuendelea kusikika kama katika hotuba yako uliyoitoa kwa wazee wa chama chako cha Tanganyika African National Union –TANU na wazee wa na Mzizima Jijini Dar es Salaam. Mwalimu ukatoa maelezo zaidi na ufafanuzi juu ya utaifishaji wa majumba katika mtaa wa Lumumba tarehe 29, Mei, 1971.

Kama hiyo haitoshi Mwalimu sauti yako bado inasikika katika hotuba uliyoitoa mwaka Mei 3, 1965 ulipofungua semina ya wakuu wa madhehebu ya dini mbalimbali nchini huko Tabora. Ambapo uliwaasa kuwa na umoja upendo na kutobaguana kwa kuona dini hii ni bora kuliko nyingine, Mwalimu ulisisitiza wote tunajenga Tanzania moja inayohitaji maendeleo.

Sauti yako bado inapenyeza katika mioyo ya Watanzania na kusikia hotuba uliyoitoa Februari mwaka 5,1967, ukiwahutubia wananchi wakati ukitanganza Azimio la Arusha, siasa ya ujamaa na kujitegemea pale Mnazi Mmoja Dar-es-salaam.

Pia, ulifanya mkutano wa hadhira ambapo Mwalimu Nyerere alihutubia wananchi wakati wa maadhimisho ya miaka 10 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar Aprili 26,1974 uliofanyika katika uwanja wa pale Amani Zanzibar.

Aidha, sauti yako inasikika katika tafrija ya wazee wa CCM waliokuita kukupongeza kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa kwanza wa CCM, katika ukumbi wa Diamond Jubelee Mei 8,1977. Hakika ulistahili pongezi kwa kuwa kazi uliyoifanya imetukuka Muungano umeshamiri na kustawi kila uchweo ni kweli unastahili pongezi za kipekee kwako binafsi na kwa Shekhe Amani Abeid Karume muasisi wa Afro Shiraz Party na CCM.

Maandamano ya wanajeshi ya kuunga mkono Azimio la Arusha, siasa ya ujamaa na kujitegemea Jijini Dar es Salaam Februari 6,1967 yalidhihirishia dunia kuwa uko katika maamuzi sahihi. Kama hiyo haitoshi imedhihirika pale misingi ya Azimio la Arusha ilipoachwa taifa likaenda mrama na mara waliposikiliza sauti yako tumetambua wapi tumekosea na kwa sasa nakuhakikishia tupo kwenye mstari sahihi kutekeleza yale uliyoyataka.

Sauti yako Mwalimu bado inasikika ulipowahutubia Watanzania siku ya mashujaa tarehe 01, Septemba, 1979 mara baada ya kumalizika kwa vita vya Tanzania na Uganda na kuipongeza Jeshi la Wananchi wa Tanzania-JWTZ kwa ushindi walioupata na kuhakikisha Uganda inajitawala katika misingi ya usawa na kuthamini utu wa mtu pale uwanja wa Taifa.

Pamoja na mambo ya siasa Mwalimu umesikika katika masuala muhimu ya Taifa na Kimataifa Mwalimu ulifungua washa ya misitu pale Mwadui Shinyanga akiwa mstari wa mbele kulinda rasilimali za misitu tulizonazo katika hotuba yako uliyoitoa tarehe 14, Septemba, 1984.

Hayo ya Kimataifa tena sio yakusema umefanya mengi mno kuanzia nchi zisizofungamana na upande wowote, Afrika, Asia, Amerika, Bara Hindi, nchi za Scandinavia, Amerika ya Kusini na Mashariki ya mbali.

Mwalimu sauti yako inasikika kimataifa pale alipohutubia mkutano wa sita wa nchi zisizofungamana na upande wowote nchini Cuba katika Jiji la Havana, Septemba 5,1979 iliyohusu masuala ya ulinzi na usalama wa Taifa huru.

Suala la Ukombozi Kusini mwa Afrika na duniani kwa ujumla hilo kwako lilikuwa ni suala linalopewa kipaumbele Mwalimu ulihutubia wakati uhuru wa Msumbiji tarehe 25 Juni 1975 katika jiji la Maputo. Pia ulikabidhiwa majengo ya chama cha ukombozi cha Msumbiji – FLERIMO kwa serikali ya Tanzania tarehe 05 Julai 1976 na kutamka yatakuwa shule, kwa kuwa elimu ni kipaumbele kwa taifa lolote ili kuleta maendeleo ya watoto wa sasa na kizazi kijacho.

Ziara Mwalimu Nyerere nchini Uingereza 1975 alihutubia mbele ya Malkia Elizabeth wa 11 ambapo, ililenga kuongelea suala la uhuru wa Zimbabwe na suala la ubaguzi wa rangi Afrika ya Kusini na utawala wa walio wengi weusi. Hivyo jinsi gani Uingereza itasaidia kuharakisha uhuru wa Zimbabwe na mlowezi kaburu wa Afrika ya Kusini kuachia madaraka kwa weusi walio wengi.

Kutokana na masilahi waliyokuwa nayo wazungu katika nchi hizo mbili Waandishi wa Habari walikulenga mara kwa mara kwa ajili ya mahojiano ambayo ulifanya mengi sana lakini mojawapo ni kuhusu Uhuru wa Zimbabwe na Afrika ya Kusini mwaka 1976 tarehe 23 Septemba.

Mwandishi alitaka kujua mazungumzo yake Mwalimu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Amerika Henry Kissinger ambaye ulimueleza ni lazima wavamizi watambue ni lazima wakubali utawala wa weusi waliowengi na Zimbabwe kamwe hatutawapa silaha kupigana bali tunaamini majadiliano ikishindikana tutatumia umoja wetu kuwaambia waondoke Zimbabwe.

Sauti yako Mwalimu inasikika katika nyanja mbalimbali maana hakubaki nyuma katika kuwatia moyo wanawake katika kugombania haki zao pia, ulitoa hotuba wakati ukifungua mkutano wa wanawake wa Afrika wa (African women Conference) Jijini Dar-es-salaam tarehe 02 Agosti 1962, uliofanyika katika ukumbi wa City hall Dar es Salaam.

Mwalimu nani asiyejua kuwa wewe ni mcha Mungu lakini ulisema waziwazi kuwa “Nchi yetu haina dini ila watu wake wana dini ulitamka maneno haya pale Tabora na kurejea maneno hayo pale Zanzibar ulipoalikwa na Mashekhe katika Baraza la Idi.

Ulitamka wazi wewe ni mkatoliki lakini si dini ya Tanzania wala si dini ya CCM wala si dini ya Serikali yako, ulisistiza bado tunahitaji kulikemea hili la udini na kuhakikisha tunapiga vita ukabila kwa sababu bado lipo kwenye baadhi ya fikra na vichwa vya watu waliofilisika kimawazo na kimtazamo wanapotafuta uongozi na kuona hawana hoja za msingi za kuomba uongozi, wao hukimbilia kwenye agenda hizo.

Nakumbuka Tanzania ya viwanda ilianza kitambo sana Mwalimu ulihamasisha viwanda, ambapo uliacha viwanda 414 vya serikali lakini hukuacha kuhamasisha sekta binafsi kujenga viwanda. Mwalimu sauti yako inasikika katika hotuba yako uliyoitoa tarehe 21 Agosti 1965 ulipoweka jiwe la msingi la kiwanda cha viberiti kilichopo eneo la Karanga mjini Moshi na kusisitiza sekta binafsi ina mchango mkubwa katika ustawi wa viwanda na kuleta maendeleo.

Mwaka 1986 Mwalimu ulingatuka katika madaraka ya urais na uliendelea kufanya safari mbalimbali mikoani na nje ya nchi. Ambapo ulitembelea viongozi wa Chama na Serikali Mkoa wa Kagera na kuhutubia katika viwanja vya shule ya msingi lubuli Bukoba Mjini 10 Septemba 1986. Ambapo ulizungumza na kujibu maswali ya wanachama wa CCM Tawi la Damwa tarafa Bunyezi Karagwe Kagera. Aidha ulichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Kusini iliyokuwa na wajumbe 28 na kupendekeza mambo makubwa ambayo leo yanatekelezwa na viongozi wetu.

Mwalimu ulitilia manani suala la sayansi na tekinolojia kwa kuwa ulijua hakika dunia ya leo bila hivyo utabaki nyuma, ulifanya mkutano huo katika ukumbi wa Karimjee Dar-es-salaam tarehe 18 Oktoba 1989 na kusisitiza kwa kutuasa dunia ijayo ni ya sayansi na tekinolojia kama hatutangamua hilo mapema tutaachwa nyuma kimaendeleo.

Kwako Mwalimu hakuna jambo dogo wala kubwa yanapokuja masilahi ya Watanzania Mwalimu ulihutubia Wilaya ya Bunda Mkoa wa Mara tarehe 10 April 1999, upandaji miti kitaifa sauti yako inasikika hadi leo katika masuala ya elimu ya watu wazima, mtu ni afya , chakula bora, kilimo uti wa mgongo, usalama barabarani na ufugaji wa kisasa. Kwa kuwa nani asiyefahamu kuwa wewe ni mwana mazingira namba moja na ni kati ya marais waliofanikiwa kutenga maeneo mengi hapa Tanzania ya kuhifadhi mapori yetu yawe ya akiba au ya wanyama pori.

Aidha, ulikaribishwa katika sherehe za Siku ya Wafanyakazi Duniani maarufu kama Mei Mosi (01 Mei 1995) Mkoani Mbeya mwaka 1995 na kupata fursa ya kuongea na hadhira ya Watanzania kwa ujumla. Hotuba hii imeweka misingi imara sana kwa Watanzania na funzo ambalo halitasahaulika katika historia ya nchi kuhusu suala zima la ubinafsishaji.

Kama hiyo haitoshi hotuba yako maarufu sana kwa Watanzania ile ya Kilimanjaro Hoteli pia uliongea na Waandishi wa Habari, mwaka 1995 kubwa likiwa ni kutuhatarisha na kutuasa juu ya nyufa zilizojitokeza za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao ni kiini na msingi wa umoja wetu kuishi bila kubaguana na kudharauliana kwa kuwa umoja ni muhimu katika kujenga Taifa letu na kuleta maendeleo jumuishi ambayo kwa sasa tuko uchumi wa kati.

Hotuba ile ina utajiri mkubwa wa kutuasa kwa kutuonyesha miiko na misingi ya uongozi, pia ikisisitiza kiongozi tumtakaye Tanzania awe na vigezo gani, hakika ni dira kwa Watanzania ya kuwa sahihi wakati wa kutumia haki yao ya msingi ya kupiga kura na kupata viongozi makini na sahihi.

Hotuba ya Mwalimu Nyerere kwenye Mkutano Mkuu wa CCM Dodoma 1995 ambapo aliwaambia wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama chake cha Mapinduzi kwamba Watanzania wamechoka na rushwa, kiongozi mtakayemchagua ashughulike na hali za wananchi wa Tanzania katika uchumi, viwandani, mashuleni, hospitalini, tatu watu wameanza kuzungumzia udini Tanzania hatuulizi dini ya mtu hata kidogo dini inatuhusu nini ?

“Sisi inatuhusu nini suala la dini inatuhusu nini sisi sasa watu wanazungumza dini wanajitapa kwa dini inatuhusu nini sisi tunataka kiongozi ambaye atatuondolea dhana hii ya udini”

Historia inatuambia kabla ya uhuru mwaka 1957, Mwalimu Nyerere alipigwa marufuku kuhutubia mikutano ya hadhara kwa miezi sita wakati serikali ya Uingereza ikidai kuwa hotuba zake zilichochea raia kuchukia serikali ya Malkia.

Ambapo mwaka 1958 Mwalimu alipelekwa mahakamani kwa madai kuwa ulikuwa amewakashifu wakuu wa Wilaya wa kikoloni, ndipo ulipohukumiwa kulipa faini ya shilingi elfu tatu au kifungo cha miezi sita . ukatoa faini hiyo kutokana na umoja na mshikamano wa Watanganyika.

Watanzania wanakuahidi kamwe hawatakusahau daima watakuenzi na kufuata misingi na miiko uliyoiweka ili kuwa na taifa bora lenye Amani, Upendo, Mshikamano, Utu na Umoja PUMZIKA KWA AMANI MWALIMU