October 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Baadhi ya wanachama na viongozi wa Kamati Kuu walioudhuria Mkutano Mkuu Maalum wa Chama cha Sauti ya Umma SAU wa kuwapatisha wagombea wa urais Tanzania Bara na Zanzibar kwa ajili ya uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba mwaka huu. (Na Mpigapicha Wetu).

SAU yawateua Muttamwega, Zonga kuwania Urais

Na Rose Itono, TimesMajira Online

CHAMA cha Sauti ya Umma SAU kimewapitisha Muttamwega Mgaywa kuwa mgombea wa nafasi urais Tanzania Bara na Issa Mohamed Zonga kwa upande wa Zanzibar katika uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 28 mwaka huu .

Mbali na wagombea hao wa urais chama hicho pia kimemtangaza Satia Musa Sebwa kutoka Zanzibar kuwa mgombea mwenza wa nafasi hiyo.

Akiwatambulisha wateule hao kwa wanachama na viongozi wengine wa Kamati Kuu kupitia Mkutano Mkuu Maalum wa Chama Taifa, Mwenyekiti wa SAU Bertha Mpata amesema kuwa, wagombea hao wamepoatikana kwa munibu wa kanuni za chama chao.

Amesema, baada ya kukamilisha mchakato huo wa kuwapata wagombea hao jambo kubwa ambalo wanapaswa kufanya ni kusimamia taratibu za vyama ili kuondoa vurugu pamoja na kuwataka kuacha kutumia rushwa wakati wa kipindi chote cha mchakato wa kuelekea uchaguzi.

“Hawa ndio wagombea wa chama chetu kwa Bara na Zanzibar ambao wataambatana na mgombea mwenza mwanamama kutokea Zanzibar na kikubwa ni kwa wagombea wetu kusimamia taratibu za vyama ili kuondoa vurugu, ” amesema Mtapa.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa chama hicho, Majalio Kyara amewaasa wanachama kuwa na weledi na siku ya uchaguzi mara baada ya kumaliza kupiga kura kila mtu arejee nyumbani kusubiri matokeo ili kuepusha mikusanyiko inayoweza kusababisha kuvunjika kwa amani.

Aidha ameupongeza uongozi wa serikali ya awamu ya tano kwa mambo mazuri iliyofanya na kusema lengo la SAU ni kushika madaraka ya kuongoza nchi ili ifike pazuri zaidi.

Mteule wa nafasi ya urais SAU kwa upande wa Bara, Mgaywa amesema kupitia uzoefu wake katika siasa atasimamia maadili ya vyama wakati wote wa mchakato kwana SAU haipo kwa ajili ya upinzani tu badala yake imelenga maamuzi yanayofikiwa na chama hicho yaweze kufika Ikulu na kuleta mabadiliko.

“Rais Magufuli pamoja na kuwa kuna changamoto kadhaa amejitahidi sana na chama cha SAU kitakaposhika dola kitakuwa ni mbadala wa CCM na si upinzani,” amesisitiza Mgaywa.

Mgombea nafasi hiyo kwa upande wa Zanzibar, Zonga alisema, Chama cha SAU kinakubalika sana visiwani humo na atakapopata nafasi atasimamia misingi yote iliyotolewa na Tume sambamba na ofisi ya msajili.

Kwa upande wa mgombea mwenza, Sebwa amesema, atahakikisha anasimamia misingi yote ya chama wakati wote wa mchakato wa kuelekea uchaguzi sambamba na kuhakikisha ilani zote za chama hicho.

Wakati huohuo, Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza ambaye alikuwa mmoja wa wageni walioalikwa kwenye mkutano huo aliwataka SAU kuacha kujihusisha na vitendo vya rushwa ili kuendelea kulinda nidhamu ya chama chao.

Amesema, endapo watia nia watachaguliwa na Tume ya uchaguzi wahakikishe wanafuata maadili yanayotakiwa ya vyama vya siasa.