June 25, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Sangu: Michango ya Hifadhi ya Jamii ni Haki ya Msingi ya Mfanyakazi

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Ajira na Mahusiano ya Kazi, Deus Sangu, amewataka waajiri nchini kuhakikisha wanawasilisha michango ya hifadhi ya jamii ya wafanyakazi wao kwa wakati ili kulinda maslahi yao na kuwawezesha kunufaika ipasavyo na mafao wanayostahili wanapostaafu.

Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa 67 wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Waziri Sangu amesema Serikali inaendelea kusimamia mifuko ya hifadhi ya jamii ili kuhakikisha wafanyakazi wanapata usalama wa kipato baada ya kustaafu, huku akisisitiza umuhimu wa waajiri kutekeleza wajibu wao kwa mujibu wa sheria.

“Tunawaomba waajiri wote nchini kuhakikisha wanawasilisha michango ya wafanyakazi kwa wakati. Hii ni haki ya msingi ya mfanyakazi na ndiyo inayomuwezesha kuwa na uhakika wa maisha bora baada ya kustaafu. Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa wajibu huu kwa manufaa ya wafanyakazi na uchumi wa taifa,” amesema Sangu.

Waziri huyo pia amezungumzia malalamiko ambayo yamekuwa yakitolewa na baadhi ya waajiri kuhusu viwango vya michango ya hifadhi ya jamii, akisema tafiti mbalimbali zilizofanywa zimebaini kuwa viwango hivyo ni himilivu na vina uwezo wa kuhakikisha wafanyakazi wanapata mafao yanayoweza kuwasaidia kujikimu wanapostaafu.

“Kumekuwa na maoni kwamba viwango vya michango ni vikubwa, lakini tafiti zilizofanyika zimeonyesha kuwa viwango vilivyopo vinaweza kubebwa na waajiri na wafanyakazi huku vikihakikisha mfanyakazi anapata mafao stahiki yatakayomsaidia katika maisha yake ya baada ya ajira,” ameongeza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Wakili Suzanne Ndomba-Doran, amesema chama hicho kitaendelea kushirikiana na Serikali pamoja na waajiri wa sekta binafsi ili kuimarisha mifumo ya hifadhi ya jamii na mazingira bora ya kazi nchini.

“ATE itaendelea kufanya kazi kwa karibu na Serikali na wadau wengine kuhakikisha tunakuwa na mfumo imara wa hifadhi ya jamii unaolinda maslahi ya wafanyakazi na wakati huo huo kusaidia ukuaji wa biashara na uchumi wa nchi,” amesema Wakili Ndomba-Doran.

Aidha, amesema ushirikiano kati ya Serikali, waajiri na wafanyakazi ni nguzo muhimu katika kujenga mazingira bora ya ajira na kuongeza tija katika maeneo ya kazi.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Masha Mshomba, amesema waajiri ambao wamekuwa wakichelewesha kuwasilisha michango ya wafanyakazi wamepewa fursa ya msamaha wa faini ili kuwawezesha kulipa madeni yao na kurejea katika mfumo rasmi wa uwasilishaji wa michango.

“Tumetoa msamaha wa faini kwa waajiri wenye madeni ya michango ya wafanyakazi ili kuwapa nafasi ya kurekebisha hali hiyo. Fursa hii itaendelea hadi mwezi Desemba mwaka huu, hivyo tunawahimiza kuitumia kabla ya muda huo kuisha,” amesema Mshomba.

Naye Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Hery Mkunda, amewataka wafanyakazi nchini kufanya kazi kwa weledi, uadilifu na kujituma huku wakitambua kuwa haki zao za kikazi zinaambatana na wajibu wa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

“Ni muhimu wafanyakazi kutambua kuwa haki na wajibu ni vitu vinavyokwenda pamoja. Tunapaswa kufanya kazi kwa weledi, uaminifu na uwajibikaji ili kuongeza tija katika maeneo yetu ya kazi na kuchangia maendeleo ya taifa,” amesema Mkunda.

Mkutano huo wa 67 wa ATE umezikutanisha taasisi mbalimbali za Serikali, waajiri na wadau wa sekta ya ajira kujadili masuala yanayohusu mazingira ya kazi, hifadhi ya jamii na mikakati ya kuimarisha ustawi wa wafanyakazi pamoja na ukuaji wa uchumi wa Tanzania.