June 25, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Falsafa ya 4R Ya Rais Samia, yaongeza Ushirikiano wa Tanzania,China

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

Balozi wa Tanzania nchini China, Suleiman Haji Suleiman, amesema ushirikiano wa kidiplomasia na kiuchumi kati ya Tanzania na China umeendelea kuimarika kwa kipindi cha miaka 61, na kuzaa mafanikio makubwa katika sekta mbalimbali za maendeleo, biashara na uwekezaji.

Akizungumza kuhusu uhusiano huo, Balozi Suleiman amesema mafanikio yanayoonekana leo ni matokeo ya mazingira bora ya uwekezaji na diplomasia ya uchumi yanayoendelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia falsafa ya 4R inayojumuisha Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Kujenga Upya.

Amesema Tanzania na China zimejenga ushirikiano wa muda mrefu unaotokana na urafiki wa kihistoria, kuaminiana na manufaa ya pamoja, hali iliyochochea ukuaji wa biashara, uwekezaji na fursa za maendeleo kwa wananchi wa mataifa hayo mawili.

“Katika kipindi hiki cha Awamu ya Sita, Tanzania na China zinaendelea kunufaika na fursa nyingi za kiuchumi ambazo zinaweza kuongeza ustawi wa wananchi na kukuza uchumi wa nchi zetu,” amesema Balozi Suleiman.

Ameongeza kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana kwa karibu na China katika maeneo mbalimbali kwa lengo la kuongeza kiwango cha biashara, kuvutia uwekezaji zaidi na kuharakisha maendeleo ya kiuchumi.

Kuhusu Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), Balozi Suleiman amesema Ubalozi wa Tanzania jijini Beijing utakuwa na banda maalum litakalowakutanisha wadau mbalimbali, ikiwemo Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uwekezaji Tanzania (TISEZA), kwa lengo la kutangaza fursa za uwekezaji, biashara na utalii zilizopo nchini.

Katika sekta ya elimu, amesema ushirikiano kati ya Tanzania na China umeendelea kuwanufaisha Watanzania wengi kupitia ufadhili wa masomo, mafunzo ya kitaaluma na programu za kubadilishana wanafunzi pamoja na wahadhiri kati ya taasisi za elimu za nchi hizo mbili.

Aidha, amesema ubalozi unaendelea kufungua milango ya ushirikiano wa kitaaluma katika nyanja za sayansi, teknolojia na ubunifu ili kuongeza ujuzi na ushindani wa Watanzania katika soko la kimataifa.

Akizungumzia sekta ya utalii, Balozi Suleiman amesema idadi ya watalii kutoka China imeongezeka kwa kiwango kikubwa katika miaka ya karibuni, kutoka takribani watalii 18,000 mwaka 2022 hadi zaidi ya 82,000 mwaka huu, jambo alilosema ni matokeo ya kuimarika kwa mahusiano ya kidiplomasia na kiuchumi kati ya nchi hizo mbili.

“Serikali itaendelea kutumia diplomasia ya uchumi kufungua masoko mapya, kuvutia uwekezaji na kuongeza fursa za elimu, ajira na maendeleo kwa Watanzania,” amesema.

Hata hivyo, amebainisha kuwa licha ya ukuaji wa biashara kati ya Tanzania na China, bado kuna changamoto ya uwiano wa biashara kati ya nchi hizo mbili. Amesema takwimu zinaonesha kuwa kati ya mwaka 2021 na 2025 thamani ya biashara kati ya Tanzania na China ilifikia dola za Marekani bilioni 23.2, ambapo Tanzania iliuza bidhaa zenye thamani ya dola bilioni 1.8 pekee, huku ikiagiza bidhaa kutoka China zenye thamani ya dola bilioni 21.3.

Kwa mujibu wa Balozi Suleiman, suluhisho la changamoto hiyo ni kuongeza thamani ya mazao yanayozalishwa nchini, kuboresha vifungashio na kuimarisha uzalishaji unaokidhi viwango na mahitaji ya soko la kimataifa ili kuongeza mauzo ya bidhaa za Tanzania katika soko la China.