Na Zena Mohamed, TimesMajira Online, Dodoma.
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje (Outer Ring Road) yenye urefu wa Kilomita 112.3 katika Jiji la Dodoma kesho.
Akieleza kuhusu uwekaji jiwe la msingi katika mradi huo jijini hapa leo Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka katika kikao chake na waandishi wa habari amesema kuwa barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha lami hali itakayoruhusu uwepo wa fursa mbalimbali.
Amesema hafla ya uwekaji jiwe la msingi katika mradi huo itafanyika katika eneo la Makutupora-Veyula kuanzia saa 1:00 asubuhi huku akisema maandalizi muhimu yote yamekamilika.
Mtaka ameeleza kuwa ujenzi huo utagharimu kiasi cha shilingi za kitanzania Bilioni 221 na kwamba ujenzi huo utakamilika ifikapo mwaka 2025 na kuweka mandhari safi ya Jiji la Dodoma.
Pia Mtaka ametaja fursa zitakazo tokana na barabara hizo kuwa itakuwa kiungo muhimu kwa barabara nyingine za Jiji la Dodoma ikiwa huku akisema imegawanywa Kwa wakandarasi wawili ambao ni M/sAVIC INTL Project na China Civil Engineering Construction Cooperation zote kutoka Jamhuri ya watu wa China.
Hata hivyo ametumia nafasi hiyo kuzitaka Taasisi zote za Serikali mkoani hapa,Taasisi binafsi,makundi mbalimbali na mikoa jirani pamoja na wananchi wake kujitokeza kwa wingi katika hafla hiyo ili kubaini mapema fursa nyingi zitakazo patikana kupitia ujenzi huo.
“Nitoe maelekeza kwa jeshi la polisi Mkoa wa Dodoma kuruhusu madereva wa daladala (kukatisha ruti) kufanya usafirishaji wa abiria kutoka sehemu mbalimbali kuja katika eneo la Makutupora-Veyula ili kurahisisha huduma hiyo kuwawezesha watu kufika kwa wakati katika eneo hilo,”amesema.
Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa barabara nchini(TANROADS),Mkoa wa Dodoma Mhandisi Leonard Chimagu amesema kuwa ujenzi wa barabara hiyo ya mzunguko utajengwa kwa awamu mbili.
Akifafanua awamu hizo mbili amesema kuwa awamu ya kwanza itahusisha ujenzi wa Kilomita 52.3 kupitia Nala,Veyula,Mtumba na Ihumwa wakati awamu ya pili itahusisha Kilomita 60 kupitia Ihumwa, Matumbulu na Nala.
“Ujenzi huu ukikamilika utafungua fursa za kiuchumi kwa wakazi wa Dodoma ikiwa ni pamoja na kuondoa msongamano wa magari uliopo sasa kwa kuwa magari yanayoenda mikoa mingine watatumia barabara hizo bila kupitia ndani ya Jiji,”amesema.
More Stories
DC Korogwe awataka viongozi wa vijiji kuwatumikia wananchi kwa uadilifu
Premier Bet yamtangaza mshindi mkubwa
Dkt. Kazungu atembelea miradi ya umeme Dar es Salaam