May 17, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Samia kushuhudia ujazaji maji Bwawa la Nyerere leo

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

RAIS Samia Suluhu Hassan, leo anatarajia kuwaongoza Watanzania kushuhudia ujazaji wa maji katika Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere (JNHPP).

Hafla hiyo inafanyika Rufiji, ikiwa ni mwendelezo wa juhudi za nchi kupambana na changamoto ya umeme inayolikumba Taifa, mara kwa mara kunapotokea ukame.

Taarifa za Rais Samia kushuhudia tukio hilo, zimetolewa na Waziri wa Nishati, January Makamba na kusema hayo ni maendeleo makubwa kwa historia ya Tanzania katika kuendeleza mradi huo mkubwa nchini.

Alisema kuwa, mradi huo kwa sasa umefikia asilimia 78 ya utekelezaji wake tangu kuanza kwake.

Alisema kuwa, kutokana na ukubwa wa zoezi hilo na umuhimu wa mradi huo kitaifa, ni ishara kuwa ndoto za Taifa katika kutekeleza mradi huo zinatimia, ambapo zoezi hilo litazinduliwa na kushuhudiwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Alifafanua kuwa, handaki la kuchepusha maji lina urefu wa mita 700, yaani viwanja saba vya mpira wa miguu na lilijengwa miaka mitatu iliyopita kwa gharama ya sh. takribani Bilioni 235.

Bwawa hilo pia litakuwa ni kivutio cha watalii kwa kuwa liko ndani ya hifadhi na litabadili kabisa taswira ya hifadhi hiyo na thamani ya hifadhi hiyo itaongezeka ndani na nje ya Tanzania.

Murugenzi Mkuu wa TANESCO, Maharage Chande aliweka wazi kuwa inakadiriwa kuwa misimu miwili ya kipindi cha mvua, itaweza kujaza maji katika bwawa hilo.

“Tunaanza kujaza maji kesho (leo) ambapo kuna mvua za vuli, pia tunategemea mvua za masika mwezi Machi 2023, ambazo zitakuwa mvua za msimu wa kwanza, pia tutapata vuli ndani ya kipindi hicho, kisha tutapata zile za masika katika mwaka 2024 pamoja na vuli ya kipindi hicho, hivyo mvua mbili kubwa za masika zinaweza kujaza bwawa kwa hesabu zilizopo,” Alisisitiza Chande.

Zoezi hilo litahudhuriwa na watu takribani 2000 na litatangazwa moja kwa moja kupitia vyombo vya habari ili watanzania wote waweze kushuhudia maendeleo na hatua iliyofikiwa katika kutekeleza mradi huo.