May 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Samia awapa maagizo mazito viongozi MSM

*Akerwa migogoro ya wenyeviti wa halmashauri, wakurugenzi,
ashukia wapigaji fedha za mapato, atoa maelekezo muhimu manne

Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline, Zanzibar

RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa maagizo matatu kwa viongozi wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa (MSM) ikiwemo kuondoa migogoro kati ya wenyeviti wa halmashauri na wakurugenzi wao.

Amesema migogoro hiyo inachelewesha maendeleo ya wananchi, na wakati mwingine inamlazimisha kuwatenganisha kwa kumuhamisha mkurugenzi ili kuleta utulivu kwenye halmashauri husika.

Hayo yamesemwa jana na Waziri wa TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 38 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) kwa niaba ya Rais Samia. Mkutano huo unafanyika kwa siku tatu mjini Zanzibar.

Mchengerwa alitaja maagizo mengine yaliyotolewa na Rais Samia, ni pamoja na kuwataka viongozi wa MSM kuhakikisha wanakusanya mapato, lakini mapato hayo yatumiki viuri na wao wasiwe sehemu ya kufuja mapato hayo.

Amesema anazo taarifa kuwa baadhi ya halmashauri kuna mashine hewa za kukusanya mapato kielektroniki (POS), lakini baadhi ya POS zimezimwa, na mapato hayaingii serikalini.

Agizo la tatu ni kutaka viongozi kutatua kero za wananchi, kwani baadhi ya viongozi kwenye ngazi ya mikoa na wilaya wameshindwa kutatua kero za wananchi, mpaka viongozi wa kitaifa wanapofika kwenye maeneo yao, ndipo wanaelezwa kero hizo, na kutaka kero zifanyiwe kazi kabla ya viongozi wa kitaifa hawajakwenda kwenye maeneo hayo.

“Rais anatoa maagizo kwa viongozi wa Serikali za Mitaa. Mosi, Rais ametaka viongozi kuondoa migogoro baina yao, na hasa Mwenyekiti wa Halmashauri na Mkurugenzi wake. Baadhi ya halmashauri, Mwenyekiti na Mkurugenzi wake wanakuwa hawaelewani. Sasa unajiuliza wote mnajenga nyumba moja, nini kinafanya mgombane!

Jambo hilo linafanya Rais aweze kuwatenganisha viongozi hao kwa kumuondoa Mkurugenzi. Pili, Rais anataka ukusanyaji wa mapato ufanyike kwa usahihi, lakini pamoja na hayo yasitumike vibaya, na viongozi wasiwe sehemu ya ufujaji mapato hayo. Na tatu, Rais ametaka viongozi kutatua kero za wananchi mapema, na sio wananchi wanatoa kero zao wanapowaona viongozi wa kitaifa,” amesema Mchengerwa.

Mchengerwa amesema baadhi ya halmashauri wanafanya vizuri katika ukusanyaji mapato, kwani baadhi yao zimevuka asilimia 100. Lskini amebaini baadhi ya halmashauri zinaweka makadirio madogo kwenye ukusanyaji, hivyo TAMISEMI wanakuja na vigezo vipya katika ukusanyaji mapago ikiwemo kuwa wabunifu katika ukusanyaji huo.

Waziri Mchengerwa amesema Rais Dkt. Samia alitoa kila nyenzo na fedha za kuwezesha kutekeleza miradi ya wananchi, hivyo Wakurugenzi wanategemewa sana na Rais Dkt. Samia kuona wanasimamia na kukamilisha miradi hiyo ili iweze kuleta tija kwa wananchi.

“Wakurugenzi waondoleeni msongo wa mawazo wenyeviti wenu wa halmashauri, madiwani, wenyeviti wa vijiji na vitongoji kwa kutekeleza miradi ya wananchi.

Na simnajua sasa hivi ni saa saba (kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu)!… sio saa ya mkononi, nadhani mmeshanifahamu,” alisema Mchengerwa.

Mchengerwa aliwataka wanawake kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, lakini pia kushiriki kwenye kupiga kura, kwani wanawake wana uwezo mkubwa kwenye kuongoza.

Mchengerwa amesema amebeba hoja ya madiwani ya kutaka madiwani waongezewe posho na maslahi mengine, kwani hiyo italeta chachu na tija katika kusukuma mbele maendeleo ya wananchi, na kuongeza kuwa, amepokea hoja hiyo, na tayari mengine alishamfikishia Rais Dkt. Samia.

Kwenye taarifa yake, Makamu Mwenyekiti wa ALAT Taifa, Sima Sima aliomba, pamoja na mambo mengine, ipo haja kwa madiwani na wakurugenzi kuongezewa posho na maslahi mengine, nia ni kuboresha maisha yao, na kuweza kufanya kazi kwa ufanisi.