June 16, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Samia aridhia ombi la Umoja wa Afrika

*Ni la kuwa mwenyeji na kuongoza maadhimisho ya miaka 20 tangu kuanzishwa Baraza la Amani na Usalama la AU, kuhudhuriwa na marais wastaafu

Na Jackline Martin,Timesmajiraonline,Dar

RAIS Samia Suluhu Hassan, ameridhia ombi la Umoja wa Afrika (AU) la kuwa Mwenyeji na kuongoza maadhimisho ya miaka 20 tangu kuanzishwa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika yatakayofanyika Mei 25, mwaka huu (kesho kutwa).

Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba, wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Amesema maadhimisho haya yanatarajiwa kuhudhuriwa na wageni takriban 120 kutoka nchi mbalimbali.

Miongoni mwa watu mashuhuri watakaoshiriki maadhimisho hayo ni pamoja na Makamu Rais wa Uganda, Jessica Alupo, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat na Rais Mstaafu wa Nigeria, Olesegun Obasanjo.

Wengine Rais Mstaafu Burundi, Domitien Ndayizeye, Rais Mstaafu wa Msumbiji, Joachim Chissano na Rais Mstaafu wa Tanzania, Jakaya Kikwete.

“Kwa hapa nchini, tumealika takriban washiriki 700. Hivyo, Watanzania hatuna budi kujiandaa kupokea ugeni huo mkubwa,” alisema Waziri.

Amesema maadhimisho hayo yatatoa fursa kwa wajumbe wa baraza kujadili namna bora ya kuimarisha diplomasia na masuala ya ulinzi na usalama katika Bara la Afrika na dunia kwa ujumla.

Vilevile amesema maadhimisho hayo pia yamelenga kupokea maoni ya wajumbe kuhusu utendaji kazi wa Baraza na namna ya kuweza kuliimarisha huku akiainisha baadhi ya changamoto zinazolibanili baraza hilo ikiwemo kuendelea kwa migogoro ya muda mrefu ya Somalia, DRC, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Libya pamoja na Sudan.

“Katika kusherehekea maadhimisho hayo Mei 24, 2024 kutafanyika Mjadala wa Wazi kwenye Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ili kupokea maoni yao kuhusu utendaji kazi wa Baraza na namna ya kuweza kuliimarisha,” amesema.

Pia Waziri Makamba amesema Maadhimisho hayo yanatoa fursa kwa Waafrika wote na watu wote wenye kuitakia mema Afrika kutoa maoni yao ya kuliimarisha Baraza ili liweze kushughulikia changamoto za kiusalama kwenye Bara la Afrika.

Makamba amewahimiza wadau wote walioalikwa kushiriki kwenye kilele cha maadhimisho siku hiyo kujitokeza kwa wingi kumuunga mkono Rais Dkt. Samia kwa heshima hiyo kubwa aliyopewa na Umoja wa Afrika.

“Nawakaribisha wananchi kujitokeza kwa wingi kwenye Mjadala Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ili kutoa maoni yao.

Maadhimisho hayo kwa mwaka huu yamebebwa na kaulimbiu isemayo “Miaka 20 ya Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika ikiwa Chombo cha Maamuzi; Miongo miwili ya Afrika ya Amani na Usalama tunayoitaka.”