May 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Samia apeleka fedha za Uhuru kwenye mabweni 8

Na Mwandishi wetu,Dar es Salaam 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri mkuu Sera Bunge na Uratibu, George Simbachawene amesema fedha zilizokuwa zimetengwa na Wizara na Taasisi kwa ajili ya Maadhimisho ya Sherehe za Uhuru mwaka huu zitapelekwe Ofisi ya Rais – TAMISEMI na kutumika kujenga mabweni katika shule nane za Msingi za wanafunzi wenye mahitaji maalum hapa nchini.

Akizungumza hayo jana na Waziri wa Nchi Ofisi ya waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu George Simbachawene katika mkutano wake na waandishi wa habari Mjini Dodoma,amesema fedha hizo kiasi cha sh. 960,000,000 zitatumika kujenga shule ya msingi Buhangija Shinyanga, Goweko Tabora, Darajani Singida, Mtanga Lindi, Songambele Lindi, Msanzi Rukwa,  Idofi Njombe, na Longido Arusha.

Amesema dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni  kuwajali na kuwajengea mazingira rafiki watu wenye mahitaji maalum hapa nchini. “Hili ni jambo kubwa la kishujaa na la kupongezwa sana na Wananchi wote wa Tanzania,”amesema na kuongeza

“Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 61 ya Uhuru wa Tanzania Bara mwaka huu 2022 yatafanyika kwa Midahalo na Makongamano mbalimbali yatakayofanyika katika Wilaya zote hapa nchini kujadili, kutafakari kwa pamoja na kukumbuka tulikotoka, tulipo na tunakoelekea kuhusu Maendeleo Endelevu ambayo Nchi yetu adhimu Tanzania imeyafikia,”amesema

Amesema hivyo siku hiyo  hakutakuwa na Gwaride na shughuli nyingine za Kitaifa,maadhimisho ya miaka 61 ya uhuru yanatarajia kuadhimishwa kwa Kauli mbiu inayosema  “AMANI NA UMOJA NI NGUZO YA MAENDELEO YETU”.

“Makongamano hayo yatatanguliwa na ratiba mbalimbali kwa Viongozi wa Mikoa na Wilaya kufanya shughuli za Kijamii kama vile kufanya usafi katika maeneo ya Hospitali, shule, nyumba za Wazee na makundi yenye mahitaji maalum”amesema

Aidha amelekeza Ofisi zote za Serikali hapa nchini kupambwa kwa mapambo ya rangi za Bendera ya Taifa pamoja na picha ya  Rais Dkt.Samia.