May 17, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Sagini atoa maagizo kufuatia ajali ilioua 13

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Jumanne Sagini amemuagiza Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini pamoja na vyombo vya usimamizi wa sheria barabarani kuwachukulia hatua ikiwezekana kuwafutia leseni madereva wote wanaokiuka sheria ili kupunguza vifo vinavyotokana na uzembe.

Sagini ametoa agizo hilo mara baada ya kufika eneo iliyotokea ajali na kutembelea majeruhi katika ajali iliyohusisha gari la Ally’s lililokuwa linatoka Dar es Salaam kwenda Mwanza kugonga treni ya mizigo katika makutano ya barabara na reli maeneo ya Manyoni mkoani Singida.

“Nimuelekeze Kamanda wa Usalama Barabarani Taifa kupitia idara zake chini ya RTO wawe wakali kuondoa huruma kwa watu wanaovunja sheria kama hawa, vyombo vyote vya usimamizi wa sheria za barabarani ikiwemo Latra na Polisi lazima tuchukue hatua madhubuti kusaidia Watanzania wasipoteze maisha kama haya ambayo yametokea ni uzembe mkubwa wa Dereva wetu”, ameeleza Sagini.

Aidha anaelezea sababu za ajali hiyo kuwa kitendo cha Bus kugonga kichwa cha Treni mpaka kikahama kikaacha njia yake inaonyesha dhairi kwamba dereva alikuwa kwenye mwendo mkali sana.

“Jambo hili linatuhuzunisha na mara zote tumekuwa tukiwakumbusha madereva na wamiliki wa magari, madereva wao wazingatie sheria za usalama barabarani bahati nzuri eneo hili linajulikana, dereva huyu wa kampuni ya Ally’s sio mgeni barabara hii kwamba unapofika Manyoni baada ya kituo kuna reli halafu round about, ambapo kwa maeneo yote anapaswa kwenda mwendo mdogo”, ameeleza Sagini.

Pia anatoa wito kwa abiria kuhusu madereva wanapovunja sheria.

“Wito wangu kwa Watanzania wanapokuwa kwenye vyombo vya moto kama hivi wasaidie kuwakumbusha madereva juu ya wajibu wao wa kuendesha gari kwa kuzingatia sheria za usalama barabarani,”.

Mmoja kati ya majeruhi ameomba mamlaka ya usafirishaji iweze kuzingatia juu ya vidhibiti mwendo kwenye magari ili kupunguza ajali za barabarani.

“Sijui kama kuna utaalam wa ku monitor speed za magari kwa sababu abiria hawapo conscious muda wote hawawezi kujua kama gari linaweza kuwa linakimbia kwa speed, kwa hiyo kama kuna namna ambayo magari yanaweza yakadhibitiwa,“ ameeleza majeruhi.