May 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Sagini atangaza siku 14 kuondoa namba za ‘3D’,madereva wa serikali kukiona

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imetangaza siku 14 kwa watumiaji wa vyombo vya moto barabarani kuondoa namba za magari zilizoongezwa ukubwa maarufu kama ‘3D.

Pia na vimulimuli kwa magari yote yasiyoruhusiwa kuwekwa, namba zote zenye vibao vyeusi na zizonatumia namba za chasis, taa zozote na stika ambazo zimeongezwa kwa matakwa ya wamiliki au madereva.

Akizungumza na Waandishi wa Habari baada ya Kikao cha Baraza la Taifa la Usalama Barabarani Machi 04, 2024 Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani Jumanne Sagini (Mb) amesema kuwa namba hizo hazitengenezwi na wakala aliyepata kibali kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS.

Bali zinatengenezwa kiholela mtaani na herufi hizo kubandikwa juu ya namba halali na kutosomeka katika umbali unaotakiwa ambapo katika viwango vya TBS namba ya chombo cha moto isomeke kwa umbali usiopunga mita 100 ambapo 3D haifiki kiwango hicho.

“Mambo yote yanayohusiana na usalama barabarani hufanywa kwa mujibu wa sheria sio utashi wa mtu mmoja mmoja au binafsi kuhusu matumizi ya namba yamebainishwa vizuri sana na sheria kwamba namba zinazowekwa zinatakiwa ziweje? ziwe zimeandikwa na nani? anayetambulika na nani? ziwe na ubora gani? namba hizi zote hazijawekwa kwa bahati mbaya,”.

Amesisitiza kuwa zoezi la ubanduaji wa namba zilizoongezwa ukubwa litaendeshwa hata kwenye magari ya Serikali ambapo yakibainika na makosa ya namna hiyo wanaotumia watachukuliwa hatua.

Sagini amesema kuwa,ving’ora vinatoa ishara fulani ili magari mengine yaweza kupisha.

“Nisisitize kuwa, magari yanayotakiwa kuwekwa bing’ora yanajulikana kama ya Polisi, Zimamoto ya wagonjwa na yale yaliyopo katika misafara ya viongozi kufanya hivyo bila kibali maalum ni ukiukwaji wa sheria,”.

Kwa upande wake Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini ambaye pia ni Katibu wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Ramadhani Ng’anzi ameeleza kuwa, wanapiga marufuku namba zilizoongezeka ukubwa kwa sababu kiusalama.

Ambapo ameeleza kuwa 3D sio salama kutokana na mifumo na kamera kutoitambua huku na namba za magari lazima ziwe 2D.

“Baada ya tarehe 15 Machi, 2024 tutaendelea kuzibandua na tukiona ile plate namba haisomeki vizuri tutakukamata na hili zoezi mnatakiwa muondoe wenyewe kwa hiyari la sivyo Jeshi la Polisi litakukamata kwa kuvunja sheria hata tukikuta namba haisomeki vizuri yaani imechubuka,”amesema.

Aidha, Kamanda Ng’anzi ameongeza kuwa, operesheni itajumuisha na taa/sport light kinyume na taratibu za mtengenezaji au kibali kutoka kwa Mkaguzi wa magari na uwekaji wa stika za rangi mbalimbali kwenye taa kubwa mbele na nyuma ya gari, ambazo zinabadilisha mwanga wa taa halisi mfano stika nyeusi, blue nyekundu na tinted.