November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ruvuma Queens yazipiku timu VPL

Na Mwandishi Wetu, Songea

TIMU ya wanawake ya Ruvuma Queens inayoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara maarufu kama ‘Serengeti Light Women’s Premier League’ wamezipiku baadhi ya timu zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) baada ya kubadili mfumo na kuingia kwenye mfumo wa kisasa wa uendendeshaji wa klabu hiyo.

Kwa sasa timu hiyo inajulikana kama ‘Ruvuma Queens Football Club Company Limited’ baada ya Machi 26, mwaka huu kupata Leseni ambayo sasa inawaruhusu kujiendesha kwa mfumo wa kampuni.

Afisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Onesmo Ndunguru, ameliambia Majira kuwa, mchakato wa mabadiliko ya klabu hiyo ambayo ilianzishwa mwaka 2015 ulianza Januari mwaka huu hadi Machi 26 ambapo walipata cheti rasmi kunachowatambulisha kama kampuni.

Amesema, kutokana na kufanikisha jambo hilo mipango yao kwa sasa ni kufikia malengo kadhaa waliyoyaweka ikiwemo kupata mafanikio makubwa zaidi hata ya baadhi ya klabu mbalimbali hapa nchini zinazoshiriki Ligi Kuu kwa muda mrefu.

Ndunguru amesema kuwa, kama isingekuwa janga la ugonjwa wa Corona, basi wangekuwa mbali kwani hadi sasa tayari wameshamaliza ukarabati wa ofisi za klanu hiyo lakini pia wameshamaliza ukatabati wa hostel za wachezaji wao ambao baadhi wanatoka nje ya mji huo.

“Kwanza tunawashukuru viongozi wetu kwa kufanikisha jambo hili kwani hadi sasa tumeshapata cheti kinachotutambulisha kama kampuni ambayo itakuwa na wakurugenzi wawili ambao ni mwanzilishi wa klabu mwenye hisa 55 huku yule aliyemshawishi kuingia kwenye mfumo huo akichukua hisa 45. Kwa kuanzia tunataka kuzipiku baadhi ya timu zilizoshiriki Ligi Kuu kwani tayari tumeshapata ofisi na hosteli za kisasa ambazo pia zinaweza kutumika na zaidi ya timu mbili, ” amesema Mtendaji huyo.

Ndunguru ameweka wazi kuwa, pia mipango yao ni kuhakikisha wanachukua alama tatu katika mechi zao zote zilizobaki msimu huu endapo Serikali itaruhusu michezo kuendelea huku pia msimu ujao wakijipanga kuwa na kikosi bora ambacho kitaweza kupambana na kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake

Amesema kuwa, hadi Ligi inasimama walikuwa na utaratibu wa kununu goli moja kwa zaidi ya sh. 100,000 jambo ambalo lilewaweka kwenye nafasi nzuri kwani hadi Machi 16, walikuwa nafasi ya nne wakiwa na pointi 27 huku wafungaji wao Diana Lucas akiwa na goli saba sawa na Amina Ramadhani, Husna Mpanja amefunga goli sita huku Mariam Keneth akifunga tano.

Mtendaji huyo amesema kuwa, hadi sasa wachezaji wao wanaendelea vizuri na programu mbalimbali waliopewa na viongozi wao wa benchi la ufundi kuhakikisha wanakuwa bora zaidi na kufanya vizuri katika mechi zao zilizobaki.