April 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RPC Tanga apiga marufuku uchomaji wa matairi siku ya mwaka mpya

Na Hadija Bagasha, TimesMajira Online, Tanga

Kamanda wa polisi Mkoa Tanga Safia Jongo amepiga marufuku tabia ya uchomaji wa matairi katika sikukuu ya mwaka mpya na kusisitiza kuwa mwenye nyumba atakayekutwa eneo lake limetumika kuchoma matairi na yeye atakamatwa.

Kamanda Jongo ametoa kauli hiyo wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika kituo kikuu cha polisi Chumbageni kilichopo jijini Tanga namna walivyojipanga kukabiliana na uhalifu katika siku hiyo.

Kamanda Jongo amesema jeshi la polisi haitavumilia uhalifu wa namna hiyo kwa kuwa matairi hayo yanaharibu miundombinu ya barabara ambayo serikali imetumia fedha nyingi kuitengeneza.

Amesema ni marufuku kuchoma matairi kwa kuwa yanaharibu miundombinu ya barabara ambayo serikali imetoa pesa nyingi kujenga huku watu wachache wakiziharibu kwa kusherehekea sherehe ambayo inapaswa kukaa ndani na kufanya ibada kwa kumshukuru Mungu kuweza kuuona mwaka mwingine.

Tunaelekea mwaka mpya hivyo mwaka mpya una changamoto nyingi sana za watu kusherehekea kwa kuharibu miundombinu ya serikali ikiwemo barabara wanachoma matairi nasema leo mwenye nyumba ambaye nyumba yako mbele yako nimelikuta tairi linachomwa nitaanza na wewe, “amesisitiza kamanda Jongo.

Ameongeza kuwa sina muhali naendelea na ile ile kauli mbiu yangu ya mama mkanye mwanao ukimmuacha mwanao siku ya mwaka mpya asherehekee kwa kuchoma matairi na kufanya uhalifu au uporaji nikimkamata usije nitajua umemtuma na wewe utakuwa mtuhumiwa namba mbili baada ya mtoto wako.

Katika hatua nyingi Kamanda Jongo amesema katika mkoa Tanga kumeibuka wimbi la kughushi noti bandia ambapo jeshi la polisi mkoani humo limefanikiwa kukamata jumla ya noti bandia zenye thamani ya milioni mbili na laki moja na arobaini huko wilayani Kilindi.

Kamanda Jongo amesema noti bandia hizo zilizokamatwa ni za shilingi elfu kumi kumi hivyo amewataka wananchi kuwa makini wanapofanya bidhaa za kununua au kuuza kuhakikisha wanazikagua noti wanazopokea kwa kuwa wimbi hilo la noti bandia bado lipo na wanakwenda madukani kununua vitu vya jumla na rejareja.

Sambamba na hayo kamanda Jongo amesema katika operesheni ya kuendelea kupambana na ujangili wamefanikiwa kukamata meno mawili ya tembo pamoja na nyama ya Twiga kilo 120 na kilo 2 za nyama ya swala vyenye thamani ya zaidi ya milioni 80.

“Tumekamata pikipiki yenye namba MC 630 aina ya Kinglion iliyokuwa imebeba meno mawili ya tembo lakini mbali na meno hayo ya tembo pia tulikamata kilo 120 za nyama ya twiga na nyama ya swala kilo 2,”amesema Kamanda Jongo.

This image has an empty alt attribute; its file name is WhatsApp-Image-2021-12-28-at-12.42.41-PM.jpeg
Kamanda wa polisi Mkoa Tanga Safia Jongo akiwaonyesha waandishi wa habari noti bandia walizokamata wilayani Kilindi Mkoani Tanga picha na Hadija Bagasha Tanga.