January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Royal Tour yavunja rekodi mapato ya utalii

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.

Filamu ya Tanzania The Royal Tour,imevunja rekodi kwa kuendelea kuliingizia Taifa mapato kupitia sekta ya Utalii kutoka trilioni 3.01 mwaka 2021 hadi trilioni 5.82 toka ilipozinduliwa Aprili 28 mwaka 2022 hadi sasa.

Ongozeko la mapato hayo ni kutokana kuongezeka kwa idadi ya watalii nchini kutoka nje na ndani ya nchini huku watu zaidi ya bilioni 1.2 wameisikia, kuiona na kuifuatilia Tanzania kupitia filamu hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa leo,Aprili 28,2023 Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbas,amesema kuwa Filamu hiyo imetimiza mwaka mmoja leo toka kuzinduliwa nchini Marekani ambapo amesema sekta hiyo inaingiza asilimia 25 ya fedha zote za kigeni nchini.

Dkt. Abbas amezungumzia ongozeko la watalii nchini ambapo amesema kuwa watalii kutoka nje wameongezeka kutoka 620,867 mwaka 2020 hadi 1,454,920 katika kipindi cha Disemba mwaka jana sawa na ongezeka la asilimia 57.7.

“Watalii wa ndani wameongezeka kutoka 788,933 mwaka 2021 hadi 2,363,260 mwaka 2022,”amesema.

Ameeleza kuwa Taasisi za utalii zimeendelea kuweka rekodi ambapo Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) ndani ya miezi sita kuanzia Julai hadi Aprili mwaka huu imeweka rekodi kwa kupata watalii 1,412,719, idadi ambayo hawajawahi kuipata tangu ianzishwe.

Aidha Mamlaka ya Hifadhi ya Taifa Ngorongoro (NCAA) kwa miezi tisa imepata watalii 638,950 na mapato ya sh. bilioni 146.3 ambayo hawajawahi kuyapata.

“Watalii wanaotembelea maeneo ya misitu na uwindaji picha wameongezeka kutoka 38,000 hadi 159,000 mtawalia kati ya mwaka 2021 na 2022,”amesema.

Pia amezungumzia manufaa katika njia ya anga amesema kuwa filamu hiyo pia imeleta manufaa kwa sekta ya usafiri wa anga ambapo miruko ya jumla ya ndege za kimataifa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) iliongezeka kwa asilimia 28 kutoka miruko 6,115 Aprili mwaka 2021 hadi 7,850 Aprili mwaka huu.

Vilevile ameeleza ushiriki wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika filamu ya Royal Tour,ulivyoleta mafanikio ambapo Novemba mwaka jana huko Dallas, Texas, Marekani, Taasisi ya Tuzo za Afrimma ilimtangaza Rais Samia kuwa Rais mwanamke wa kwanza Afrika kushinda Tuzo ya Mageuzi Katika Uongozi, wakitamka bayana kuwa mojawapo ya vigezo na mafanikio ni ushiriki wake katika Royal Tour.

Pia ameeleza kuwa watu takribani bilioni 1.2 mpaka sasa wameijua, kuisikia, kuiona au kuifuatilia Tanzania kutokana na filamu ya Royal Tour.

“Ikumbukwe Rais Dkt. Samia alifanya mahojiano na New York Times, New Yorker Magazine, CBS, Travel Weekly, Essence Magazine ikiwa ni sehemu ya Royal Tour, alifanya pia mikutano na wafanyabiashara wakubwa Marekani.

“Kupitia PBS Stations na PGW Digital, Wamarekani takribani milioni 100 wameiona Royal Tour kupitia PBS stations na milioni tano wametazama kupitia mitandao ya kijamii ya PGW. Na hii ni mpaka April Mosi mwaka huu na kazi inaendelea,

“Kupitia mitandao ya Amazon na Apple TV+, watu takribani milioni 20 duniani wameitazama filamu ya Royal Tour, kupitia mitandao ya China: Royal Tour iliyotafsiriwa Kichina kupitia mitandao ya Baidu, Bilibili, Hainan Channel na Hainan Digital imewafikia watu zaidi ya milioni 50,”amesema.

Pamoja na hayo amesema kuwa uwekezaji umeongezeka kwa mujibu wa ripoti ya kituo cha Biashara nchini (TIC), hamasa na mguso wa filamu ya Royal Tour imeongezeka.

“Akiwa Marekani mwaka jana, Rais Dk. Samia wakati wa Royal Tour alishuhudia mikataba nane ya awali ambayo miwili ikihusu sekta binafsi na sita ya kiserikali. Mikataba hii uwekezaji wake utafikia thamani ya zaidi ya sh. trilioni 11.7,

“Na hadi sasa baadhi ya wawekezaji hao wameshafika nchini na kupewa ardhi kama kampuni ya Camdemi HB (Hotel Arumeru), kampuni ya Polo Properties imeshasajili mradi TIC na kampuni za Northern New Feed zimeshafika nchini na taratibu zinaendelea,

“Hadi Machi mwaka huu, jumla ya miradi mikubwa 26 ya uwekezaji katika utalii imesajiliwa, ikilinganishwa na miradi 16 iliyosajiliwa Machi mwaka 2020 kabla ya Royal Tour,”amesema.