January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

‘Royal Tour’ ya Rais Samia Suluhu Hassan yaanza kuleta neema Tanzania, Wawekezaji waanza kumiminika


 
Na Mwandishi Maalum,timesmajira,Online

SHUGHULI za Royal Tour zilizokuwa zikifanywa kwa mara ya kwanza nchini na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan za kutangaza vivutio vya Utalii, Biashara na Uwekezaji nchini zimeanza kuzaa matunda kwa wawekezaji kuanza kujitokeza kwa uwekezaji wa hoteli za kisasa ndani ya hifadhi za Taifa.

Hayo yamebainishwa na Serikali kupitia kwa Waziri wa Maliasili na Utalii , Dkt. Ndumbaro mara baada ya mkutano  wake maalum na  Wawekezaji uliofanyika Dar es Salaam mapema leo

Ambapo amekutana na wawekezaji hao kutoka Bara la Ulaya katika nchi ya Bulgaria watakaojenga hotel za Nyota tano ‘brand’ za Kempinski kwenye hifadhi Nne za Taifa nchini.

Waziri Dk. Damas Ndumbaro amesema mpango mkakati wa Mhe Rais Samia Suluhu Hassan kupitia kuandaa kipindi cha Royal Tour umeweza kuzaa matunda hayo na wao kama Wizara wameupokea na sasa ni utekelezaji.

”Juhudi kubwa za kimkakati za Royal Tour zilizoendeshwa na Rais wetu zimeweza kuzaa matunda ambapo leo tumepokea wawekezaji mahiri kutoka Bara la Ulaya ambao watawekeza kwenye hoteli kwa kujenga hoteli za nyota tano za ‘brand’ ya Kempinski  kwa uwekezaji wa Dola za Kimarekani Milioni 72. [USD 72 Milioni].

”Kwa hiyo unaweza kuipata hoteli ya Kempinski baada ya ujenzi huo kukamilika… Kempinski Serengeti,  Kempinski Manyara, Kempinski Tarangile na Kempinski Ngorongoro.” Amesema Dk. Ndumbaro.

Waziri Dkt. Ndumbaro ameongeza kuwa, ujenzi huo ni mkubwa sana  na unakadiriwa kuanza rasmi mwezi Januari 2022 ambapo amemshukuru  kwa mara nyingine Rais kwa kuwezesha kuwapigia ‘pass’ na wao kupitia wizara ya Maliasili ni utekelezaji ikiwemo kupokea Wawekezaji katika sekta hiyo ya Utalii.

”Tunaenda kasi tayari hii Royal tour  kwangu mimi kama Waziri  na Wizara ya Utalii na Maliasili kwa ujumla wake tunaichukulia kama ‘pass’ ya mwisho katika mpira, unapopewa pasi ya mwisho kazi yako wewe ni kufunga tu. Kwa hiyo sisi tumeshafunga ‘Goal’ lingine hilo kuhakikisha kwamba Royal Tour inakuwa na mafanikio zaidi” amemaliza Waziri Dkt.Ndumbaro.

Agosti 28, mwaka huu Rais Samia Suluhu Hassan alianza rasmi kurekodi vipindi vya Royal Tour maeneo mbalimbali ya vuvutio vya utalii na uwekezaji ikiwemo Tanzania Bara na visiwa vya Zanzibar.

Ambapo katika ziara hiyo ya kuandaa vipindi hivyo kutembelea na kuonesha kwa wageni vivutio mbalimbali vya Utalii, Uwekezaji, Sanaa na Utamaduni vilivyopo nchini na vitarushwa duniani kote kupitia vipindi vya Royal tour