May 15, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi kutoka katika maeneo mbalimbali ya Jijini Dar es salaam wakiwa wamefurika wakipata huduma katika Banda la WAKALA wa Usajili Ufilisi na Udhamini(RITA) katika Maonesho 44 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea katika Viwanja vya Julias Nyerere barabara ya Kilwa Road(Picha na Irene Clemence)

RITA yapunguza gharama vyeti vya kuzaliwa

Na Irene Clemence, Times Majira Online, Dar es Salaam

WAKALA wa Usajili Ufilisi na Udhamini(RITA), imefanya punguzo la gharama za vyeti vya kuzaliwa kutoka Sh. 20,000 ya awali na kufikia Sh.10,000 kwa watu wazima huku watoto ikiwa ni Sh.3,500.

Akizungumza katika Maonesho 44 ya Biashara ya Kimataifa maarufu Sabasaba yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julias Nyerere barabara ya Kilwa Road Jijini Dar es Salaam, Ofisa Usajili Mwandamizi kutoka(RITA), Hamisa Kileo amesema idadi ya viambatanisho kwa Sasa imepugua ambapo mtu anaweza kupata cheti kwa kiambatanisho kimoja.

Amesema, wamejipanga kuhakikisha kila mwananchi asiyekuwa na Cheti cha kuzaliwa anamiliki.

Alibainisha kuwa, RITA imejipanga vizuri kusajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa wale wote ambao wamezaliwa Tanzania Bara lakini hawana cheti hicho hivyo tunawasihi wananchi hao wajitokeze kwa wingi katika banda la RITA lililopo hapa viwanja vya Sabasaba .

“Cheti cha kuzaliwa ni nyaraka muhimu inayotumika katika nyanja mbalimbali katika mahitaji ya binadamu kama vile elimu, ajira, kupata mikopo ya elimu ya juu, bima ya afya, pasi ya kusafiria n.k. Hata hivyo cheti hiki kinaonesha utambulisho wa kwanza wa mwananchi mwenyewe kwa maana ya mahali alipozaliwa, majina ya mtoto, majina ya wazazi, tarehe ya kuzaliwa pamoja na ubini wa muhusika,”amesema Kileo.

Naye Ofisa Habari wa Rita Grace Kyasi amesema, uwepo kwa huduma nyingi zinazohitaji mtu awe na cheti cha kuzaliwa imepelekea asilimia kubwa ya wananchi kuona kuwa kuna umuhimu mkubwa wa kuwa na cheti hicho mapema.

Amesema, kwa sasa muitikio ni mkubwa wa wananchi kujitokeza katika banda la RITA ili kupata huduma hiyo.

“Cheti cha kuzaliwa kimekuwa kikitumika kupata huduma mbalimbali kama vile kupata elimu ya msingi, sekondari, kupata huduma ya afya, kupata ajira katika taasisi za Serikali, jeshini na sekta binafsi,”amesema Kyasi.

Kyasi ameongeza kuwa, cheti cha kuzaliwa humpa mtoto haki za kurithi mali za wazazi wake. Alisisitiza Kyasi .

Katika viwanja vya Maonyesho ya Sabasaba mwaka huu, umati wa watu unaendelea kufurika kwa lengo la kutafuta vyeti hivyo na kusababisha banda hilo kujaa watu wakati wote.